Friday, March 6, 2020

WAZIRI UMMY AWATAKA WANAWAKE KUCHANGAMIKIA FURSA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu akizungumza na wanawake wajasiriamali mkoani Simiyu wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Wanawake Wajasiriamali kuelekea Siku ya Wanawake Duniani.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amezindua maonesho ya wajasiriamali na huduma na kuwataka wakazi wa Simiyu kujitokeza kuchangamkia fursa hasa wanawake ili kujikwamua kiuchumi.

Ameyasema hayo leo wakati akifungua maonesho ya wanawake wajasiriamali na kuupokea msafara wa kijinsia ukizunguka katika katika mikoa tisa kutoa elimu ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Waziri Ummy amefungua maonyesho hayo ikiwa ni kuelekea kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani yatakayohitimishwa tarehe 8 Machi, 2020.

Aidha amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka na Katibu Mkuu, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia wazee na watoto anayeshughulikia Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, John Jingu kwa kufanikisha  maadhimisho  hayo zikiwemo
Taasisi mbalimbali.

Akizungumzia uboreshaji wa bidhaa lishe amesema Wizara ya Kilimo na Wizara ya  Afya, zinaweza kushirikiana kuboresha chakula lishe kwa watoto na kukabiliana na udumavu kwa watoto.

"Tukishirikiana kuwawezesha wanawake hawa kutumia teknolojia rahisi kukabiliana na udumavu kwa watoto" Alisema Waziri Ummy.

Amepongeza huduma na elimu kupitia misafara ya kupinga ukatili wa kijinsia iliyoratibiwa  na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali.

"Misafara hii imewafikia watu wengi na hivyo kupata elimu itakayowasaidia kuondokana na  vitendo vya ukatili" alisema.

Ameongeza kuwa anazo taarifa za wanaume wanaopata vipigo kutoka kwa wenza wao hivyo, wasione aibu kutoa taarifa kwenye madawati ya jinsia kwa ajili ya kupata msaada. 

"Ingawa unyanyasaji wa vipigo uko kwa wanawake lakini wanaume msiogope kuripoti pale mnaponyanyaswa ili mpate msaada" alisema

Kwa upande wake Katibu Mkuu- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt. John Jingu amesema Wizara kwa kushirikiana na wadau imejidhatiti katika kuhakikisha inatoa elimu kwa jamii ili kuweza kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia

Amesema kupitia makongamano na msafara wa kijinsia, Wizara imewafikia wadau wengi na lengo lilikuwa ni kuwafikia watanzania katika ngazi mbalimbali.


Akitoa salamu za Wizara ya ya kilimo, Naibu Waziri wa Wizara hiyo Hussein Bashe amesema wizara yake inatambua mchango wa wanawake katika sekta hiyo. 

"Kila penye wakulima wanne, watatu ni wanawake hivyo mchango wa wanawake katika kilimo ni mkubwa sana tunautambua sana mchango wenu wanawake" alisema

Maadhimisho ya  Siku ya Wanawake duniani 2020 yanaongozwa na Kaulimbiu ya isemayo Kizazi cha Usawa kwa Maendeleo ya Tanzania ya sasa na baadaye.

No comments:

Post a Comment