Monday, March 2, 2020

RC WANGABO AWAONYA WAKURUGENZI WANAOENDELEZA UDUMAVU KWA WATOTO RUKWA

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Lishe ya Mkoa pamoja na Halmashauri Kadi maalumu inyofafanua Tathmini ya utekelezaji wa Afua za lishe (score card) katika Mkoa wa Rukwa.

Mwenyekiti wa kamati ya lishe ya mkoa ambaye pia ni mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wajumbe wa kamati hiyo kuandaa zawadi kwaajili ya Mkurugenzi wa halmashauri anaefanya vizuri na anayefanya vibaya katika kutenga shilingi 1,000 kwaajili ya kila mtoto wa chini ya miaka mitano aliyepo katika halmashauri yake ili kutekeleza shughuli za lishe na kukabiliana na utapiamlo unaosababisha udumavu ndani mkoa.
Amesema kuwa wakurugenzi hao wanachangia kwa kiwango kikubwa kuupeleka mkoa mahala pabaya pamoja na taifa la Tanzania kwa ujumla kutokana na kuwa na lishe duni na hatimae kusababisha kukosekana kwa nguvu kazi jambao ambalo litarudisha nyuma juhudi za nchi katika kufikia uchumi wa kati wa viwanda kufikia mwaka 2025 na kusema kuwa hatuwezi kufikia uchumi huo kwa kuwa na Watoto waliodumaa.
“Hawa Wakurugenzi ndio ambao wanatupeleka huko, kwahiyo lazima tutafakari sana wakurugenzi kwahiyo yule ambaye atakuwa yuko nyuma sana yule tutamkabidhi kinyago kisichofaa lakini yule atakayefanya vizuri tutamkabidhi zawadi iliyo nzuri Zaidi, kwahiyo kamati na RAS kwa kuisimamia hiyo kamati ‘mta-design’ hiyo zawadi yenye “positive motivation” na “ very negative motivation” ili watu waone kwamba tunatoka hapo tulipo kuliko kila siku tunasema lakini habari ni ile ile,” Alisema
Aliongeza kuwa Mkoa wa Rukwa umebarikiwa tofauti na mikoa mingine ambayo inatekeleza mkataba wa usimamiaji wa shughuli za lishe kwasababu mkoa huo unasaidiwa na mradi wa Lishe Endelevu  ambao unafika katika vijiji vyote 339 ndani ya mkoa na hivyo kuwataka watendaji wote wa serikali kushirikiana na mradi huo kuhakikisha mkoa wa Rukwa unaondokana na udumavu kwa msaada wa mradi huo ili na hao watu wa mradi wajisikie fahari kufanikisha suala hilo ambalo ndio lengo kubwa la mradi lakini pia ndio lengo la taifa.
Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati wa mkutano wa tahmini ya utekelezaji wa mkataba wa utendaji kazi na usimamizi wa shughuli za lishe katika mkoa, ambapo wajumbe wa kamati za halmashauri nne za mkoa huo zilihudhuria, kamati zinazowajumuisha wataalamu kutoka katika kila idara za halmashauri pamoja na mkoa, viongozi wa dini, vyombo vya habari, vijana pamoja na wazee.
Wakati akitoa mchango wake katika mkutano huo Mkurugenzi wa mradi wa Lishe Endelevu Joyceline Kaganda alisema kuwa Mradi huo uliozinduliwa mwaka 2019 na kutegemewa kumalizika baada ya miaka minne ulilenga kutekeleza asilimia 25 ya mpango wake kwa mwaka wa Kwanza lakini kutokana na umuhimu wa kuharakisha kupambana na utapiamlo mradi umelenga kumalizia asilimia 75 zilizobaki kwa mwaka wake wa pili ambapo tayari wahudumu wa afya wa ngazi ya jamii 439 wameshapatiwa mafunzo.
“Wiki ijayo wengine 234 wataendelea kufundishwa, sasa kuwafundisha wale haitoshi, kwahiyo mradi jinsi ulivyokuwa umepangwa, ukishawafundisha wanapewa nyenzo na nyenzo katika jamii ni ule mkoba wa siku 1,000, mkoba wa njano wahudumu wanavaa mgongoni silaha ya kupambana na utapiamlo, sasa hiyo mikoba inaweza ikatuchelewesha kwasababu kuna wahudumu wamefundishwa lakini mikoba haijaja kwasababu anayetoa hiyo mikoba ni taasisi ya Lishe na Chakula tu,” Alisema 
Awali wakati akiwasilisha tathmini ya hali ya lishe katika mkoa wa Rukwa, Mganga mkuu wa Mkoa huo Dkt. Boniface Kasululu alisema kuwa kiwango cha udumavu kitaifa ni asilimia 31.8 wakati mkoa wa Rukwa una asilimia 47.9 hiyo ni kutokana na utafiti uliofanywa mwaka 2018 kuonyesha hali ya lishe kitaifa
“Mkoa wa Rukwa una Watoto waliodumaa 90,466 kati ya Watoto 188,864 ambao ni sawa na asilimia 47.9, lakini pia mkoa una Watoto 27,140 ambao ni sawa na asilimia 2.2 wana utapiamlo mkali na hali hii ni kutokana na Watoto hawa kuwa na upungufu wa virutubisho ambapo kwa Tanzania virutubisho vinavyotiliwa mkazo ni Vitamin A, Madini joto (Iodine), Asidi ya Foliki (Folic Acid),na Madini Chuma (Iron),” Alisisitiza.
Halikadhalika, Wakati akiwasilisha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa utendaji kazi na usimamizi wa shughuli za lishe katika mkoa, Afisa Lishe wa Mkoa Asha Izina alisema kuwa kutoka mwezi Juni hadi Disemba mwaka 2019 mkoa ulilenga kutoa elimu katika ngazi ya jamii kwa kuwatumia wahudumu wa afya ya jamii lakini pia katika ngazi ya vituo vya kutolea huduma ya afya pamoja na kufuatilia utolewaji wa matone ya Vitamin A.
“Katika utoaji wa Elimu Lishe ngazi ya Jamii walengwa ni watu 176,220 lakini waliopatiwa elimu ni 2,375 ambao ni sawa na asilimia 1.3, pia katika utoaji wa elimu ya lishe ngazi ya vituo vya kutolea huduma ya afya walengwa ni watu 176,220 lakini tuliwafikia watu 86,367 ambao ni sawa na asilimia 49 lakini katika kutoa matibabu kwa Watoto wenye utapiamlo mkali, mkoa ulilenga kuwafikia Watoto 27,140 lakini tuliowatambua ni Watoto 273 ambao ni swan a asilimia 1,” Alisema
Aidha aliongeza kuwa kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kulifanikisha suala hilo ikiwemo kuwepo kwa wato huduma wachache wenye uwezo wa kutoa elimu ya ulishaji wa Watoto wadogo ngazi ya jamii na vituo vya kutolea huduma za Afya, uelewa mdogo kwa watoa huduma za afya wa kutambua na kutibu utapiamlo mkali pamoja na halmashauri kushindwa kutoa fedha za utekelezaji wa afua za lishe.
Halmashauri za Mkoa wa Rukwa zilitegemewa kutenga kiasi cha Shilingi 356,234,595 kwaajili ya utekelezaji wa afua za lishe lakini hadi mwezi Disemba mwaka 2019 zilizotolewa na kutumika ni Shilingi 24,768,750 ambayo ni sawa na asilimia 7.

No comments:

Post a Comment