Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo (kulia) akisisitiza jambo kwa Naibu Balozi wa Uholanzi nchini Tanzania Bibi Lianne Houben ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka nchini Uholanzi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo
(kushoto) akipokea kitabu kinachoeleza
masuala mbalimbali kuhusu nchi ya Uholanzi kutoka kwa Naibu Balozi wa Uholanzi
nchini Tanzania Bibi Lianne Houben mara baada ya mazungumzo yao leo Jijini
Dodoma kuhusu masuala ya uwekezaji.
Umoja wa Ulaya umeahidi kuendelea kuiunga
mkono Serikali ya Tanzania katika jitihada za kuimarisha mazingira ya biashara
na uwekezaji nchini ikiwa ni pamoja na kuvutia wawekezaji wengi zaidi kutoka
nchi za Umoja wa Ulaya kuja kuwekeza hapa nchini.
Hayo
yamesemwa Januari 22, 2021 Jijini Dodoma na Mhe. Manfred Fanti, Balozi wa
Umoja wa Ulaya nchini Tanzania alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Rais anayeshughulikia Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo.
“Nimekuwa nikisikia ushuhuda kutoka kwa
wawekezaji wengi wanaotoka nchi za Umoja wa Ulaya kuwa wanapata faida katika
uwekezaji wao hapa nchini na nikiwa kama mwakilishi wa Umoja wa Ulaya nchini
Tanzania ni jukumu langu kuhakikisha kuwa nashirikiana ipasavyo na Serikali ya
Tanzania kuvutia wawekezaji wengi zaidi kuwekeza Tanzania”, alisema Mheshimiwa
Balozi Fanti.
Aliongeza kuwa, Umoja wa Ulaya unatambua
jitihada zinazoendelea kufanywa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi
wa Rais Dkt. John Pombe Joseph Magufuli katika kuboresha mifumo ya kisheria,
kisera na ya kitaasisi ili kuweka mazingira rafiki zaidi yatakayovutia
wawekezaji na hivyo wako tayari kuendelea kuiunga mkono Serikali ili kufanikisha
lengo hilo.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Kitila
Mkumbo na Balozi Fanti walijadili pia maeneo bayana ambayo Tanzania na Umoja wa Ulaya wanaweza
kukuza ushirikiano wa uwekezaji ikiwemo
katika sekta ya uzalishaji nguo, uchimbaji na uchakataji wa madini, uchakataji
wa mazao ya mifugo na uvuvi, uzalishaji wa nishati.
Vilevile Waziri Mkumbo aligusia baadhi ya
maeneo ya kimkakati ambayo tayari Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali
imeweka nguvu kuyatekeleza ikiwemo kuandaa na kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Uwekezaji, utekelezaji wa
programu ya kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara (ROADMAP) pamoja na kuandaa mfumo kabambe wa ukusanyaji takwimu za
uwekezaji nchini.
Aidha, Alimweleza Balozi huyo kuwa hayo ni
baadhi ya maeneo ambayo Serikali ipo tayari kuendelea kushirikiana na Umoja wa
Ulaya, ili pamoja na mambo mengine, kumaliza kabisa changamoto zinazowakabili
wawekezaji wa kigeni hapa nchini.
Kwa upande mwingine Waziri huyo wa
Uwekezaji alikutana pia na Bibi Lianne Houben, Naibu Balozi wa Uholanzi nchini
Tanzania ambapo katika mazungumzo hayo walijadili na kukubaliana maeneo
mbalimbali yanayoweza kuboreshwa ili kuvutia wawekezaji wengi zaidi, hususani
wanaotoka nchi ya Uholanzi. Baadhi ya maeneo hayo ni pamoja na kuweka mfumo
mzuri wa kuziwezesha Taasisi mbalimbali Wezeshi zinazohudhumia wawekezaji
kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi huku zikizingatia maslahi mapana ya
wawekezaji, pamoja na suala la uhaba wa wafanyakazi wenye ujuzi na fani
mbalimbali ambazo wawekezaji wanazihitaji.
Uholanzi ni moja ya nchi zinazoongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi nchini Tanzania waliowekeza katika sekta za mbalimbali kama vile Kilimo (kwa mfano makampuni ya maua yaliyowekeza Mikoa ya Arusha na Kilimanjaro), huduma za kifedha (kwa mfano Benki ya NMB), Viwanda (kwa mfano Kampuni Unilever na Heineken), usafirishaji (kwa mfano Kampuni ya KLM). Takwimu zinaonesha kuwa takribani miradi 161 ya kutoka Uholanzi imesajiliwa katika za Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ikiwa na mitaji yenye jumla ya thamani ya Dola za Marekani biilioni 1.1 na kutoa ajira 13,995.
No comments:
Post a Comment