Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb)
……………………………………………
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo – Sumbawanga
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) ameliagiza jeshi la Polisi nchini kumkamata na kumfungulia mashtaka ya uhujumu uchumi Kaimu Mrajis wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Rukwa Anosisye Mbetwa.
Waziri Hasunga ametoa agizo hilo jana tarehe 28 Disemba 2019 wakati akizungumza kwenye kikao cha kazi kilichowakutanisha viongozi na wanachama wa vyama vya ushirika (AMCOS) katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa.
Mrajis huyo ameweka kizuizini kwa kubainika kushiriki kuingia mkataba na Kampuni ya kusambaza mbolea ya ELI AGROVENT CO kinyume na taratibu za serikali hali iliyopelekea chama kikuu cha ushirika mkoani humo Ufipa Cooperative Union (UCU) kutapeliwa shilingi Milioni 277 huku wanachama wake wakiendelea kuhangaika juu ya upatikanaji wa mbolea.
Miongoni mwa vipengele vya Mkataba huo ulioingiwa tarehe 22.11.2019 vinasema kuwa Kampuni hiyo itamuuzia UCU mbolea ya Tani 1,901.05 yenye thamani ya shilingi Bilioni 2,384,266,812 ambapo bei ya mbolea hiyo iko juu ukilinganisha na maelekezo ya serikali juu ya bei elekezi za mbolea nchini.
Hadi kufikia tarehe 3.4.2020 chama hicho kinatakiwa kiwe kimekamilisha malipo hayo huku mkataba ukionesha kuwa malipo hayo yanasimamiwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa asilimia 100 jambo ambalo Ofisi ya Mkoa haifahamu.
Waziri Hasunga alisema kuwa lengo la kuanzishwa vyama vikuu vya ushirika katika mikoa ni kuweza kusaidia kuagiza pembejeo kwa niaba ya wanachama ili gharama za mbolea na hivyo kuushangaa mkoa wa Rukwa kwa kukubali kuingia mkataba wa kuuziwa mbolea ambayo bei yake ipo juu na kufafanua kuwa bei kubwa ya mbolea inatokana na gharama za usafirishaji gharama za faida kutoka bandarini kuja huku na kuongeza kuwa kuona manufaa ya ushirika bei ya ushirika inatakiwa iwe chini ya bei za soko ambazo wanauza wafanyabiashara kwenye masoko.
“Tulisema vyama vya ushirika visaidie kuagiza pembejeo kwa niaba ya wanachama ili gharama za mbolea zishuke hivi hapo kwenu huku rukwa ndio zimeshuka hapo yaani bei mnapeleka mbele ndio mnasema imeshuka halafu mnasema watu wawe na imani na hivyo vyama haiwezekani bei kubwa ya mbolea inatokana na gharama za usafirishaji gharama za faida kutoka bandarini kuja huku bei ya ushirika inatakiwa iwe chini ya bei za soko” Alikaririwa Mhe Hasunga na kuongeza kuwa
“Bei za soko ambazo wanauza wafanyabiashara kule kwenye masoko ziwe juu za kwenu ziwe chini ndio mtasema ushirika una manufaa ushirika gani unakwenda kuuza bei ya juu ambayo sio sawa na soko, utakuwa na akili timamu wewe utoe hela yako ukanunue bei ya juu wakati ungenunua kwa shilingi 54000 ungebaki na hela ya kwenda kumnunulia mtoto daftari”
Kadhalika, Mhe Hasunga ameagiza kukamatwa na kufunguliwa kesi ya uhujumu Uchumi Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kusambaza mbolea ya ELI AGROVENT CO Bw Elias Ndomba kutokana na kuwauzia wakulima mbolea kinyume na bei elekezi ya serikali iliyotangazwa hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment