Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) akiwa na Mbunge wa Mbulu vijijini Mhe. Flatei Gregory
Massay na Mkuu wa Wilaya ya Mbulu Bw. Chelestino Mofuga pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Babati
Mhandisi Iddy Msuya wakielekea kukagua mradi wa Tumati uliopo Mbulu
vijijini.
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) akipata maelezo ya mradi wa Arri Harsha kutoka kwa Mhandisi
Maji wa Halmashauri ya Mbulu Philemon Kamar.
Wananchi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Mbulu wakimsikiliza kwa makini Waziri wa Maji, Mhe. Prof.
Makame Mbarawa (Mb) hayupo pichani.
……………….
Waziri wa Maji, Mhe. Prof. Makame
Mbarawa (Mb) amefanya ziara ya kukagua miradi ya maji yenye changamoto
katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mkoani Manyara.
Waziri Mbarawa amefanya ziara hiyo
ili kubaini changamoto zilizopo katika miradi ya maji ili serikali
iweze kutafuta ufumbuzi wa haraka na wananchi wa Mbulu waweze kupata
majisafi na salama na kutekeleza azma ya kumtua mama ndoo kichwani.
Waziri Mbarawa amesema changamoto
kubwa iliyokuwepo ni kuwa wakandarasi wanaopewa kazi hizo za kutekeleza
miradi, wanaweka gharama kubwa za ujenzi na kujenga miradi chini ya
viwango.
Mhe. Mbarawa amesema kwa muda
mrefu Serikali imekuwa inalipa gharama kubwa za kujenga miradi ya maji
nchini kutokana na ubabaishaji wa wakandarasi wa kuweka gharama kubwa,
kujenga miradi isiyokuwa na ubora na miradi kutokamilika kwa wakati
hivyo kuwafanya wananchi wakose majisafi na salama.
“Kuanzia sasa Serikali imekuja na
utaratibu mwingine wa kuwatumia wataalam wake wa ndani na Mamlaka za
Maji za eneo husika katika utekelezaji wa miradi ya maji ili kupunguza
gharama kubwa zilizokuwa zinawekwa na wakandarasi”, Prof. Mbarawa
amesema
Miradi iliyokaguliwa ni mradi wa
maji wa vijiji vya Mongahay, Tumati, mradi wa maji wa vijiji vya Arri,
Yaeda Ampa, Haseng, Harsha Bashay na Yaeda. Mhe. Mbarawa ameahidi
kupeleka kiasi cha fedha Tsh. 150 milioni kwa mradi wa Tumati na Tsh.
300 milioni kwa mradi wa Arri Harsha ambazo zimeshafika katika Mamlaka
ya Maji Babati kwa ajili ya kuanza kazi za kukamilisha kazi zilizobaki.
Mhe. Waziri Mbarawa akizungumza
na wananchi wa Halmashauri ya Mbulu na kusikiliza kero zao amewaahidi
kwamba kero zao zitafanyiwa kazi ili kuhakikisha wanapata majisafi na
salama.
Waziri Mbarawa amewataka wananchi
wa Mbulu kutunza miundombinu ya miradi ya maji na kutunza vyanzo vya
maji ili viwe endelevu kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kizazi
kijacho.
No comments:
Post a Comment