Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Sheria Ndogo William Ngereja akizungumza jambo katika Semina ya
Waheshimiwa Wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria
Ndogo).
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo (katikati)
akizungumza jambo kwenye Semina ya Wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge
(Nishati na Madini na Sheria Ndogo), Kulia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo William Ngeleja.
Baadhi ya Wabunge walioshiriki Semina ya
Wabunge wa Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo),
wakifuatilia semina hiyo.
Baadhi ya Wabunge walioshiriki Semina ya
Kamati za Kudumu za Bunge (Nishati na Madini na Sheria Ndogo) wakifutilia
semina hiyo.
Dodoma
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limesema litaharakisha Mchakato
wa Uanzishwaji Sheria ya Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini ikiwemo
kuishauri Serikali na kueleza kuwa, ni fursa nzuri ya kusimamia rasilimali
madini na itapunguza hasara kwa wadau.
Kauli hiyo iliyotolewa Januari 23, jijini Dodoma na Makamu Mwenyekiti wa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo, William Ngeleja kwa niaba ya
Mwenyekiti wa Kamati hiyo Andrew Chenge na kwa niaba ya Mwenyekiti wa Kamati ya
Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dustan Kitandula inafuatia maoni
yaliyotolewa na Wajumbe wa Kamati hizo ambapo wameeleza kuwa suala hilo
lilichelewa.
Wajumbe hao wamekutana katika Semina maalum iliyoandaliwa na Wizara ya
Madini kwa kamati hizo kwa lengo la kupitia na kutoa maoni katika Andiko la
Waraka wa Bodi ya Usajili wa Wanajiosayansi nchini.
Kufuatia hatua hiyo, Bunge limeipongeza Wizara ya Madini kwa kuanzisha
wazo hilo na kueleza kuwa, kutokuwepo kwa bodi hiyo kulipelekea
kufilisika na hasara kwa baadhi ya wadau wa madini ambao walipatiwa taarifa zisizo
sahihi za tafiti huku baadhi wajiolojia wasio waadilifu wakitoa taarifa
hizo wakijua siyo sahihi na kuwasababishia hasara wawekezaji hususan
wazawa.
Pia, Ngeleja ameitaka Wizara kuhakikisha inazingatia nafasi ya
wachimbaji wadogo wakati wa uanzishwaji wa sheria hiyo na kueleza kuwa
wanapaswa kupewa nafasi wakati Taratibu na Kanuni mbalimbali kuhusu Sheria hiyo
zinapoandaliwa.
Vilevile, amesisitiza kuhusu Wizara kutafakari kwa weledi suala la
vyanzo vya mapato kwa ajili ya kujiendesha baada ya kuanzishwa bodi hiyo
na kueleza kuwa, suala hilo linatakiwa kuangaliwa kwa umakini ili
kutoibebesha serikali mzigo wa kuwa chanzo pekee cha mapato.
Wakitoa maoni yao, Mbunge Catherine Ruge ametaka Bodi hiyo kutokuwa
chanzo cha mikwamo katika utekelezaji wa majukumu ya wanatasnia bali kuwa
chombo cha kuwawezesha kukua.
Naye, Mbunge wa Simanjiro, James Olle Millya amesema ‘’pamoja na
kuchelewa kuanzishwa bodi hii labda hatujatumia rasilimali zetu kama wengine,
naamini uwepo wa bodi hii utatuweka kwenye nafasi nzuri’’. Aidha, Millya
ameishauri serikali kuangalia namna itakavyosimamia kampuni za kigeni zitakazo
kuja kuwekeza nchini.
Akifungua Semina hiyo, Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema imelenga
kuweka uelewa wa pamoja ili kuwawezesha wajumbe wa kamati hizo kutoa maoni
kutokana na umuhimu wao katika uanzishwaji wa Sheria ya bodi hiyo.
Aidha, ameongeza kuwa, wataalam wa jilojia nchini wamekuwa hawana chombo
kinachowaongoza, taratibu wala sheria suala ambalo lilipeleka baadhi kutoa
taarifa za uongo kwa wadau, na hivyo kupelekea hasara kwa kutoa taarifa za
tafiti za madini zisizo sahihi.
‘’ Tumekuwa nyuma sana kuanzisha chombo hiki, wenzetu walianza zamani
mfano Sheria ya Local Content ipo kwa minajili ya kulinda nchi na wananchi na
bidhaa zao. Tumeona kuja na chombo hiki kutasaidia kulinda haki zao, fursa za
kulindwa na kutambuliwa kisheria,’’ amesisitiza Naibu Waziri Nyongo.
Ameongeza kuwa, Uwepo wa bodi hiyo utasaidia kudhibiti tabia hizo
ikiwemo kuweka taratibu, wataalam wataongeza tija katika rasilimali madini na
kutakuwa na chombo maalum cha kuwalinda.
Akiwasilisha andiko hilo, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Wizara ya
Madini, Edwin Igenge pamoja na mambo mengine ameeleza umuhimu wa kuanzishwa
bodi hiyo, majukumu na muundo wa bodi ya usajili ya Jiosayansi, uhusiano
wa bodi hiyo na vyombo vingine.
Ametoa uzoefu kwa nchi nyingine za Afrika na Ulaya ambazo tayari zina
bodi kama hizo tofauti na Tanzania na kuzitaja nchi za Kenya bodi yake ilundwa
miaka 27 iliyopita, Afrika Kusini miaka 17 na Kanada miaka 20 iliyopita.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Madini Dodoma (MRI), Prof. Hudson
Nkotagu amewaeleza wajumbe wa kamati hizo kuwa ni wataalam wenye sifa tu ndiyo
watakaofanya kazi hizo na kuongeza kuwa, wagunduzi watatambuliwa.
Akitoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja zilizoibuliwa, Katibu Mtendaji wa
Tume ya Madini Prof. Shukrani Manya amewaeleza wajumbe hao kuwa, bodi hiyo
inalenga kuwadhibiti wataalam wasio waaminifu wanaotafuta fedha kupitia taaluma
hiyo huku wakiacha hasara kwa wadau na kuongeza kuwa, itasaidia kuleta weledi
na kuwasaidia wadau kutokupoteza fedha zao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa
Madini Tanzania (GST), Prof. Justinian Ikingura akitoa ufafanuzi kuhusu suala
la sampuli hoja iliyoibuliwa na wajumbe wengi ameeleza kuwa, masuala ya maabara
na sampuli yana maadili , na taratibu zake, hivyo, bodi hiyo itaepusha madhara
mengi ambayo yamesababishwa na wataalam wasiokuwa waaminifu.
Chanzo: Wizara ya
Madini
No comments:
Post a Comment