Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Kusaya akiwa ameshika banio la kufungulia maji katika mtaro uliokamilika kwenye skimu ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa.Katibu Mkuu huyo alifanya ziara ya kushtukiza kwenye mradi huo leo Ijumaa kuona maendeleo ya maagizo aliyoyatoa Aprili 22,mwaka huu.
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akitoa maelekezo kuhusu ghala la kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo alipofanya ziara ya kushtukiza kwenye mradi huo.Katikati ni Eng.Amandus Urio msimamizi wa mradi .
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa barakoa ) akimsikiliza mwakilishi wa kampuni ya Gopa Construction LTD inayojenga skimu ya umwagiliaji kijiji cha Kigugu wilaya ya Mvomelo.Katibu Mkuu amekerwa na kampuni hiyo kufikia asilimia 48 ya kazi tangu ilipoanza kujenga Juni 2019.
Katibu Mkuu Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiongea na mafundi wanaojenga eneo la kuweka tenki la maji kwa ajili ya matumizi ya wakulima wa kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa kwenye skimu ya umwagiliaji zao la mpunga.
Katibu Mkuu
Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya amesema ameridhishwa na hatua ya ujenzi wa skimu
ya umwagiliaji kijiji cha Mvumi wilaya ya Kilosa ambayo imefikia asilimia 94 ya
ujenzi na tayari wakulima wameanza kunufaika .
Ametoa
kauli hiyo leo tarehe (15 .05.2020) alipofanya ziara ya kushtukiza kukagua
maendeleo ya mradi huo uliopo wilaya ya Kilosa Mkoa wa Morogoro chini ya mradi
wa Kuongeza Tija na uzalishaji wa zao la
Mpunga (ERPP)
“ Nimefurahi kuona skimu ya umwagiliaji kijiji
cha Mvumi imefikia asilimia 94 ya kazi zilizopangwa katika mkataba.Nimeridhika
na kazi ya mkandarasi huyu kwani tayari wakulima wanatumia maji toka kwenye
mifereji iliyokamilika kulima mpunga “ alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo alisema mradi wa umwagiliaji
kijiji cha Mvumi umegharimu shilingi Bilioni 1.97 na utanufaisha wakulima wengi
wa zao la mpunga katika wilaya ya Kilosa kuongeza uzalishaji na tija.
Akizungumzia
kazi zilizofanyika tayari Mhandisi Emanuel Nobert wa kampuni ya Whitecity
International Co.Ltd ya Dar es salaam amesema mradi ulihusisha ujenzi wa mitaro
ya umwagiliaji yenye urefu wa mita 1,374 na kukarabati mitaro mingine yenye
urefu wa mita 2,690.
Aidha
Mhandisi Norbert alisema wamejenga
barabara (access road) yenye urefu mita 6,876 ili kurahisisha usafiri wa mazao
na wakulima pamoja na ujenzi wa choo,bafu na kisima cha maji kwa ajili ya
wakulima shambani .
Katika
hatua nyingine Kusaya alikagua skimu ya umwagiliaji kijiji cha Kigugu wilaya ya
Mvomelo na kusema hajaridhishwa na kazi
ya mkandarasi Gopa Construction Ltd kwa gharama shilingi bilioni 1.93
aliyefikisha asilimia 48 tu tangu alipoanza kujenga tangu Juni mwaka jana 2019
.
“ Sijaridhishwa na mwenendo wa ujenzi wa skimu
hii ya Kigugu.Mkandarasi hujatimiza wajibu wako.Nataka kufikia tarehe 30
Mei mwaka huu kazi ikamilike”
alisisitiza Katibu Mkuu Kusaya
Katika ziara hiyo ya kushtukiza Kusaya pia alikagua ghala la kijiji cha Mbogo
Komtongo ambalo ujenzi wake umefikia asilimia 88 na kugharimu shilingi milioni
790.87 chini ya kampuni ya M/s Shekemu
na lile la kijiji cha Kigugu asilimia 92 kwa gharama ya shilingi milioni
816.37 chini ya Mkandarasi M/s Ami & Vai Investment.
Ziara hiyo
ya kushtukiza inafuatia ziara aliyofanya Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo
tarehe 22 Aprili mwaka huu alipoongoza ujumbe
wa Makatibu wakuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara,Ofisi ya Makamu wa
Rais- Mazingira na Ofisi ya Rais Tamisemi kutembelea miradi hiyo.
Miradi hiyo
yote inatekelezwa na Wizara ya Kilimo kupitia Mradi wa ERPP kwa lengo la
kusaidia wakulima wa zao la mpunga mkoa wa Morogoro kuongeza uwezo wa kuzalisha
na kuhifadhi mazao yao.
No comments:
Post a Comment