*Ni kwa wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka 2019/2020
WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amesema hadi kufikia Novemba 3, mwaka huu, Serikali
imekwishatoa mikopo ya sh. bilioni 162.8 kwa wanafunzi 46,838 wa mwaka
wa kwanza nchini kote.
“Kwa mwaka
2019/2020, Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 450 kwa ajili ya
mikopo kwa wanafunzi walengwa 128,285. Na hadi tarehe 3 Novemba, 2019
wanafunzi 46,838 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka 2019/2020, walikuwa
wamepewa mikopo inayofikia shilingi bilioni 162.8,” amesema.
Ametoa kauli hiyo
leo jioni (Jumapili, Novemba 10, 2019) wakati akizungumza na maelfu ya
waumini waliohudhuria Baraza la Maulid kitaifa katika viwanja vya Benki
Kuu (BoT) Capripoint, jijini Mwanza.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli, amesema Serikali
inatambua kuwa utoaji wa huduma ya elimu ni gharama na kuwa baadhi ya
wananchi hawawezi kumudu gharama hizo, hivyo ikaamua kuanzisha utaratibu
wa kutoa mikopo ya elimu ya juu kupitia Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.
“Mikopo
inayotolewa na Serikali, huongozwa na Sheria ya Bodi ya Mikopo (Sura
178) inayotaja vigezo vya wahitaji na wenye udahili lakini wasio na
uwezo wa kumudu gharama zote au sehemu ya gharama za mafunzo au kwenye
maeneo ya kipaumbele ikiwemo yatima na wanaotoka familia zenye kipato
duni.”
“Hata, hivyo
Serikali inaendelea kufanyia kazi maoni na mapendekezo ya wadau
mbalimbali ili kuboresha mfumo wa utoaji mikopo ya elimu ya juu. Nitumie
nafasi hii kuwapongeza sana BAKWATA kwa kuweka mkakati wa kuunga mkono
jitihada za Serikali katika eneo hili.”
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu amewataka viongozi mbalimbali watumie maadhimisho ya mazazi
ya Mtume Muhammad (S.A.W) kama chachu ya kujiuliza juu ya uongozi wao,
na kwa kiasi gani uongozi wao unaacha alama kwa wale wanaowaongoza.
“Kipindi hiki
tunachoadhimisha mazazi ya Mtume huyu mbora wa darja, hebu nasi kama
viongozi wa waumini tujiulize na tujitathmini, je, ni kwa kiasi gani
tunamuenzi kwa kufuata mwenendo mzima wa Mtume Muhammad Swalla Allahu
Alayh Wasallam. Je, ni kwa kiasi gani uongozi wetu umekuwa ni wenye
kuacha athari njema kwenye nyoyo na fikra za waumini?”
Amesema wataalamu,
waandishi na watafiti wa masuala ya uongozi walitumia muda mwingi
kumsoma Mtume Muhammad (S.A.W). “Sababu kubwa iliyowavutia kumtafiti,
kumsoma na hata kumuandikia makala na vitabu mbalimbali ni mafanikio
makubwa aliyoyapata katika uongozi wake. Itoshe tu kusema kwamba Mtume
Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam alikuwa ni mtu wa familia na
kiongozi makini kabisa.”
Aliwataka watambue
kwamba mtu anaweza kuteuliwa kuwa sheikh au imamu lakini hawezi kuwa
kiongozi bora mpaka pale uteuzi au kuchaguliwa kwake utakapothibiti
katika nyoyo na fikra za wale anaowaongoza.
“Nitoe rai kwamba
wakati tunapoelekea kwenye uchaguzi wa viongozi wa BAKWATA kwa ngazi
mbalimbali baadaye mwaka huu, suala la kumuogopa Allah mtukufu na
kufuata mwenendo wa bwana Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam
uwe ndiyo mwongozo wetu wa kuwapata viongozi,” alisisitiza.
Mapema,
akitoa salamu za BAKWATA Taifa, Katibu Mkuu wa BAKWATA, Ustaadh Nuhu
Jabir Mruma alisema Baraza hilo limeanzisha vikundi 82 vya uzalishaji
vinavyojishughulisha na kazi za bustani na shamba darasa.
Kuhusu masuala ya
utoaji wa haki na sheria, Katibu Mkuu huyo alisema watu 59,824
walipatiwa msaada wa kisheria na wataalamu wasaidizi wa sheria
(paralegals) 79 katika maeneo mbalimbali nchini.
Alisema Desemba
mwaka huu, BAKWATA itafanya uchaguzi katika ngazi mbalimbali. “Kupitia
chaguzi hizo, tunatarajia kupata viongozi wabunifu, waadilifu na
wachapakazi. Ninawasihi Waislamu wenye sifa wajitokeze kugombea nafasi
husika.”
Pia alitumia fursa
hiyo kuwaomba Waislamu wote wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi wa
viongozi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, mwaka huu ili
watumie haki yao ya kuchagua viongozi wanaofaa. “Kuacha kupiga kura ni
kuwapa wengine fursa wakuchagulie viongozi wanaowataka. Tuepuke
kuchaguliwa viongozi tusiowataka,” alisema.
No comments:
Post a Comment