Thursday, July 8, 2021

DKT MABULA: MARUFUKU KUJENGA KIHOLELA MAENEO YA MIJI

Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kata ya Kiseke juu ya Bajeti mpya ya mwaka wa fedha 2021/2022 na miradi itakayotekelezwa kutokana na bajeti hiyo iliyopitishwa hivi karibuni na Vikao vya Bunge la Bajeti
Wananchi wa kata ya Kiseke waliojitokeza kumsikiliza Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kusikiliza kero na changamoto za wananchi.
Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa kata ya Kahama juu ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo

Wananchi wametakiwa kujenga kwa kufuata sheria, kanuni na taratibu za ardhi na mipango miji pindi wanapotaka kuendeleza maeneo yao hasa yale ya mijini ili kujiepusha na hasara zinazoweza kujitokeza ikiwemo kuvunjiwa nyumba zao kwa kutozingatia matumizi sahihi ya ardhi ya eneo husika.

Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati akizungumza na wananchi wa kata za Kahama na Kiseke  ikiwa ni muendelezo wa ziara yake aliyoianza  mwanzoni mwa wiki kwaajili ya kusikiliza kero za wananchi, kuhamasisha utekelezaji wa shughuli za maendeleo, kukumbusha juu ya uchukuaji wa tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 na kutoa mrejesho wa vikao vya Bunge la bajeti lililoisha hivi karibuni ambapo akawataka wananchi hao kuhakikisha kabla ya kununua eneo na kulifanyia maendelezo kujiridhisha na matumizi sahihi ya ardhi ya eneo hilo kwa kushirikisha ofisi za ardhi za majiji na manispaa za eneo husika, viongozi wa maeneo yao, majirani wa pande zote ili kupunguza migogoro isiyokuwa ya lazima na hasara kwa kuingia gharama zisizo na umuhimu

‘.. Ni marufuku kujenga kiholela katika maeneo yote ya manispaa kwasababu yalishatangazwa kama maeneo ya miji, Huwezi kufanya uendelezaji wowote bila kuwa na kibali, bila kuwa na ramani, bila kuhusisha ofisi zinazohusika ..’ Alisema

Aidha Mhe Dkt Mabula akawataka wananchi kuacha kununua ardhi kiholela kwani kila kipande cha ardhi kimepangiwa matumizi yake huku akiahidi matofali yote yatakayohitajika katika ujenzi wa shule mpya ya msingi mtaa wa Isela wakati wataalamu kutoka taasisi za Tanesco, Tarula na Mwauwasa wakitaja miradi mbalimbali ya maendeleo inayoenda kutekelezwa katika maeneo hayo

Kwa upande wake mwakilishi wa mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Hassan Masala, Afisa Tarafa wa wilaya hiyo Ndugu Godfrey Mzava akamhakikishia ulinzi na usalama ndani ya wilaya hiyo sambamba na kuwataka wananchi kutoa taarifa juu ya vitendo vya kiharifu na kushiriki utekelezaji wa miradi ya maendeleo

Nae mwakilishi wa mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela, Afisa ardhi na mipango miji Ndugu Shukran Kyando amekemea vitendo vya matumizi ya ardhi bila vibali vya manispaa ikiwemo kuendesha biashara ya ufyatuaji wa matofali katikati ya makazi ya watu jambo linalochangia uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha kelele

Moja ya wananchi walioshiriki mkutano huo  Bi Hawa Kiboto mbali na kumpongeza Mbunge Dkt Angeline Mabula kwa ziara hiyo akaomba usimamizi zaidi wa sera ya afya inayotaka mama wajawazito na watoto wa chini ya miaka mitano kuhudumiwa bila gharama pindi wanapohitaji huduma ili kuokoa maisha ya mama na mtoto pindi inapojitokeza dharula

No comments:

Post a Comment