Tuesday, February 2, 2021

TATIZO LA UMEME SONGWE LAPATIWA MUAROBAINI


Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Medard Kalemani amesema, Serikali imetenga takriban dola milioni 450 kwa ajili ya kujenga kituo cha kupoza umeme Songwe kitakachosambaza umeme Tunduma, Ikana, Laela hadi Kamsamba katika maeneo yote ambayo hayana miundo mbinu ya umeme.

Waziri Kalemani ameyasema hayo tarehe 31 Januari 2021 alipotembelea eneo la Majimoto lililoko wilaya ya Mbozi mkoani Songwe.

Waziri Kalemani ameishukuru Serikali kwa kutenga fedha hizo zitakazowezesha ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Songwe na kutatua tatizo la umeme mkoani Songwe.

Waziri Kalemani amesema, kuna takriban zaidi ya kilomita 2000 za mzunguko katika mkoa wa Songwe ambazo hazina kituo cha kupoza umeme. Waziri kalemani amesema ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Songwe, utamaliza tatizo la umeme kutokuwa wa uhakika katika mkoa wa Songwe.

Waziri Kalemani amesema, utaratibu wa ujenzi umeshaanza na kituo cha kupokea na kupoza umeme kitajengwa karibu na Tunduma na kusambaza umeme kuelekea Katavi na kuunganisha kwenda Kigoma ambapo itaunganisha hadi Geita - Nyakanazi.

Waziri Kalemani amesema, kuna grid inaitwa ‘North West Grid’ na kuwa, ukanda huu haukuwa na Grid ya Taifa na hivyo mkoa wa Songwe kuathirika kwa hilo. Lakini sasa kuna mpango madhubuti wa muarobaini wa kuondokana na kero hiyo na utekelezaji umeshaanza.

Waziri Kalemani amesema, Wizara ya Nishati inakusudia kuwa,  ndani ya miezi 18, hali ya upatikanaji wa umeme mkoani Songwe itakuwa imerekebika na pia katika maeneo tajwa hapo juu.

Akizungumzia Kuhusu usambazaji wa umeme, Waziri Kalemani amefafanua kuwa, kukatika kwa umeme, kunasababishwa na Songwe kutokuwa na njia ya uhakika ya umeme. Amefafanua kuwa, hali ya umeme wa Mbeya na Songwe ni tofauti sana kwani Mbeya hawana shida ya umeme na kuwa kwa sasa mkoa wa Songwe unapata umeme kutoka katika kituo cha kupoza umeme cha Mwakibete, ambacho kina jumla ya MW 150.

Waziri Kalemani ameeleza kuwa, matumizi ya mkoa wa Mbeya peke yake ni MW 75 na mkoa wa Songwe ni MW 15 kwa sasa, kwa hiyo umeme ulioko Mbeya, unatosha kutoa umeme kwa mikoa ya Mbeya na Songwe na kubakiza takribani MW 68.  Amesema, shida iliyopo ni njia ya kuusafirisha umeme huo ambayo ndiyo inajengwa na ni ndefu kwa kilomita za mzunguko 2010 na ndiyo maana kukosekana kwa kituo cha kupoza umeme kunasababisha tatizo la kukatika kwa umeme katika mkoa wa Songwe.

Amefafanua kuwa kutokana na njia ya umeme kuwa ndefu, kunahitilafu nyingi zinazotokea njiani na kusababisha kukatika kwa umeme lakini umeme unaozalishwa katika kituo cha Mwakibete unatosha kutoa umeme kwa Mikoa ya Mbeya na Songwe na kuwa na ziada.

Akizungumzia kuhusu usambazaji wa umeme kwenye vijiji vya mkoa wa Songwe, Dkt. Kalemani amekumbushia kuwa, wakati mpango wa kupeleka umeme vijijini unapangwa mwaka 2008, mkoa wa Songwe ulikuwa sehemu ya mkoa wa Mbeya na vijiji vingi vilivyopelekewa umeme, vilikuwa ni vijiji vilivyokuwa karibu na mkoa wa Mbeya.

