Kufuatia kuendelea kuwepo kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Vyuo vya Elimu na Juu na Vyuo vya kati, Serikali imewakutanisha wawakilishi kutoka baadhi ya Vyuo Vikuu nchini kujadiliana na kutafuta mwelekeo sahihi katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia vyuoni.
Kikao kazi hicho ambacho kimefanyika jijini Dar Es Salaam kimewakutanisha baadhi ya wawakilishi wa Wakuu wa vyuo na wahadhiri mbalimbali kwa lengo la kutafuta mwarobaini wa tatizo la unyanyasaji wa kijinsia vyuoni.
Akimwakilisha Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Mboni Mgaza amesema katika maeneo mengi ya Vyuo, Waathirika wakubwa wa vitendo hivi vya ukatili wamekuwa ni Wanafunzi wa kike kutokana na unyonge wao na hivyo kushindwa kupambana na vitendo hivyo.
Amesema kutoka na changamoto hizo, Serikali imeandaa Mwongozo wa utaratibu wa uanzishaji na uendeshaji wa dawati la jinsia katika Vyuo vya Elimu ya Juu na vya Kati litakaloleta chachu ya mabadiliko ya uelewa na ujasiri wa utoaji wa taarifa za vitendo vya ukatili zinzofanyika katika Taasisi za Elimu ya Juu.
“Mwongozo huu utaimarisha mfumo wa kushughulikia na kutokomeza Ukatili wa kijinsia pamoja na kuzingatia uingizwaji wa masuala ya jinsia katika Mipango, Bajeti, mikakati na program za Vyuo.” alisema
Ameongeza kuwa Serikali inatambua kuwa sekta ya elimu ina mchango mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya Taifa na kutambua hilo mkazo mkubwa umekuwa ni kuimarisha elimu kuanzia ngazi ya Msingi hadi Chuo Kikuu kwa kupambana na vitendo vya Ukatili wa kijinsia katika Taasisi hizo za Elimu.
“Tunatarajia kuwa kupitia Mwongozo huu wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Kati utatoa kipaumbele katika masuala ya jinsia, ikiwa ni pamoja na kuwa na takwimu mbalimbali zilizoanishwa kijinsia na mipango mahususi ya kuondoa tofauti za kijinsia.”
Kwa upande wake, Mkuu wa Taasisi ya Ustawi wa Jamii Dkt. Joyce Nyoni amesema Vitendo vya Ukatili dhidi ya Wanafunzi walioko Vyuoni ni suala lisilokubalika katika jamii yetu ya Tanzania kwa kuwa vinarudisha nyuma jitihada za Serikali katika uboreshaji wa Elimu kwani waathirika wa ukatili hupata madhara ya kimwili, kisaikolojia na wakati mwingine hulazimika kurudia mwaka au kushindwa kuendelea na masomo.
Ameongeza kuwa kama Taasisi ya Ustawi wa Jamii watashirikiana na Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii kuhakikisha Mwongozo huo unafanyiwa kazi kwa Taasisi za Elimu ya juu kwa kuanzishwa kwa madawati ya Jinsia.
Baadhi ya Washiriki kutoka vyuo kutoka Chuo Kikuu Ardhi, Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine, Chuo Kikuu Kishiriki cha Sayansi za Tiba Muhimbili na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam wamesema Muongozo huo unaoletwa utakuwa mwanzo mzuri wa kuwa na Madawati ya Jinsia yenye nguvu katika Taasisi za Elimu ya Juu.
Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii inaanda muongozo wa uanzishwaji wa Madawati ya Jinsia katika Taasisi ya Elimu Juu utakowezesha kuwa na namna sahihi ya uwazishwaji wa madawati ya Jinsia katika Vyuo Vikuu na Vyuo vya Kati nchini.
No comments:
Post a Comment