Hivi karibuni Rais John Pombe Magufuli amezindua Bunge la 12 la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kufuatia ushindi wa kishindo alioupata katika uchaguzi wa mwezi Oktoba, ambapo alichaguliwa kuiongoza nchi kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Katika
hotuba yake ya uzinduzi, Rais Magufuli alionyesha dira, falsafa, mwelekeo na
vipaumbele vya nchi katika kipindi cha uongozi wake wa miaka mitano. Pamoja na
mengi aliyozungumzia , Rais aliahidi kuboresha vitambulisho vya wajasiriamali
ili waweze kutambulika rasmi na kuweza kupata mikopo katika taasisi za fedha
hapa nchini.
Rais
Magufuli alisema kuwa, kama alivyoahidi wakati wa kampeni kwamba katika kipindi
cha uongozi wake wa miaka mitano ijayo, Serikali itaendelea kuboresha mazingira
ya kufanya biashara kwa wajasiriamali wadogo, machinga, mama lishe, baba lishe
waendesha boda boda na bajaji.
Tangu
ilipoingia madarakani, Serikali ya Awamu ya Tano ilianza kuwatambua rasmi
wajasiriamali wadogo nchini pote kwa kuwapatia vitambulisho ambavyo vilikuwa
vinalipiwa shilingi 20,000 kwa mwaka. Utambuzi huo uliwapa uhuru wajasiriamali
hao wadogo kufanya biashara zao bila kubugudhiwa na mtu au mamlaka yoyote hivyo
kujiongezea kipato.
Vitambulisho
hivyo vya awali vilitolewa na Rais Magufuli mwaka 2018, ambapo jumla ya
vitambulisho 670,000 vilitolewa na kuwawezesha wafanyabiashara ndogo ndogo
kutambulika nchini na kuhakikisha wanafanya shughuli zao bila kusumbuliwa na
kama ilivyokuwa awali ambapo walikuwa wanasumbuliwa sana na mamlaka mbalimbali
za miji na halmashauri.
Katika
utaratibu wa awali, kila mkoa ulipewa vitambulisho 25,000, ambapo kila
mjasiriamali aliyekihitaji alikilipia na pesa ilipelekwa TRA na vilikuwa
vinatolewa kwa hiari. Utaratibu huo ulimwezesha kila Mkuu wa Mkoa kukusanya
shilingi milioni 500 ambazo ni mchango wa sekta hiyo ya wafanyabiashara.
“Miaka
mitano iliyopita tulianzisha utaratibu wa kutoa vitambulisha maalum kwa
wajasiriamali wetu wadogo, tunakusudia kuviboresha vitambulisho hivyo kwa
kuweka picha na taarifa nyingine muhimu kama ilivyo kwenye vitambulisho vya
Taifa (NIDA) na kwenye Hati za kusafiria(Pasipoti)”, alisema Rais Magufuli.
Kuboreshwa
kwa vitambulisho hivyo kutakuwa ni fursa nyingine muhimu kwani wataweza kukua
na kutajirika na kuondokana na dhana ya kuwa wafanyabiashara wadogo ambapo hii
itawezekana kwa sababu wataweza kutambulika kwenye taasisi za fedha na kuweza
kupata mikopo kwa ajili ya kukuza biashara.
Aidha,
kutokana na maboresho hayo wajasiriamali hao wataweza kukuza mitaji yao kwa
kuwa sasa watakuwa na uwezo wa kukopa na kuweza kupanua biashara zao nchi
nzima. Hivyo ni wakati muafaka kwao kukuza na kupanua biashara zao kwa sababu
ya uwezo wao wa kuongeza mtaji utakuwa umerahisishwa.
Endapo
wajasiriamali hao wataitumia fursa hii ipasavyo
mbali na kuweza kupata mikopo ya biashara , wataweza pia kupata mikopo
mikubwa ambayo itawanasua katika umaskini ikiwa ni pamoja na kubadilisha
biashara zao kutoka kuwa ndogo ndogo na kuwa za kati hadi za juu.
Vitambulisho
hivyo pia vitawafanya wajiamini zaidi ikiwa ni pamoja nakuongeza bidii katika shughuli zao kwani sasa wataweza kukopesheka kutokana na kuwa na vitambulisho
hivyo vilivyoboreshwa. Hivyo wafanya biashara hawana budi kuchangamkia fursa
hii kwa kuhakikisha kuwa wanavipata pale vitakapokuwa vimeanza kulipiwa.
Kufuatia
kauli ya Rais kuhusu kuboresha vitambulisho hivyo wajasiriamali wameonesha
kufurahishwa na hatua hiyo na kusema kuwa sasa ni wakati wa kukuza mitaji yao na kuinuka kiuchumi.
Mama Lishe, Mwajuma Salum wa soko la Mwananyamala amesema kuwa, “ Rais Magufuli
kweli ni mkombozi wa wanyonge, miaka yake mitano ya mwanzo alitupatia
vitambulisho na hivyo kutuwezesha kufanya biashara zetu kwa amani bila
kusumbuliwa na mtu yeyote, sasa amesema
ataboresha vitambulisho hivyo ili tuweze kukopesheka, Mungu amlinde”.
Naye
muuza matunda katika eneo la Afrika Sana Sinza, Mary Zephania amesema, “
Vitambulisho vikiboreshwa na nikapata cha kwangu hatua ya kwanza nitakwenda
kuomba mkopo ili nikuze mtaji wa biashara yangu ili ikiwezekana niweze
kusafirisha matunda hata nje ya nchi”.
Baadhi
ya wafanyabishara wadogo wadogo wa soko la Manzese wamesema kuwa wana imani na
Serikali ya Rais Magufuli ambayo wakati wote ina dhamira ya kuwaondoa katika
umaskini, maana tangu Rais aingie madarakani amekuwa akihimiza kuondolewa
changamoto mbalimbali zinazowakabili wajasiriamali.
Tangu
kuingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amechukua hatua mbalimbali za
kuimarisha uchumi na kuwakomboa wananchi kutoka katika umaskini na kuwawezesha
kufanya biashara bila kusumbuliwa ili kuwafanya wawe matajiri. Aidha katika
hotuba yake kwa Bunge la 12, ameendelea kusema kuwa Serikali atakayoiunda
itaendeleza jitihada za kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment