Mbunge mpya wa jimbo la Singida Mashariki Mhe Miraji Jumanne Mtaturu akiwa na mwandishi Mwandamizi na mchambuzi wa habari nchini Ndg Mathias Canal leo tarehe 10 Septemba 2019 mara baada ya mahojiano kuhusu nafasi ya Ubunge aliyoipata Mhe Mtaturu.
Na
Innocent Natai, WazoHuru Blog-Dodoma
Mbunge mpya wa jimbo la Singida Mashariki Mhe
Miraji Jumanne Mtaturu amesema kuwa mafanikio ya kiuongozi aliyoyapata
yametokana na kuwaunganisha wanachama na wananchi, jambo ambalo limefanikisha
wananchi kuzidi kukiamini Chama Cha Mapinduzi na kushiriki shughuli za
maendeleo.
Mhe Hasunga ameyasema hayo leo tarehe 10 Septemba
2019 nje ya ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma wakati akifanya mahojiano maalumu na
WazoHuru Online Tv.
Mtaturu amesema kuwa kitendo cha kuwaunganisha
wananchi na wanachama wakati akiwa kama katibu wa Chama cha Mapinduzi wilaya ya
Mufindi mkoani Iringa vilevile Katibu wa CCM mkoa wa Mwanza amefanikisha
kurejesha majimbo mawili yaliyokuwa upinzani ikiwemo jimbo la Nyamagana na
Ilemela.
Akizungumzia nafasi aliyopewa ya kuongoza wilaya ya
Ikungi ambayo ina majimbo mawili ya Singida Magharibi na Singida Mashariki
ambapo mojawapo ya jimbo ambalo amegombea na hatimaye kuwa mbunge, amesema kuwa
akiwa katika nafasi hiyo alifanikiwa kutatua kero za wananchi na kujua mahitaji
halisi ya wananchi wa wilaya hiyo na kitendo kilichompa umaarufu na kuzidi kuaminika.
Ameongeza kuwa wakati alipofika katika wilaya hiyo
pia alihakikisha ulinzi na amani vinakuwepo kwa wananchi wote, ukilinganisha na
kwamba wakati akianza uongozi wake
katika wilaya hiyo palikuwepo na mauwaji yaliyokuwa yanatokea maeneo ya
wafugaji.
Aidha, akizungumzia changamoto za utekelezaji na ucheleweshwaji
wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa wananchi kujitolea kwenye maendeleo
ya elimu katika wilaya ya Ikungi, amesema kuwa anaipongeza sana serikali
kutokana na mfumo wa elimu bure kwani umesaidia sana kuboresha na kuongeza
kiwango cha elimu nchini.
Akishirikiana na wananchi alifanikiwa kuboresha
mazingira ya elimu (Maabara ya Ikungi) kwa kushirikishana pia katika shughuli
za maendeleo jambo lililopelekea kuondoa ile dhana waliyokuwa wamejengewa ya
kwamba serikali ina fedha nyingi kwahiyo wasichangie shughuli za maendeleo.
Pia amewataka wananchi na wanachama wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) kuzidi kushirikiana na serikali katika kuchangia maendeleo ili kusaidia
miradi mbalimbali kumalizia
Mtaturu aliapishwa rasmi kuwa mbunge wa Jimbo la Singida
Mashariki September 3 mwaka huu ambapo alichukuwa kiti hicho kilichokuwa
kinashikiliwa na Tundu Lisu aliyevuliwa ubunge na Spika Job Ndugai mnamo Juni
28 mwaka huu kwa makossa ya kukiuka sheria na taratibu za Bunge.
Akizungumzia kuhusu kupingwa ubunge wake amesema kuwa
alichokifanya Tundu Lisu kilikuwa ni sahihi kwa upande wake kwa sababu alikuwa
akitafuta haki yake.
“Ni jambo la kawaida la kimtazamo na kwa sababu mtu
anatafuta haki alipaswa afanye vile na mimi kwa sababu sikuwa mshtakiwa sikuwa
na tatizo, kwa hiyo kimsingi nilikuwa nasubiri maamuzi ya Jaji ili mimi
niendelee na taratibu zingine’’alisema Mtaturu
Aliongeza kuwa hakuwa na tatizo lolote kimsingi
katika zoezi zima la uchaguzi alifuata utaratibu wote katika kupata nafasi
hiyo, hivyo pingamizi lililowekwa lilikuwa halimuhusu yeye lilikuwa baina ya
mlalamikaji na Spika wa Bunge Mhe Job Ndugai ndio maana mahakama ikalitupilia
mbali pingamizi hilo.
Akitoa mapendekezo yake ya mambo atakayofanya baada
ya kuanza kazi zake akiwa mbunge wa jimbo hilo amesema kuwa atapambana
kuhakikisha Hosipitali ya wilaya inakamilika haraka iwezekanavyo, kuendelea
kuchimba visima vya maji maeneo mbalimbali, Ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA)
ambacho kitawasaidia vijana wa Singida na nchi nzima ili kuweza kupata ajira na
ujuzi wa kuweza kufanya shughuli mbalimbali.
Aidha, ameahidi kuendelea kupambana na changamoto
ya umeme, kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora, afya na kuhakikisha
anaboresha uchumi wa kaya kwa kuanzisha mradi ujulikanao kama “Kopa ng’ombe
lipa ng’ombe’” ambao utawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi.
MWISHO
No comments:
Post a Comment