Waziri wa
Nishati Dkt. Medard Kalemani, ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO)
mkoani Dodoma kuwa, ndani ya kipindi cha miezi sita kuanzia sasa, Vijiji na
maeneo yote ya mkoa huo yawe yamepata umeme, kuunganisha na kuwawashia wateja,
atakayeshindwa kutekeleza hilo atakuwa amejifukuza kazi mwenyewe.
Dkt.
Kalemani alisema hayo, wakati wa mkutano wake na wafanyakazi wa TANESCO wa Mkoa
wa Dodoma, wenye lengo la kufahamiana, kusikiliza changamoto zinazowakabili
wafanyakazi hao pamoja na kutoa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi wa shirika
hilo uliofanyika Januari 22, 2021 mkoni humo.
Aliwaeleza
wafanyakazi hao kuwa, wao ndiyo wenye dhamana na jukumu kubwa la kuhakikisha
kuwa Mkoa wa Dodoma unapata umeme wa kutosha na wa uhakika katika maeneo yote,
kuunganisha na kuwawashia wateja.
Dkt.
Kalemani alisisitiza kuwa, mkoa huo kwa sasa una wakazi wengi sana na bado
wanaendelea kuongezeka kwa kuwa ni Makao Makuu ya Nchi, umeme mwingi
unahitajika katika shughuli mbalimbali, hivyo lazima kila mfanyakazi awe sehemu
ya shirika hilo na afanye kazi kwa kasi zaidi, ubunifu mkubwa na kwa usahihi
ili kukidhi mahitaji ya umeme na kuboresha zaidi huduma zitolewazo na shirika
hilo.
“Sitakubali
kupata aibu ya baadhi ya maeneo na Vijiji vya Makao Makuu ya Nchi, kutokuwa na
umeme, mkoa huu unazaidi ya Megawati 400 za umeme, lakini matumizi ni Megawati
45 tu kwa sasa, wakati kuna wateja wengi ambao wanahitaji umeme na maeneo
mengine bado hayajafikiwa kabisa na huduma hiyo,TANESCO Dodoma fanyeni kazi!”, alisisitiza Dkt.
Kalemani.
Hata hivyo
alitoa siku 14, kwa shirika hilo mkoani humo kumfikishia taarifa ya namna
walivyojipanga katika kusambaza umeme kwa wananchi, kuunganisha wateja wa
zamani na kupata wapya, kuzalisha na kusafirisha umeme katika maeneo mbalimbali
nchini.
Vile vile
alipiga marufuku kwa baadhi ya watumishi wenye tabia ya kuchelewesha majalada
ya kazi, kwa kusema kuwa vitendo hivyo vinachelewesha utendaji kazi na
kutotimiza malengo kwa wakati.
Alisisitiza
kuwa, asilimia kubwa ya utendaji kazi katika ofisi hufanyika kwa mfumo wa
maandishi kupitia majalada, endapo mmoja atachelewa au kukwamisha, kazi husika
itachelewa na kutotekelezeka kwa muda uliopangwa.
“Ni mwiko
na marufuku kukaa na jalada mezani zaidi ya siku moja ofisini, kama huwezi
kulifanyia kazi sema au upeleka kwa wanaoweza kulifanyia kazi, tunataka kazi
ziende haraka na kwa wakati, ukiona huwezi kufanya kazi kwa kasi hii ninayotaka
ni bora uondoke ofisini! Alisema Dkt.Kalemani.
Katika
hatua nyingine, Dkt. Kalemani aliiagiza
TANESCO, kuangalia upya utaratibu wa kuajiri au kuwapa kazi wafanyakazi wa muda
maalum( STE) ambao muda mwingi wanakuwepo maeneo kazi (Site) kufanya kazi za
kuchimba mashimo, kusimika nguzo na kuvuta nyaya.
Aidha
alitaka STE wasiokuwa na mikataba wapewe mikataba, wenye sifa ya ajira
waajiriwe na wale wasiokuwa na sifa na wamefanya kazi muda mrefu, wapewe
mafunzo maalum ili wapate ajira.
Pia alitaka
shirika hilo kuboresha maslahi wa wafanyakazi hao na kuangalia namna bora ya
kuwapa motisha sehemu za kazi waweze kufanya kazi zao kwa furaha, amani na
utulivu na kuboresha utendaji kazi wao.
Sambasamba
hilo, alitoa miezi miwili kwa wapimaji na watathmini ( Surveyor) pamoja na
watoa namba (Control Number) kwa wateja kwa ajili ya kulipia gharama za
kuunganishiwa umeme, kubadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia weledi na
taaluma zao, na atakayeshindwa kufanya hivyo afukuzwe kazi.
Dkt.
Kalemani aliweka wazi kuwa watumishi wa vitengo hivyo wamekuwa wakilalamikiwa
kwa kutotekeleza majukumu yao kwa wakati na kuchelewa kutoa huduma kwa wateja.
Aidha
aliliagiza shirika hilo kuwapatia pikipiki wafanyakazi wote wa kitengo tathmini
na upimaji kurahisisha utendaji kazi wao.
Akizungumzia
kitengo cha huduma kwa wateja, Dkt. Kalemani alitaka wahusika kutumia lugha
rafiki na zinazofaa kwa wateja, kuweka watoa huduma vijana ili waweze kufanya
kazi kwa kasi na haraka zaidi.
“Vitengo
hivi vinalalamikiwa sana, wanatakiwa kubadilika, unakuta mteja amejipanga na
yupo tayari kupata huduma, lakini mtathimi hafanyi kazi yake, halikadhalika na
mtoa namba, ukija huduma kwa wateja anatumia lugha ya mbaya, jamani badilikeni
la sivyo mtajifukuza kazi wenyewe”, alisema Dkt. Kalemani.
Akizungumia
zoezi la kuwaunganishia umeme wateja, Dkt. Kalemani alisema wateja wote
wanaohitaji umeme waunganishiwe kwa gharama halisi zilizoelekezwa na Serikali,
marufuku kwa mteja kulipa zaidi ili apate huduma hiyo kwa haraka na mapema
zaidi ya wenzake, kufanya hivyo ni kutoa Rushwa.
Alisema kuwa kuanzia mwezi Februari serikali itaanza kusambaza na kuunganisha umeme kw vijiji vyote nchini vilivyosalia na kazi hiyo itafanyika kwa kipindi cha miezi 18.
No comments:
Post a Comment