Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza na Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu waliokutana kujadili namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dkt.Francis Michael akitoa mada kwa Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu kilichofanyika jijini Dodoma.
Mkuu wa Uelimishaji kutoka Taasisi ya Kupambana na Kutokomeza Rushwa TAKUKURU Bw. Asseri Mandari akitoa mada kuhusu jitihada za Taasisi hiyo katika kupambana na rushwa ya ngono katika sehemu za kazi na katika Sekta ya elimu hasa elimu ya juu katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika vyuo vya elimu ya juu.
Baadhi ya Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika kikao kilichofanyika jijini Dodoma kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vya elimu ya juu nchini.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano WAMJW
.................
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amekemea matukio ya vitendo vya ukatili wa kijinsia katika Vyuo vya elimu ya juu hasa vitendo vya rushwa ya ngono.
Dkt. Jingu ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kilichowakutanisha Wakuu wa vyuo vya elimu ya juu kilichohusu namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia katika maeneo ya Vyuo vya elimu ya juu.
Dkt. Jingu ameongeza kuwa tatizo la ukatili wa kijinsia limekuwa likishamiri katika Vyuo vya elimu ya juu kwani imeripotiwa kuwa wahadhiri wengi wamekuwa wakitumia madaraka yao kuwalazimisha wanafunzi kufanya nao ngono kwa lengo la kuwafaulisha mitihani.
Amesema kuwa sio wanafunzi pekee wanaokumbana na vitendo hivyo ila hata wafanyakazi wanaofanya kazi katika Vyuo vya elimu ya juu wanakubwa na vitendo vya ukatili wa kijinsia hivyo nguvu ya ziada inahitajika katika kupambana na vitendo hivyo vyuoni.
"Tumeshuhudia uwepo wa matukio ya ukatili wa kijinsia katika vyuo vyetu vya elimu ya juu hasa rushwa za ngono hili sio sawa tunatakiwa kulikemea kwa nguvu zote" alisema Dkt Jingu.
Dkt. Jingu amesema kuwa katika kuhakikisha tunapambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia Serikali na Wadau wanatekeleza Mpango Mkakati wa Kitaifa wa Kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na Watoto ili kuhakikisha kuwa vitendo hivyo vya ukatili wa kijinsia nchini vinatokomezwa kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2030.
Aidha Dkt. Jingu amewataka wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatoa elimu na maelekezo ili kujenga uelewa wa kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hasa kwa wanafunzi wa kike kwa kwa ajili ya kuepuka matakwa ya wahadhiri wanaotumia hila kuendekeza ukatili wa kingono vyuoni.
Pia Dkt. Jingu amewataka Wakuu wa vyuo hao kuhakikisha wanatekeleza Agizo la Waziri Ummy Mwalimu la kuanzisha madawati ya jinsia katika vyuo vyao ili kuwezesha kuondokana na vitendo vya kikatili na kujenga mazingira yaliyosalama katika vyuo vyetu.
Naye Mkurugenzi wa Taasisi ya Taaluma za Jinsia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dkt. Lulu Mahai amesema kuwa Vyuo vya elimu ya juu vinawajibu mkubwa wa kuhakikisha wanatoa elimu kuhsu kupambana na vitendo vya kikatili kwa wanafunzi wa wafanyakazi na wanaamini baada ya kikao hiki watarudi na kuanzisha madawati ya jinsia na kamati mbalimbali zitakazosaidia kupambana na matukio ya ukatili wa kijinsia katika Taasisi na Vyuo vyote nchini.
No comments:
Post a Comment