Amesema, Mbeya ina vijiji takriban 502 lakini vijiji vilivyobakia kuunganishiwa na huduma ya umeme ni vijiji 91 tu na Mbeya ina vijiji vingi kuliko Songwe yenye vijiji vipatavyo zaidi ya 300 hadi 500. Lakini bado Songwe kuna vijiji 120 lakini vilikuwa pembeni sana na wakati huo kwenye mradi wa REA wa kupeleka umeme vijijini, Mbeya iliangaliwa kama mkoa wa Mbeya wakati huo Songwe haukuwa mkoa. Hivyo Songwe ilivyokuwa mkoa, ikaangukiwa na vijiji vichache vilivyokuwa kwenye mradi, lakini sasa muarobaini wake umepatikana.

Waziri Kalemani amemfahamisha Mkuu wa mkoa wa Songwe kuwa, Serikali imetoa jumla ya bilioni 851 kwa nchi nzima, kupeleka umeme katika vijiji vyote ambavyo bado havijaunganishiwa na huduma ya umeme.

Amesema, vijiji vyote vya Songwe vilivyobaki tayari viko kwa wakandarasi na Songwe imepatiwa wakandarasi wawili ili kuharakisha usambazaji wa umeme katika vijiji vya Songwe. Dkt. Kalemani amesema, utaratibu wa kuleta umeme kwenye vijiji hivyo, unaanza tarehe 02 Februari, 2021.

Waziri Kalemani ameweka bayana kuwa hapa Tanzania, kuna vijiji 12,268 lakini vijiji 10,109 tayari vina umeme ambapo ni vijiji 2059 tu ambavyo ni pamoja na maeneo ya vijiji vya Songwe na vitongoji ambavyo bado havijapelekewa huduma hiyo. Amesema vijiji vyote hivyo vitafikishiwa umeme ndani ya miezi 18 kuanzia tarehe 05 Februari, 2021.

Waziri Kalemani amebainisha kuwa Serikali imefanya kazi kubwa kwani wakati Serikali ilipoanza kupeleka umeme vijijini mwaka 2015 vijiji vilivyokuwa na umeme vilikuwa ni vijiji 2000 tu. Lakini leo vijiji vyenye umeme hapa nchini ni vijiji zaidi ya 10,000 vilivyounganishiwa na huduma ya umeme ndani ya miaka mitano.

Amesema kazi ya kupeleka umeme katika vijiji vilivyobakia itakamilika ndani ya muda mfupi.

Waziri Kalemani ametoa wito kwa wakandarasi watakaopewa kazi ya kupeleka umeme vijijini, kuhakikisha wanafanya kazi hiyo ipasavyo na kukamilisha upelekaji wa huduma ya umeme kwenye vijiji na vitongoji ndani ya vijiji hivyo, inakamilika chini ya miezi 18.

Amesema baada ya hapo suala la kijiji katika nchi yetu kuwa hakina umeme litakuwa ni historia.

Aidha Waziri kalemani amesema, upelekaji wa umeme kuanzia sasa utakuwa shirikishi, ambapo Mkandarasi anapoingia kwenye maeneo ya wananchi, ataanza kuwaona viongozi wa maeneo husika ili wapewe maeneo ya vipaumbele kuhakikisha, maeneo muhimu kama taasisi za umma, yanapata umeme kwa haraka.

Dkt. Kalemani amewaomba viongozi wote wa taasisi zote, kuainisha maeneo yote ya kitaasisi ili wakandarasi wa REA wanapoanza kazi ya kuunganisha umeme, waanze na maeneo hayo kama maeneo ya vipaumbele.

“Unapopeleka umeme kwenye kituo cha afya, unahudumia zaidi ya wananchi 300 kwa mkupuo. kwa hivyo nitoe rai kwa wananchi, viongozi na wakandarasi wa mradi, kuzingatia maeneo ya kitaasisi kama kipaumbele.” Amesema Dkt. Kalemani.

Akizungumzia kuhusu kuhusu Mradi wa Umeme wa Jotoardhi ‘Geo Thermo’ amesema, hapa nchini tuna rasilimali, tuna uwezo na tuna vyanzo vingi vya umeme wa Jotoardhi na ndiyo maana Wizara ya Nishati imeanza kuvitembelea ili vifahamike vema.

Amesema, katika Mikoa ya Mbeya na Songwe pekee, tunayo miradi inayoweza kuzalisha zaidi ya MW 165 za Jotoardhi na kuna maeneo mengine kama vile Natron (Arusha), Luhoi (Pwani) na Kiejo Mbaka (Mbeya), Ngozi (Mbeya) pamoja na Songwe ( Songwe).

