Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akisalimiana na Mkuu wa Mkoa
wa Tanga Martine Shigela (kushoto) mara baada ya kuwasili mkoani humo kwa ziara
ya siku mbili (Januari 7-8, 2020) kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa
(TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Tanga
waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Anna
Mghwira akiongea na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison
Mwakyembe (hayupo pichani) alipowasili mkoani humo kwa ziara ya siku mbili
(Januari 9-10, 2020) kujionea namna Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC)
linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Kilimanjaro
waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata taarifa kupitia shirika hilo.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa tatu kulia) akiwa katika picha ya pamoja
na Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo (wa nne kushoto) alipowasili mkoani humo
kwa ziara ya siku mbili (Januari 11-12, 2020) kujionea namna Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili
wananachi wa mkoa wa Arusha waendelee wapate haki yao ya msingi ya kupata
taarifa kupitia shirika hilo.
Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kulia)
akiangalia mitambo ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ya kurushia
matangazo iliyopo eneo la Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga alipokuwa
ziara ya kikazi (Januari 8, 2020) kujionea namna shirika hilo linavyoboresha
usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Tanga waendelee kupata haki
yao ya Kikatiba ya kupata taarifa kupitia shirika hilo. Wa pili kulia ni Mkuu
wa wilaya ya Lushoto Januari Lugangika.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa
na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (wa kwanza kushoto waliotangulia) akielekea
eneo ilipo mitambo ya Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ya kurushia
matangazo iliyopo makao makuu ya wilaya ya Longido mkoani Arusha alipokuwa
ziara ya kikazi (Januari 12, 2020) kujionea namna shirika hilo linavyoboresha
usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Arusha waendelee kupata haki
yao ya Kikatiba ya kupata taarifa kupitia shirika hilo. Wa pili kulia waliotangulia
ni Mkuu wa wilaya ya Longido Frank Mwaisumbwe.
Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC) Mhandisi Upendo Mbelle (kulia) akitoa maelezo kwa
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe (katikati)
alipokuwa ziara ya kikazi (Januari 12, 2020) kujionea namna shirika hilo
linavyoboresha usikivu wa matangazo yake ili wananachi wa mkoa wa Kilimanjaro
ili waendelee kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata taarifa kupitia shirika
hilo. Wa pili kulia waliotangulia ni Mkuu wa wilaya ya Rombo Agnes Hokororo.
TBC ni shirika la utangazaji la umma lililoanzishwa
kwa mujibu wa Sharia ya Mashariki ya Umma ya mwaka 1992 kutoa huduma ya
utangazaji kwa umma kwa njia ya redio na televisheni na kupewa mamlaka ya kutangaza
vipindi mbalimbali vinavyoakisi misingi ya maadili ya Kitanzania kupitia vipindi
vya elimu na burudani; kutoa habari za aina mbalimbali, taarifa na uchambuzi
kwa mtazamo wa Kitanzania na kuendeleza maslahi ya taifa na ya umma.
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na
Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amesema Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) ni
chombo muhimu kwa wananchi kuweza kupopata taarifa na kujua matukio mbalimbali yanayotokea
nchini kwa mustakabali wa taifa ili wananchi waweze kujiletea maendeleo.
Waziri Dkt. Mwakyebe amesema hayo
alipokuwa akihitimisha ziara yake ya Kanda ya Kaskazini ambapo alitembelea mikoa
ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha kwa lengo la kuangalia hali ya usikivu wa Redio
ya Taifa TBC inayowarahisishia wananchi katika mikoa hiyo kupokea taarifa za
maendeleo ya nchi yao.
“Suala la wananchi kupata taarifa sahihi
na kwa wakati sio la hiyari, ni suala la Kikatiba, tunatekeleza hitaji la
Katiba Ibara ya 18 (d) ‘Kila mwananchi anahaki ya kupata taarifa ya masuala
mbalimbali yanayomhusu yanayohusu maendeleo ya taifa na ni wajibu wa Serikali
ya awamu ya tano kufanya hivyo’” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliendelea kusema “Namshukuru sana
Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwamba aliliona hili mapema ameingia tu
madarakani wakati usikivu wa TBC Taifa ambayo ni redio yetu ulikuwa ni 54 tu
nchi nzima, sasa hivi tunaongea ni asilimia 73 na tunatarajia ifikapo mwishoni
mwa mwaka 2020 usikivu utafikia zaidi ya asilimia 90 nchi nzima” Dkt.
Mwakyembe.
Akiwa mkoani Tanga alitembelea kituo
cha mitambo ya kurushia matangazo kiliyopo Mnyusi Hale wilayani Korogwe ambapo TBC
Taifa inarusha matangazo katika masafa
ya FM 87.7 Mhz na TBC FM inarusha matangazo
katika masafa ya FM 89.7 Mhz wakati wilayani Lushoto mitambo ya TBC Taifa ipo katika eneo la Kwemashai wilaya ya
Lushoto inarusha matangazo yake katika
masafa ya FM 87.9 Mhz na TBC FM inarusha matangazo katika masafa ya FM 89.9
Mhz.
