Wednesday, August 18, 2021

MBELE YA WABUNGE, WAZIRI MKENDA AWEKA BAYANA MSIMAMO WA SERIKALI KUHUSU MATUMIZI YA (GMO)

Waziri wa Kilimo Mhe. Prof. Adolf Mkenda (Mb)

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma


Serikali imeendelea na msimamo wake kuhusu kupiga marufuku shughuli za utafiti wa mbegu za uhandisi jeni (GMO) hapa nchini huku ikisisitiza ulazima wa kuongeza tija na uzalishaji wa mbegu nchini


Waziri wa kilimo Mhe Prof Adolf Mkenda ametoa kauli hiyo ya serikali leo tarehe 18 Agosti 2021 wakati akizungumza kwenye kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji alipkuwa akijibu swali la Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Dkt Bashiru Ally Kakurwa aliyetaka kufahamu kuhusu msimamo wa serikali matumizi ya GMO.


Uamuzi huo wa serikali umekuja baada ya miaka 10 ya mijadala, upinzani na majaribio ya njia hiyo mpya na ya kisasa ya kilimo.


Kampeni za majaribio ya mbegu za GMO nchini Tanzania zilianza mwaka 2008 chini ya mradi wa Water Efficiemt Maize For Africa (WEMA) unaodhaminiwa na wakfu wa matajiri Bill&Merinda Gates lakini majaribio rasmi yalianza kufanyika mwaka 2016.


Mwaka 2018 Serikali ya Tanzania kupitia kwa aliyekuwa katibu mkuu wa Wizara ya Kilimo Mhandisi Mathew Mtigumwe ilipiga marufuku shughuli za utafiti wa mbegu za uhandisi jeni (GMO) pamoja na kuamuru kuteketeza mazao yote ya aina hiyo ambayo tayari yalikuwa yanafanyiwa tafiti.


Mtigumwe aliamuru kusitishwa kwa majaribio hayo yaliyokuwa yanafanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (Tari) katika kituo chake cha Makutupora mkoani Dodoma.


Mbegu za GMO kutokana uvamizi wake wa kiasili hulazimisha wakulima wengine kuzitumia ili wapate mavuno na kufanya utegemezi wa mbegu hizo kuwa mkubwa.


Hoja kuu za kupinga matumizi ya mbegu hizo za GMO ilikuwa ni kuhusu usalama wa kiafya kwa watumiaji, mazingira na soko la mbegu.


Waziri Mkenda amesema kuwa Katika ulimwengu wa sayansi kuna msuguano mkubwa wa usalama wa kiafya kwa wanaadamu kula vyakula vilivyotokana na mbegu za GMO lakini tatizo kubwa la matumizi ya mbegu hizo ni kuiongeza utegemezi mkubwa wa mbegu ilihali taifa lipo katika mkakati wa kuhakikisha linaongeza uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi.


"Waheshimiwa wabunge wenzangu hakuna sababu ya kuagiza mbegu nje ya nchi maana tuna ardhi nzuri yenye udongo wenye rutuba kwa ajili ya mazao yetu, hivyo wajibu wetu ni kuhakikisha Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI) inaendelea kufanya utafiti wa kina na Mamlaka ya Mbegu (ASA) kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo kuzalisha mbegu bora na kwa wingi" Amekaririwa Prof Mkenda


MWISHO

No comments:

Post a Comment