Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akimvisha kofia ya CCM Msanii, Baby Madaha katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale, Oktoba 25, 2020. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akizungumza na Bw. Jivunie Mponda baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale, Oktoba 25, 2020.
MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema uchaguzi mkuu umekaribia sana na amewaonya wana-Lindi na Watanzania wote wajihadhari na viongozi wanaohubiri udini.
Ametoa onyo hilo jana (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza kwa nayakati tofauti na wakazi wa kata tano za Kibutuka, Ngunichile, Lionja, Ruponda na Chiola alipokuwa njiani akirejea Ruangwa kutoka Liwale kupitia Nachingwea.
Alikuwa wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na mgombea ubunge wa jimbo la Nachingwea, Dkt. Amandus Chinguile na madiwani wa kata alizopitia.
“Uchaguzi mkuu umekaribia, tuwe makini na wanaohubiri udini. Kiongozi anayehubiri udini huyo hafai kuwa kiongozi wa Watanzania. Wako wengine wanaoanza kuigawa nchi kwa ukanda, ukianza kuigawa nchi kwa ukabila, unaua misingi ya Taifa hili.”
“Leo tuko wamoja kwa sababu ya amani iliyodumishwa na waasisi wa Taifa hili. Leo makabila tofauti wanaishi pamoja bila kubaguana. Ndiyo umekuwa utamaduni wetu. Hata hapa kuna Wamasai, Wangindo, Wachaga na kadhalika. Tunahitaji tumchague kiongozi atakayetunza amani ya nchi yetu,” alisisitiza.
Alisema: “Natambua, wananchi wenzangu mmekuwa na muda wa miezi karibu miwili wa kufanya tathmini na tafakari ya kina ili nani awe kiongozi wa nchi hii, nani awe mwakilishi wa jimbo hili na nani awe mwakilishi wa kata hii kwa maana ya diwani. Nataka niwahakikishieni kwamba kiongozi anayefaa anatoka Chama cha Mapinduzi,” alisema.
“Nimeangalia katika wote wanaotaka kupewa Urais, hakuna kiongozi mwenye hizo sifa zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli. Tulimpa miaka mitano ya kuongoza nchi, amefanya mambo makubwa na nyote mmeona ama kusikia yaliyofanyika kupitia vyombo vya habari.”
Akifafanua sifa za kiongozi anayetakiwa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Tunataka tupate kiongozi mahiri, mzalendo, mwadilifu na mwaminifu ambaye ni lazima tujiridhishe kuwa ataweza kuongoza nchi hii yenye watu zaidi ya milioni 60 na makabila tofauti.”
“Hatuhitaji kumchagua Rais ambaye sasa hivi anasema akiwa madarakani ataweka rehani madini yetu ili aweze kupata fedha za kuwawezesha wananchi. Sasa hivi nchi inapata mgao wa madini wa sh. bilioni 500 na ndiyo maana tunajenga hospitali, shule na barabara. Zamani tulikuwa tunapata shilingi bilioni 50 tu.”
Aliwataka wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli ili apambane na wala rushwa na akawaonya wasimchague kiongozi ambaye amezungukwa na mafisadi au wala rushwa. Aliwataka wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli kwa kura nyingi za ndiyo ili aweze kuleta maendeleo na kukamilisha yale mazuri aliyoyaanzisha.
“Tunataka kiongozi atakayelinda rasilmali za Taifa hili. Na huyo si mwingine bali ni Dkt. Magufuli. Ndugu zangu wa CHADEMA naomba kura zenu, wana ACT naomba kura zenu, CUF naomba kura zenu, na CHAUMA naomba kura zenu. Mchagueni Dkt. Magufuli awe Rais kwa sababu maendeleo hayana chama,” alisema.
Akielezea ni kwa nini anawaomba kura wananchi wa vyama vyote bila kujali itikadi zao za kisiasa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Ni kwa sababu tunatafuta kiongozi wa nchi. Uongozi wa nchi unataka mtu mchapakazi na mwenye nia ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, na huyu si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.”
No comments:
Post a Comment