Mlezi wa umoja huo, Ahamed Asas aliwapongeza Umbi akisema unaundwa na vijana wenye hali ya kujiajiri, wanaoaminika na kutimiza ahadi zao pale wanaposaidiwa
KAMPUNI ya Asas Group ya
mjini Iringa imeudhamini Umoja wa Madereva Bajaj Iringa (UMBI) kupata mkopo wa
zaidi ya Sh Milioni 650 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita-uliowawezesha
kununua bajaj 97 zilizokopeshwa kwa mwanachama mmoja mmoja.
Kati ya bajaj hizo, bajaj
40 zenye thamani ya Sh 280 zilikabidhiwa juzi kwa wanufaika wa mkopo huo katika
hafla iliyoongozwa na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William
Lukuvi, mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela na mlezi wa umoja huo, Ahamed
Asas.
Mwenyekiti wa UMBI, Noberth Sumka alisema kwa
udhamini wa kampuni hiyo ya Asas umoja wao uliaminika na Finca Microfinance
Bank na kwa nyakati tofauti kupata mikopo iliyowawezesha kufikia mafanikio
hayo.
“Baada ya huko nyuma kutoa
mikopo ya bajaj 57 kwa wanachama wetu, leo tena wanachama 40 ambao awali
walikuwa madereva wa bajaj za watu wengine nao wananufaika na mkopo huu,”
alisema.
Kwa kupitia umoja huo
alisema, kila dereva aliyokopeshwa bajaj anatakiwa kufanya marejesho ya mkopo
ambao thamani yake pamoja na riba ni takribani Sh Milioni 9 katika kipindi cha
miezi 12 kuanzia sasa.
Kwa upande wake mlezi wa
umoja huo, Ahamed Asas aliwapongeza Umbi akisema unaundwa na vijana wenye hali
ya kujiajiri, wanaoaminika na kutimiza ahadi zao pale wanaposaidiwa.
“Bila uaminifu wao katika
urejeshaji wa mikopo wanayopewa, umoja huu usingefikia hatua waliyofikia
hivisasa. Ni vijana wenye dhamira ya dhati na wanapokusudia wanafanya,”
alisema.
Katika kuwaongezea hali ya
kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, mlezi huyo ameahidi kuchangia malipo ya
leseni kwa madereva 100 wa umoja huo na kuwakatia bima ya afya ili iwe rahisi
kwao kupata huduma za matibabu pale wanapohitaji.
“Gharama ya leseni ni Sh
70,000 kwahiyo mimi nitachangia Sh 50,000 kwa kila dereva na dereva atakayepata
ofa yangu atalazimika kuchangia 20,000 ili aweze kupata leseni hiyo,” alisema.
Na kwa kupitia umoja huo,
mlezi huyo ametoa Sh Milioni moja kukidhamini pia Chama cha Walemavu Iringa
hatua iliyokiwezesha kukopeshwa bajaj moja.
Akikabidhi bajaj hizo,
Waziri Lukuvi aliipongeza kampuni ya Asas kwa udhamini wake kwa madereva hao
akisema hatua hiyo itawawezesha kujitegemea lakini pia kuendana na falsafa ya
Rais Dk John Magufuli ya Hapa Kazi Tu.
“Yote haya yanafanyika na
kufanikiwa kwasababu Rais Dk Magufuli ametengeza mazingira mazuri ya watu wa
kipato cha chini kukopesheka na kufanya shughuli zao bila kubughuziwa,” Lukuvi
alisema.
Mkuu wa Wilaya ya Iringa
Richard Kasesela aliwapongeza madereva hao na akawataka wazingatie sheria zote
muhimu zikiwemo za barabarani wakati wakitumia vyombo hivyo.
“Msiwasilikilize wanasiasa,
zingatieni sheria kama mnataka fursa hii mliyoaipata iwapeleke hatua ya mbele
zaidi,” alisema.
Kasesela alisema mkoa wa
Iringa unazo fursa nyingi katika sekta mbalimbali na kama vijana watakuwa
tayari kuzitumia ipasavyo, zina uwezo mkubwa wa kubadilisha maisha yao.
No comments:
Post a Comment