**************************************
MWENGE wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa wilayani Nachingwea.
Kiongozi wa mbio za mwenge
kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo
iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.
Miradi hiyo ni mabweni mawili
kwenye shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi wa maji wa
Kitandi katika kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye kata
ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.
Akizungumza na wananchi
waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10, 2019)
kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw.
Mkongea amewataka wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi
kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia wajitokeze
kupiga kura siku ya uchaguzi huo, Novemba 24, mwaka huu.
Mapema, akizungumza na wakazi
waliojitokeza kuupokea mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema
mwenge wa uhuru unakimbizwa maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha
wananchi washiriki kwenye shughuli za maendeleo.
“Mwenge wa Uhuru unakimbizwa
kwenye maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze
kushiriki kwenye miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na
kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere na hivyo, tunakumbushwa kuyaenzi mawazo yake,” alisema.
Mbali ya kuwahimiza washiriki
kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema
kuna makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa taarifa zao
kwenye Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.
“Wanaotakiwa kushiriki zoezi
hili, ni wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini
vimefutika; waliohama maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako
watapigia kura mwakani; waliokuwa na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015
na sasa wamezidi umri huo; na wale ambao mwakani wanatarajia kufikisha
umri wa miaka 18,” alisema.
Mapema, akizungumza baada ya
kupokea mwenge huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi.
Rukia Muwango alisema leo utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi
yenye thamani ya sh. milioni 781.5 itazinduliwa.
Kesho (Ijumaa, Oktoba 11)
mwenge huo utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na
Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio
hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment