Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Bodi ya nafaka na
Mazao Mchanganyiko (CPB) imeagizwa kushirikiana na Taasisi zingine za Serikali
ikiwemo Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) katika kuimarisha
upatikanaji wa masoko ndani na nje ya nchi.
Agizo hilo limetolewa
tarehe 27 Mei 2021 na Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Ndg Andrew Massawe wakati
alipofanya ziara ya kikazi katika Ofisi za Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko kwa lengo la kufahamiana, na kuzungumza na Menejimenti ikiwa ni kufuatilia utekelezaji wa majukumu unaofanywa na Bodi hiyo katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto ya masoko kwa mazao ya wakulima nchini.
Massawe amesema kuwa CPB na NFRA zinapaswa kuwajibika ipasavyo katika kununua na kuuza mazao ya wakulima ndani na nje ya nchi kwani kufanya hivyo kutaongeza wigo wa masoko ya mazao ya wakulima.
Ameitaka CPB
kujiimarisha zaidi katika kununua na kuuza mazao ya wakulima ikiwa ni pamoja na
kuhakikisha gharama za uendeshaji (operational cost) zinakuwa ndogo, na kwà
kufanya hivyo Taasisi itapata faida na mkulima atapata manufaa Kwà mazao yake
kuwa na uhakika wa soko.
Katibu Mkuu Massawe
amewataka watendaji CPB kutumia muda wao wote wanapokuwa kazini kufikiri
kibiashara kwani Bodi hiyo ni maalumu kwa mujibu wa sheria kwa ajili ya kufanya
biashara ya mazao.
Katika hatua nyingine
Katibu Mkuu Massawe ameagiza watumishi wote wa Taasisi hiyo kuwajibika ipasavyo
ikiwa ni pamoja na kuonyesha ushirikiano maradufu kwani kumekuwa na sintofahamu
baini yao kwa kuchukiana wenyewe kwa wenyewe.
Amesema CPB inapaswa
kuimarisha na kuwa na mahusiano mazuri ya kikazi kwani utekelezaji wa majukumu
ya ufanyaji biashara wanayoifanya inahitaji mahusiano mazuri baina yao.
“Hapa ndani nasikia
mnavurugana sana, hamuwezi kufanya kazi kwa mafanikio kama hakuna maelewano,
Maneno yanakuwa mengi kwanini mnavurugana kwani shida nini ambacho
hakizungumziki, Nawasihi Mkae meza moja na kuzungumza kwanini taasisi inakuwa
na ugomvi na kutokuelewana” Amekaririwa Katibu Mkuu Massawe
Akizungumza kwa niaba
ya wafanyakazi Mkurugenzi wa Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko Dkt Anslem
Moshi amekiri kuwepo kwa sintofahamu baina ya wafanyakazi na kumuhakikishia
Katibu Mkuu huyo jambo hilo kulichukulia hatua za haraka iwezekanavyo.
No comments:
Post a Comment