Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilosa Asajile Mwambambale wakati akitoka
eneo la Kiwanda cha Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd Kilosa Morogoro
jana. Kulia kwa Lukuvi ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akizungumza na wananchi wa kijiji cha
Magomeni wilaya ya Kilosa mkoa wa Morogoro (hawapo pichani) jana
alipokwenda kusikiliza malalamiko ya wakazi wa kijiji hicho kuhusiana na
shamba la Mwekezaji Farm Africa Agro Focus Ltd. Kushoto ni ya Wilaya ya
Kilosa Adam Mgoyi.
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
**********************************
Na Munir Shemweta, WANMM KILOSA
Wananchi wa
kijiji cha Magomeni kilichopo tarafa ya Kilosa Mjini wilayani Kilosa
mkoa wa Morogoro wametoa kilio chao kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi William Lukuvi wakitaka kupatiwa shamba la Mwekezaji
Farm Africa Agro Focus Ltd marufu kama kwa Karamagi kwa madai kuwa
mwekezaji wa shamba hilo ameshindwa kuliendeleza.
Wananchi hao
wamemueleza Lukuvi kuwa kijiji hicho hakina ardhi ya kutosha kuwawezesha
wananch hao kujishughulisha na kilimo na eneo kubwa katika kijiji hicho
ni eneo la shamba la Farm lenye ukubwa wa ekari 13,000.
Wananchi hao
wa kijiji cha Magomeni walitoa kilio chao kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi jana tarehe 08 Novemba 2019 wakati Lukuvi akiwa
katika ziara yake wilayani Kilosa kuendelea na jitihada za kutatua
migogoro ya ardhi katika mkoa wa Morogoro.
Wamedai kuwa
pamoja na Muwekezaji kuwa na eneo kubwa lakini ameshindwa kuliendeleza
kama taratibu zinavyotakiwa na badala yake sehemu kubwa ya shamba hilo
imebakia kuwa pori ingawa limeendelezwa katika eneo la usoni.
Mmoja wa
wananchi hao Ismail Masudi alimueleza Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi kuwa kwa muda mrefu wananchi wa kijiji cha magomeni
wamekuwa wakiishi kwa hofu kubwa kutokana na mgogoro wa muda mrefu kati
ya muwekezaji na wananchi wa kijiji hicho.
‘’Wananchi
tumepiga kelele sana ya kusaidiwa, Mwekezaji ana eneo kubwa lakini
wananchi wanakosa maeneo ya makazi na ya kufanyia shughuli za kilimo
huku sehemu kubwa ya shamba ka mwekezaji ikiwa ni pori’’ alisema Masudi
Mwananchi
mwingine Hatibu Musa alisema kilio kikubwa cha wakazi wa kijiji cha
Magomeni ni eneo la kulimia wakati idadi ya wakazi inaongezeka na
wananchi wamehangaika kwa takriban miaka 5 na mgogoro huku wakidai
mwekezaji hana tija.
Kwa upande
wake Wzairi wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi
alimtaka Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Adam Mgoyi kumuomba mwekezaji wa
shamba hilo kupunguza ekari 3000 kati ya 10,000 alizokuwa nazo kwa ajili
ya kuwapatia wananchi wa kijiji cha Magomeni.
‘’ Badala ya
kuanza kufuta shamba, Mwekezaji arudishe ekari 3000 kati ya 13,000
alizokuwa nazo tunataka kasi ya uendelezaji uendelee maana haiwezekani
miaka nanne ni ekari 2000 tu zilizoendelezwa’’ alisema Lukuvi
Alisema,
haingilii maamuzi ya mahakama yaliyompa ushindi Mwekezaji na wala hataki
wananchi kupingana na maamuzi ya mahakama bali hali hiyo inafuatia
mwekezaji kushndwa kuliendeleza shamba kama taratibu zinavyotakiwa
ambapo uendelezwaji unatakiwa kufanyika moja ya nane kila mwaka jambo
alilolieleza muwekezaji huyo alishindwa kutekeleza.
Taarifa
kuhusiana na shamba hilo zinaeleza kuwa Mwekezaji wa sasa Farm Africa
Agro Focus alikabidhiwa shamba mwaka 2013 na hadi kufikia sasa ni ekari
2000 pekee kati ya 13,000 ndizo zilizoendelezwa kwa kulima zao la
Korosho.
No comments:
Post a Comment