Katika mkoa wa Kilimanjaro Waziri Dkt.
Mwakyembe alitembelea kituo cha TBC Taifa cha Mabungo kilichopo wilaya ya Moshi
kinarusha matangazo katika masafa ya FM
87.9 Mhz na TBC FM katika masafa
ya FM 90.0Mhz wakati Kituo cha Tarakea kilichopo wilayani Rombo, TBC Taifa
inarusha matangazo yake katika masafa ya 87.9 Mhz na TBC FM inarusha katika
90.0Mhz.
Aidha, Dkt. Mwakembe katika mkoa wa
Arusha alitembelea mitambo ya TBC Taifa iliyopo eneo la Themi katika Jiji la
Arusha ambapo matangazo yake yanapatikana katika masafa ya FM 87.7 Mhz na TBC
FM inayorusha matangazo katika masafa ya FM 89.9 Mhz na kuhitimisha ziara yake
kwa kutembelea kituo cha TBC cha Namanga kilichopo katika wilaya ya
Longido.
Katika ziara hiyo, Waziri Dkt.
Mwakyembe amepata taarifa katika mikoa hiyo ambapo zipo changamoto mbalimbali
ilipo mitambo ya TBC ikiwa ni pamoja na ubovu wa barabara ambao unapelekea
ugumu wa kufikika kwa urahisi maeneo hayo.
Maeneo ambayo barabara ni mbovu na
zinahitaji kujengwa kwa kiwango cha lami ama kujengwa kwa zege ni pamoja na Mnyusi
kilichopo Hale wilaya ya Korogwe na Kwemashai wilaya ya Lushoto mkoani Tanga;
Mabungo kilichopo wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro pamoja na kituo cha
Namanga kilichopo katika wilaya ya Longido mkoani Arusha.
Aidha, maeneo hayo pia yanahitaji kuwepo
kwa miundombinu ya umeme wa uhakika ili kuhakikisha radio inakuwa hewani wakati
wote na wananchi waendelee kupata haki yao ya Kikatiba ya kupata taarifa sahihi
na kwa wakati za shughuli mbalimbali za Serikali kwa manufaa yao na taifa kwa
ujumla.
Nao kwa upande wao Wakuu wa mikoa hiyo
Martine Shigela (Tanga), Anna Mghwira (Kilimanjaro) pamoja na Mrisho Gambo
(Arusha) wamemhakikishia Waziri Dkt. Mwakyembe suala la miundombinu ya barabara
pamoja na umeme katika maeneo ilipo mitambo ya TBC, kwao ni kipaumbele ili redio
ya Taifa iweze kusikika katika maeneo yao na wananchi wapate taarifa
zitakazowasaidia katika shughuli za kila siku ikiwemo kilimo, ufugaji, uvuvi
pamoja na taarifa za utalii ikizingatiwa Kanda ya Kaskazini uchumi wake unachangiwa
na sekta ya utalii .
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii
Dkt. Hamis Kigwangalla katika Hotuba yake ya Bajeti Wizara hiyo kwa Mwaka wa
Fedha 2019/2020 alisema kuwa idadi ya watalii walioingia nchini imeongezeka
kutoka 1,327,143 mwaka 2017 hadi kufikia watalii 1,505,702 mwaka 2018. Ongezeko
hilo limechangia kuongezeka kwa mapato yatokanayo na utalii kutoka Dola za
Marekani bilioni 2.2 mwaka 2017 hadi kufika Dola za Marekani bilioni 2.4 mwaka
2018.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Ufundi
wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) Mhandisi Upendo Mbelle aliyeambatana na
Waziri Dkt. Mwakyembe kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo Dkt. Ayub
Rioba amesema kuwa ziara hiyo imekuwa na mafanikio makubwa kwa shirika hilo na
kuahidi vitu vyote vilivyo ndani ya uwezo wa TBC wamevichukua na watavifanyia
kazi.
Mhandisi Upendo ameongeza kwa vitu ambavyo
vipo kisera amemuoba Waziri Serikali ivipatie ufumbuzi hatua itakayosaidia
shsirika kufikia malengo yake ikiwemo miundombinu ya umeme na barabara ili kuhakikisha
usambazaji wa matangazo ya Redio ya Taifa yanawafikia wananchi wote katika
maeneo yao ili kuwa na tija kwa shirika na taifa kwa ujumla wakiamini kwao
mradi namba moja ni usikivu wa redio hiyo kwa wananchi.
No comments:
Post a Comment