Tuesday, December 15, 2020

NAIBU WAZIRI WA ARDHI DKT MABULA AFANYA ZIARA YA KUSHTUKIZA OFISI YA KAMISHINA WA ARDHI MWANZA

Naibu waziri wa wizara ya ardhi, nyumba na maendeleo ya makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amefanya ziara ya kushtukiza katika ofisi ya kamishina wa ardhi mkoa wa Mwanza ili kufuatilia maduhuri ya serikali, kukagua utendaji kazi wa makampuni binafsi yanayoendesha zoezi la urasimishaji wa makazi, umilikishaji na utoaji hati miliki kwa wananchi.

Akizungumza ofisini hapo, Naibu Waziri Dkt Angeline Mabula amesema kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia namna zoezi la utoaji hati linavyoendeshwa kwa kusuasua na kuchukua muda mrefu tofauti na inavyoelekezwa sanjari na kutoridhishwa na kazi ya urasimishaji makazi iliyokaimishwa kwa makampuni binafsi ya upimaji kwani yamekuwa yakikusanya fedha za wananchi huku kasi ya upimaji na umilikishwaji ikiwa ndogo ukilinganisha na mwitikio wa wananchi ambapo ametoa mwezi mmoja kwa kamishina huyo wa ardhi ahakikishe anashughulikia kero hizo

‘.. Lengo la Serikali ni kukusanya kodi msipowamilikisha tunakusanyaje hiyo kodi, Lakini wananchi wanachanga fedha zao alafu makampuni hayatoi huduma, Naelekeza kampuni zote zilizochukua fedha za wananchi na hakuna kilichofanyika yapelekwe kwenye vyombo vya sheria ..’ Alisema

Aidha Dkt Mabula akakemea makusanyo hafifu ya kodi ya ardhi ambapo kwa mujibu wa bajeti kiasi cha shilingi bilioni 2 kinategemewa kukusanywa kwa mkoa wa Mwanza lakini mpaka sasa jumla ya shilingi milioni 50 pekee ndio iliyokusanywa kutokana na mwitikio hafifu wa wananchi wakati Serikali imetoa milioni 30 kwaajili ya kuendesha vipindi vya redio na luninga vya uhamasishaji wa ulipaji kodi kwa wananchi.

Kwa upande wake kamishina msaidizi wa ardhi mkoa wa Mwanza Ndugu Biswalo Makwasa mbali na kuahidi kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri huyo,  Akaongeza kuwa ziara hiyo imesaidia kuboresha utendaji wao wa kazi sambamba na kuongeza kuwa mpaka sasa Ilani 10,000 zimekwisha sambazwa kwa wadaiwa hivyo maagizo yamekuja wakati muafaka na yamewaongezea kasi

Nae msajili wa hati msaidizi mkoa wa Mwanza Ndugu Ivan Amurike akataja changamoto zinazochangia kupunguza kasi ya utoaji hati na ukusanyaji wa maduhuri ya Serikali ikiwemo kutojitokeza kwa wamiliki wa ardhi kuchukua hati miliki pindi zinapokamilika.

No comments:

Post a Comment