Na Mwandishi Wetu, Lindi
Mkoa wa Lindi umetumia zaidi ya
bilioni 10.4 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Tano katika kipindi
cha miaka minne kuboresha sekta ya afya.
Akizungumza katika kipindi cha
‘TUNATEKELEZA’ Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Mhe. Godfrey Zambi amesema kuwa
baadhi ya miradi iliyonufaika na fedha hizo ni pamoja na ujenzi wa
Hosptali za Wilaya, Vituo vya Afya, na Zahanati ili kuwawezesha wananchi
kupata huduma bora za afya.
“Ujenzi wa miundombinu katika
sekta hii umeenda sambamba na upatikanaji wa dawa ambao umefikia zaidi
ya asilimia 95 katika maeneo yote ya kutolea huduma katika mkoa wetu,”
alisisitiza Zambi.
Akifafanua,amesema kuwa
kuimarishwa kwa huduma za afya katika mkoa huo kumesaidia kuwawezesha
wananchi kushiriki katika kukuza uzalishaji wa mazao ya biashara na
chakula, hivyo kukuza uchumi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.
Akizungumzia elimu bure Mhe. Zambi
amesema kuwa zaidi ya shilingi bilioni 4 zimetolewa kugharamia elimu
bure katika mkoa huo hali iliyowezesha kuongeza maradufu kiwango cha
wanafunzi wanaosajiliwa kujiunga na shule za msingi.
Kwa upande wa chuo cha ualimu
Nachinge, Mhe. Zambi amesema kuwa zimetumika kukarabati chuo hicho kwa
kuboresha miundombinu yake ikiwemo mabweni, maktaba na madarasa.
Katika sekta ya maji, Mradi wa
Ngapa umewezesha uzalishaji wa maji kufikia lita milioni 7.5
ikilinganishwa na lita milioni 2 zilizokuwa zikizalishwa awali kabla ya
kutekelezwa kwa mradi huo.
Mhe. Zambi amebainisha kuwa mkoa
huo umepiga hatua katika sekta ya uwekezaji kutokana na kuwepo kwa
nishati ya uhakika baada ya mkoa huo kuunganishwa na gridi ya Taifa hali
inayowezesha wawekezaji kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo
kilimo, gesi na uchimbaji wa madini.
“Mkoa wa Lindi umepata wawekezaji katika sekta ya uchimbaji wa madini ya graphite
na bado tunaendelea kuwakaribisha wawekezaji wengine kuja kuwekeza
katika mkoa wetu kutokana na kuimarishwa kwa miundombinu na upatikanaji
wa umeme wa uhakika,” alisisitiza Zambi.
Mkoa wa Lindi ni moja ya mikoa
iliyofanikiwa katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayolenga
kuleta mageuzi na ustawi wa wananchi katika sekta za afya, elimu, maji,
barabara na nyingine zinazolenga kukuza uchumi.
No comments:
Post a Comment