Thursday, November 19, 2020

Waziri Mkuu aridhishwa na kasi ya ujenzi wa JNHPP, azipongeza Wizara ya Nishati na TANESCO





Na Zuena Msuya, Pwani

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa bwawa la kuzalisha umeme kwa kutumia maporomoko ya maji ya Bonde la Mto Rufiji Mkoani Pwani.

Aidha ameipongeza Wizara ya Nishati pamoja na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kwa hatua waliofikia katika ujenzi wa bwawa hilo na kuwaasa kuongeza kasi ili kukamilisha mradi huo ndani ya muda uliopangwa au hata kabla ya muda huo.

Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akizindua uchepushaji wa maji ya mto Rufiji kupitia handaki ili kuruhusu ujenzi wa tuta kubwa la kuzuia ya bwawa yatakayozalisha umeme, Novemba 18, 2020, mkoani Pwani.

Akizungumzia utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo, Majaliwa alisema kuwa mradi huo ni mkubwa, wa kimkakati na aina yake  katika ukanda wa Afrika ambapo unashika nafasi ya nne kwa ukubwa, pia ni wa kwanza kwa Afrika Mashariki na kusini.

Vilevile alisema kuwa serikali imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha ujenzi wa mradi huo unatekelezeka, pia utarahisisha upatikanaji wa umeme mwingi, wakutosha na kwa gharama nafuu ili kuboresha hali ya uchumi wa kila mtanzania kwa lengo la kuchochea maendeleo ya uchumi ya nchi.

Hivyo aliendelea kuwasisitiza wasimamizi wa mradi huo kufanya kazi zao kwa weledi, uzalendo na kuweka mbele maslahi mapana ya taifa, na kwamba wahakikishe makubaliano ya kutekeleza miradi ya kijamii kama ilivyoelekezwa katika mkataba inakamilika.

Aliweka wazi kuwa, serikali inaugharamia mradi huo kwa asilimia 100, hadi sasa tayari mkandarasi ameshalipwa shilingi Trilioni 1.57  kulingana na kazi zilizofanyika: Mradi huo unatarajiwa kugharimu shilingi Triloni 6.55 hadi kukamilika kwakwe.

“Watanzania tujivunie kwa kuwa na mradi huu, tutembee kifua mbele kwa kuweza kutekeleza mradi huu, nawahakikishia kuwa mahusiano kati yetu na makampuni yanayotekeleza mradi huu ni mazuri, hatuna deni lolote kwa hatua iliyofika mpaka sasa katika mradi huu”, alisema.

“Natoa wito kwa wataalamu wetu wa ndani kutumia fursa hii ya kujengewa uwezo, kujifunza kila wanachokifanya watalaamu kutoka nje ili waje kusaidia katika miradi mingine”, alisisitiza Majaliwa.

Hata hivyo alisema kuwa mradi huo utakapokamilika utawezesha taifa kuongeza mapato yake kwa kuongeza shughuli za kiuchumi,pia kufanya biashara ya umeme kwa nchi jiraji na zenye uhitaji, na kukuza zaidi uchumi wa viwanda kwa kuwa umeme utakuwa mwingi na wakutosha na bei nafuu.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Mhandisi Zena Said alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo utaenda sambasamba na utekelezaji wa miradi ya kijamii katika vijiji vilivyo karibu, katika mkoa wa Pwani na Morogoro kwa lengo la kujenga mahusiano mazuri na wananchi.

Mhandisi Said alisema tayari mradi huo umeshatoa ajira za moja kwa moja 6,364, ambapo watanzania 5,728 wamenufaika na ajira hizo.

Aidha mkandarasi atatekeleza miradi miwili ya kijamii ambayo ni ujenzi wa barabara yenye urefu wa Kilometa 41 kutoka stesheni ya treni ya Fuga hadi katika eneo la mradi na ujenzi wa kiwanja cha cha kisasa cha michezo kinachotarajiwa kujengwa mkoani Dodoma.

Kwa upande wake, aliyekuwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani aliishukuru serikali ya awamu ya Tano kwa kuridhia na kutoa fedha za kutekeleza ujenzi wa mradi huo bila vikwazo vyovyote hadi hapo ulipifikia huku shughuli za ujenzi zikiendelea kwa kasi inayoridhisha.

Hata hivyo aliwashauri wasimamizi na wakandarasi wanaotekeleza  mradi huo kufanya kazi kwa bidii na maarifa , huku wakijua kuwa mradi huo ni kwa manufaa ya watanzania na taifa kwa ujumla, vilevile utasaidia nchi zingine kwa kuwa umeme utakaozalishwa hapo utatumika kwa shughuli mbalimbali zikiwemo viwanda ambavyo baadhi vinamilikiwa na wageni kutoka nje.

Aliwahamasisha wawekezaji kutumia firsa hiyo kuja kuwekeza zaidi nchini kwa kuwa kutakuwa na umeme wa kutosha, wa uhakika na gharama nafuu kuweza kuendesha shughuli za kiuchumi kwa faida zaidi, na pia Tanzania ina sera nzuri na bora za kuwavutia wawekezaji katika Nyanja mbalimbali za kiuchumi.

No comments:

Post a Comment