Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,
Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani
Jafo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo ofisini
kwake jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusiana na vyama vyote vya
siasa vinavyoshiriki kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa zilipelekwa
rufaa kwenye kamati za maeneo yao.
Sehemu ya waandishi wa habari
wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo alipokuwa akizungumza na waandishi wa
habari leo jijini Dodoma.
……………..
Na Alex Mathias
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amesema zaidi ya rufaa 13,500
zimewasilishwa na vyama vya siasa kwenye kamati za rufaa za uchaguzi wa
serikali za mitaa.
Aidha, amesema kwa mujibu wa
kanuni za uchaguzi huo jina la mgombea likiteuliwa linabaki kwenye
katarasi za kupigia kura hata kama amejiengua kushiriki.
Akizungumza leo na waandishi wa
habari jijini Dodoma, Jafo amesema vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki
kwenye uchaguzi huo zilipelekwa rufaa kwenye kamati za maeneo yao.
“Vyama vyote vimewasilisha rufaa
ikiwemo CCM,CUF, NCCR, ACT na rufaa zilizowasilishwa si chini ya 13,500
kamati zinaendelea kufanya maamuzi na tayari zikingine zimeshatoa majibu
ya rufaa, kesho tutapata sura halisi ya mchakato mzima wa
uchaguzi,”amesema.
Amefafanua kuwa baada ya mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu
kukamilika, kulikuwa na nafasi ya kushughulikia mapingamizi mbalimbali
ambayo yamewasilishwa kwenye kamati za rufaa za maeneo husika ambapo
mwisho wa kupitia rufaa hizo ni leo.
“Kuna ngazi za mapingamizi na jambo hili ni la kidemokrasia huwa
linafanyika, ibara ya 23 ya kanuni zetu inasema kamati za rufaa
zinamajukumu ya kupitia rufaa zote zinazojitokeza,”amesema.
Aidha amesema katika ziara yake aliyoifanya mikoa mbalimbali
kukagua shughuli zinazofanywa na kamati za rufaa kwenye mikoa mbalimbali
Singida, Dodoma, Manyara, Iringa na Njombe alipitia baadhi ya fomu
zilizokuwa zimepitiwa na kamati hizo na kubaini kuna makosa kwenye
ujazaji fomu.
“Kama vile mtu ameandika umri amezaliwa mwaka 2019, sehemu
zingine mtu ameandika hata halmashauri yenyewe haiitwi hiyo msaidizi wa
uchaguzi afanye nini?, mwingine sehemu ya saini ameweka tarehe halafu
sehemu ya tarehe ameweka saini, fomu zingine mtu amejidhamini mwenyewe,
wasimamizi walifanya kazi yao kwa mujibu wa kanuni,”amesema.
Ametaja mapungufu mengine ni kutofautiana majina kwenye fomu na daftari la wapiga kura wa uchaguzi.
“Hivi vyote ni vigezo sehemu zingine ni kama mtu mmoja alichukua
fomu akawapa watu wengine ‘wadese’ yaani fomu moja iliyokosewa kundi
lote limekosea, hii ni kutokana na viongozi hawakufanya kazi yao vizuri
ili fomu zijazwe vizuri,”amesema.
Ameongeza kuwa “Nilishasema malalamiko yote yapelekwe kamati za
rufaa kwa kuwa zinafanya kazi kwa mujibu wa kanuni na hizi kamati
hazifungwi na mtu, nashukuru baadhi ya vyama vimewasilisha na kazi
inaendelea ya kupitia rufaa hizo ikiwa leo ni mwisho.”
Jafo amesisitiza uchaguzi wa mwaka huu hauna ujazaji holela wa
fomu, na kamati za rufaa zitaendelea kupitia na kutoa maamuzi sahihi.
“Kesho tutatoa taarifa ya rufaa zilizopita na watu walioteuliwa
kushiriki uchaguzi huo, tunaendelea vizuri tunatarajia leo jioni
zitakamilisha kazi kamati za rufaa na zinafanyia kazi rufaa zote kwa
kuwa ziliwasilishwa na wagombea, na watatoa matokeo kwa vyama vyote
lakini kamati ya rufaa itakuwa imetimiza wajibu wake,”amesema.
Kuhusu mchakato wa uchukuaji na urejeshaji fomu, Jafo amesema
uchaguzi wa mwaka huu kwa mara ya kwanza ukiwa na kanuni bora zaidi ili
kila jambo lifanyike kwa utaratibu.
“Wananchi waliochukua walikuwa 555,036 na waliorejesha 539,993
sawa na asilimia 97.29 na asilimia 2.7 hawakurejesha kwasababu
mbalimbali,”amesema.
No comments:
Post a Comment