“Kwa ujumla hifadhi ya jotoardhi iliyopo hapa nchini inao uwezo wa kuzalisha zaidi ya MW 5000 katika miaka 10 ijayo tukijipanga vizuri.” Amesema Dkt. Kalemani.

Amesema kwa kuanzia Wizara ya Nishati itaanza na MW 200 ambazo zitaanza kupatikana katika eneo la Majimoto lililopo katika mkoa wa Songwe ambapo kwa kuanzia litazalisha MW 5 hadi MW 38. na pia yapo maeneo mengine.

“Tunaanza na megawati 200 mojawapo ikiwa ni kutoka katika mradi huu wa jotoardhi Songwe, huku eneo hili peke yake likiwa na uwezo wa kuzalisha megawati 5 hadi 38.” Amesema Dkt. Kalemani.

“Tanzania licha ya kuwa na jumla ya megawati 1602 kwa sasa, lakini bado hatuna hata megawati moja ya jotoardhi, ndio tunataka sasa tuharakishe.”  amesema Waziri Kalemani

Waziri Kalemani, amemtaka Meneja Mkuu wa kampuni ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC), kuharakisha utengenezaji wa miundombinu itakayowezesha upatikanaji wa umeme unaotokana na Jotoardhi haraka na kumtaka kutumia miaka miwili kuanzia sasa kuanza kuzalisha umeme wa Jotoardhi usiopungua MW 200 kutoka kwenye vyanzo ili nchi ianze kunufaika na umeme wa nishati wa jotoardhi.

 “Ningependa kuipongeza Serikali yetu kwa kutupatia shilingi bilioni 20 mwaka jana ili kuhakikisha miradi hii inatekelezwa,” amesema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani ameongeza kuwa, hadi sasa jumla ya shilingi bilioni 1.029, zimetumika katika uendelezaji wa shughuli za nishati ya jotoardhi katika Mradi wa Songwe.

Amesema, wakati shughuli za uendelezaji wa nishati ya jotoardhi katika kuzalisha umeme zinaendelea tayari TGDC imefanya jitihada kwa kutengeneza fursa ya kutumia nishati ya jotoardhi kutotolesha vifaranga, kufugia samaki, shughuli za utalii, kukaushia mazao na shughuli nyingine.

“Niwapongeze sana TGDC kwa kutumia nishati ya jotoardhi kuzalisha umeme ukawa na manufaa mengine kwa jamii. Ni jambo zuri,” amesema Waziri Kalemani.

Amefafanua kuwa ili uweze kuzalisha umeme wa nishati ya jotoardhi kunahitajika nyuzi joto 100 hadi nyuzi joto 140, lakini joto linalopatikana kwa sasa ni nyuzi joto 70 mpaka 80 ambalo ndilo linalofaa kwa matumizi mengine ya nishati hiyo.

Waziri Kalemani ameitaka TGDC kuwashirikisha wananchi ili waweze kunufaika na fursa ya uwepo wa nishati ya jotoardhi katika maeneo yao. 

Kwa upande wake, Meneja Mkuu TGDC, Mhandisi Kato Kabaka ameeleza kuwa licha ya TGDC kuendelea na uendelezaji wa nishati ya jotoardhi katika uzalishaji wa umeme, kuna teknolojia ambazo zimebuniwa na TGDC zikiwa na lengo la kuchangia katika shughuli za kiuchumi nchini.

“Mpaka sasa tumebuni teknolojia ya utotoleshaji vifaranga kwa kutumia nishati ya jotoardhi, kifaa cha kudhibiti joto la maji moto na kifaa cha kukusanya taarifa za utafiti wa nishati ya jotoardhi.” Ameeleza Mhandisi Kabaka.

Ameongeza kuwa shughuli za utafiti wa kina wa nishati wa jotoardhi katika miradi ya kipaumbele ya kuzalisha umeme zinaendelea na kwa sasa TGDC imefikia hatua ya uchorongaji visima vya jotoardhi ili kuhakiki kiwango cha hifadhi halisi ya jotoardhi iliyoko chini ya ardhi.

No comments:

Post a Comment