Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk.John Jingu,akitoa maelezo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Afisa Mfawidhi Makao ya Taifa ya Watoto Kikombo Tullo Masanja,akitoa maelezo kwa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii iliyofanya ziara ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ,Stanslaus Nyongo,akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima,akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dk.John Jingu,akizungumza mara baada ya kutembelea na kukagua Makao ya Taifa ya watoto yaliyopo eneo la Kikombo nje kidogo ya jiji la Dodoma.
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii imeipongeza Serikali kwa jitihada zake za kupambana changamoto ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu nchini, ikiwemo usimamizi wa makao ya Taifa ya watoto Kikombo.
Akizungumza wakati wa ziara ya Kamati hiyo kwenye makao hayo yaliyopo nje ya jiji la Dodoma, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii Mhe. Stanslaus Nyongo amesema Wizara imefanya jambo kubwa ambalo litasaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu kupata fursa ya kuishi mazingira mazuri na kupata malezi bora.
Mhe. Nyongo ameongeza kwamba Watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani imekuwa ni changamoto kubwa hivyo ameitaka Wizara kuhakikisha inawasaidia watoto hao ili waweze kupata elimu na stadi mbalimbali zitakazowasaidia katika maisha yao.
Aidha ameitaka Wizara kuweka mazingira wezeshi hasa kwa watumishi wa Makao hayo kwani wamejitoa katika kuhakikisha watoto wanapata malezi na makuzi Bora.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo pia ameitaka Wizara kuwahamishia watoto waliopo Makao ya Kurasini Dar Es Salaam kutokana na kukua kwa mji na uwepo wa watu wengi katika eneo hilo hali inayoweza kusababisha watoto kuendelea kuwa katika mazingira hatarishi.
“Muone namna ya kuleta watoto kutoka makao yale ya Kurasini na watoto wengine kwani bado makao haya yana uwezo wa kuchukua watoto wengi zaidi, ni eneo kubwa na zuri sio kwa Tanzania tu inawezekana hata Afrika Mashariki” amesema Mhe. Nyongo.
Pia Mhe. Nyongo amelipongeza Shirika la ABBOTT Tanzania kwa kuona suala la watoto waishio katika mazingira magumu ni muhimu na kuweka fedha kiasi cha shilingi bilioni 2 katika kuhakikisha watoto hao wanakuwa na mazingira mazuri ya kupata malezi na mafunzo mbalimbali.
“Tuwashukuru sana ABBOT FUND kwa usimamizi wa ujenzi wa kituo hiki, kimejengwa kwa hali ya juu. Sisi kama wabunge tumeridhika, kazi kubwa imefanyika. Tumejifunza na tumeona kwa kweli kimeendana na viwango vinavyotakiwa kwa malezi ya watoto. Mngeweza kupeleka fedha popote lakini mkaona umuhimu wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu, asanteni sana.” Alisema Mhe. Nyongo.
Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameihakikishia Kamati hiyo kuwa Wizara itasimamia Makao hayo ili yaweze kutoa huduma kwa Watoto waliokusudiwa kulelewa hapo.
Waziri Dkt Gwajima ameongeza kuwa, watoto kulelewa kwenye makao ni hatua ya mwisho kabisa baada ya kushindikana kuishi kwenye familia zao na kuwataka wazazi kuacha kuwatelekeza watoto wao hali inayowafanya kukimbilia mitaani.
“Nina imani ziara hii imewapa picha ya nini kinaendelea katika ulimwengu wa watoto wanaoishi mtaani hapa nchini na Serikali inafanya nini kukabiliana na hali hii, pia imewapa picha kwamba changamoto bado ni kubwa nchini, huu ni mtihani wa Taifa na Wizara, hivyo Serikali haiwezi kufanya peke yake. Nichukue fursa hii kutambua mchango wa ABBOTT FUND, tunahitaji kuimarisha ushirikiano na wadau hawa,” aliongeza Mhe. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima ameihakikishia Kamati pia kuwa ushauri uliotolewa na wabunge umepokelewa na kuahidi kuufanyia kazi kwa kuanza kuwasilisha mpango kazi mahususi utakaotumika kutekeleza maoni yaliyotolewa na wabunge hao.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema kazi kubwa inayofanyika katika makao hayo ni kufahamu uwezo na vipaji vya watoto na kuwaendeleza kila mmoja kutokana na changamoto zao na waliopo shuleni wanasaidiwa kwa kushirikiana na uongozi wa shule husika.
Akizungumza kwa niaba ya Shirika la ABBOTT FUND Mwakilishi wa Shirika hilo Natalia Lobue amesema Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani katika mazingira magumu wanapata fursa ya kuishi pazuri na kupata elimu na malezi bora.
Nao baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii waipongeza Wizara kwa jitihada za kuhakikisha tatizo la watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani linapungua kama sio kutokomezwa kabisa na kusisitiza elimu kwa jamii ili watambue kuwa watoto hao ni jukumu lao pia kuwasaidia.
No comments:
Post a Comment