Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo
kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Tanga Martine Shighela (Kushoto) wakati
akikagua moja ya itakayokuwa ofisi ya Ardhi mkoa wa Tanga wakati ziara
yake katika mkoa huo mwishoni mwa wiki. Kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la
Tanga Daud Mayeji.
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akipata maelezo
kutoka kwa Mkuu wa Idara ya Mipago Miji Ofisi ya Ardhi Kanda ya
Kaskazini Nickson Mjema (Kulia) wakati akikagua moja ya sehemu ya
kuhifadhia nyaraka za ardhi wakati akikagua inayotarajiwa kuwa ofisi ya
ardhi mkoa wa Tanga akiwa katika ziara yake mkoani humo. Kushoto ni Mkuu
wa Mkoa wa Tanga Martine Shighela.
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi akitekeleza
majukumu katika gari yake wakati wa ziara yake mkoani Tanga mwishoni mwa
wiki. Wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Tanga Martine Shighela, wa tatu
kushoto ni Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji na wa kwanza kushoto
ni Mkuu wa Idara ya Mipago Miji Ofisi ya Ardhi Kanda ya Kaskazini
Nickson Mjema (Kulia).(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
………………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM TANGA
Waziri
wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amewataka Wakuu
wa mikoa nchini kuhakikisha wanaharakisha uanzishwaji Ofisi za Ardhi za
mikoa ili kusaidia upatikanaji huduma za ardhi katika mikoa hiyo.
Lukuvi
alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki mkoani Tanga wakati alipokagua
ofisi zinazotarajiwa kuwa za ardhi katika mkoa huo ikiwa ni utekelezaji
wa agizo alilolitoa la kuanzisha ofisi za ardhi kila mkoa kwa ajili ya
kusogeza huduma za ardhi kwa wananchi.
Katika
Mkutano wa Wataalamu wa sekta ya ardhi uliofanyika hivi karibuni jijini
Dodoma Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi alitangaza
kuanzisha ofisi za ardhi katika kila mkoa ili kurahisisha huduma za
sekta hiyo ambapo sasa zinapatikana katika Kanda tisa ikiwemo ile Maalum
ya Morogoro.
Lukuvi
alisema, uharakishwaji uanzishaji ofisi za ardhi katika mikoa utasaidia
wananchi kupata huduma za ardhi katika mikoa yao tofauti za sasa ambapo
hulazimu baadhi yao kutembea umbali mrefu kufuatilia nyaraka ofisi za
kanda jambo aliloeleza linawakatisha tamaa.
Alimpongeza
mkuu wa Tanga Martine Shighela kwa kuwa Mkuu wa mkoa wa kwanza kukubali
na kupokea agizo la kuanzishwa ofisi hizo za ardhi mapema kwa lengo la
kuhakikisha migogoro ya ardhi inaondolewa katika mkoa wake.
Alisema,
pamoja na uwepo ofisi za Kanda ambazo baadhi yake zinahudumia zaidi ya
mikoa miwili lakini kero kwa wananchi kuhusiana na masuala ya ardhi
zinaendelea ndiyo maana Wizara yake imeona ianzishe ofisi za mikoa
zitakazokuwa zikitoa huduma kama zile zinazotolewa katika kanda.
Alizitaja
huduma hizo kuwa ni Upimaji, Uthamini, Mipango Miji, Usajili na Utoaji
Hati za ardhi aliloueleza kuwa ulikuwa ukipatikana ofisi za kanda pekee
jambo lililokuwa likiwalazimu wananchi kutembea umbali mrefu kufuata
huduma hiyo na kufafanua kuwa, uwepo ofisi za mikoa utaongeza ari ya
wananchi kuchukua hati kutokana na ukaribu wa ofisi.
‘’Mtu
atoke Korogwe afuate hati Moshi, trend ya kuchukua hati inapungua
kutokana na umbali maana maeneo mengine mtu anavuka mikoa miwili kwenda
kuifuata Hati na Kamishna aliyeko Moshi ni vigumu kusimamia mikoa iliyo
mbali’’ alisema Lukuvi.
Kwa
mujibu wa Lukuvi, binafsi alitaka mikoa yote 26 kuanzisha ofisi za
ardhi za mikoa kufikia Oktoba mwaka huu na Hati zitolewe katika mikoa
hiyo jambo alilolieleza kuwa litapunguza kero na kuongeza wigo mpana wa
makusanyao ya kodi ya pango la ardhi.
Lukuvi
alibainisha kuwa, baada ya kuanzishwa ofisi za mikoa sasa ramani zote
na historia ya masuala ya ardhi katika mikoa husika zitarudi katika
ofisi hizo na Wakuu wa Mikoa hawatakosa msaada katika masuala ya ardhi
kwa kuwa watalaamu wa ardhi watakuwa wakifanya kazi chini yao.
Kabla
ya kukagua ofisi hizo Waziri Lukuvi alielezwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga
Martin Shighela kuwa, mkoa wake ulipokea kwa shauku kubwa uamuzi wa
Serikali kuanzisha ofisi za ardhi katika mikoa na tayari umeshatenga
ofisi hizo kwa ajili ya kuanza kazi ili kupunguza migogoro ya ardhi
pamoja na kusogeza huduma karibu kwa wananchi.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Tanga Daud Mayeji alisema,
uanzishwaji ofisi ya ardhi katika mkoa wa Tanga utausaidia sana mkoa huo
kwa kuwa wamekuwa wakitumia muda mwingi kushughulika na masuala ya
ardhi na hufanya zaidi ya safari 50 katika kipindi cha miezi mitatu
kufuata huduma ya ardhi katika ofisi za kanda zilizoko Moshi mkoani
Kilimanjaro.
Kwa
mujibu wa Mkurugenzi huyo wa Jiji la Tanga, uwepo wa ofisi za Ardhi za
Mikoa itakuwa rahisi kwa jiji lake kushughulika na masuala mengine
badala ya kujikita katika ardhi pekee suala alilolieleza lilikuwa
likichukua muda mwingi.
No comments:
Post a Comment