Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiwasalimia wananchi wa Kata ya Rutamba, akiwa mkoani Lindi katika
ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akiwahutibia wananchi wa Kata ya Rutamba, kwenye mkutano wa hadhara,
akiwa mkoani Lindi katika ziara ya kikazi ya siku mbili, Agosti 23.2019.
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akimuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Lindi, Samwel Gunza,
kuhakikisha maji yanatoka katika Kata ya Rutamba, mkoani Lindi, Agosti
23.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
***************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Bw. Shaibu Ndemanga ampelekee
taarifa za utendaji kazi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya Bw.
Waryoba Gunza baada ya kushindwa kutoa maelezo kuhusu utekelezaji wa
mradi wa maji kata ya Rutamba.
Ametoa agizo hilo leo (Ijumaa,
Agosti 23, 2019) wakati akizungumza na wananchi katika Mkutano wa
hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Rutamba akiwa katika ziara yake ya
kikazi ya kukagua shughuli za maendeleo na huduma za jamii mkoani
Lindi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
baada ya kumtaka Mkurugenzi huyo atoe maelezo ya namna gani
walivyojipanga katika kutekeleza mradi wa maji kwenye kata hiyo ambayo
wakazi wake wanakabiliwa na tatizo la upatikanaji wa maji na kushindwa
kutoa maelezo.
Kwa mujibu wa Mhandisi wa Maji
wa Wilaya ya Lindi, Bw………alisema mradi wa kata hiyo unakabiliwa na
tatizo la uchakavu wa miundombinu na ukarabati wake unahitaji bajeti sh.
milioni 75 ambazo wameziomba kutoka Wizara ya Maji.
Waziri Mkuu amesema miradi
yote ambayo gharama zake ziko chini ya sh. milioni 100 inatakiwa
itekelezwe kwa kutumia fedha za ndani ya halmashauri husika.
“Miundombinu hiyo ilitakiwa iwe imebadilishwa. Mradi wa sh. milioni 75
unaomba fedha wizarani ni uvivu.”
Waziri Mkuu amesema suala la
huduma ya maji limewekewa msisitizo na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kuanzisha kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwawezesha
wananchi kupata maji safi na salama karibu na makazi yao.
Waziri Mkuu aliwaambia wananchi
kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kuondoa
tatizo la maji kote nchini ili kusaidia wananchi hao hasa wanawake
kutumia muda mwingi kufanya kazi za maendeleo kuliko kutafuta maji.
Hata, hivyo Waziri Mkuu
amewahakikisha wananchi hao kwamba licha ya kuagiza mradi huo wa
ukarabati wa miundombinu ya kusambazia maji ufanyike kwa haraka, pia
Serikali inatekeleza mradi mwingine wa maji wa Milola ambao ukikamilika
maji yatafikishwa hadi Rutamba.
Wakati huo huo,Waziri Mkuu
amewaagiza Wakuu wa Wilaya nchini wahakikishe wanawasimia vizuri
watumishi wa umma na kuwachukulia hatua wote watakaobainika kushindwa
kutekeleza majikumu yao ipasavyo.
“Rais Dkt. John Pombe Magufuli ana
nia njema ya kuwapa huduma safi wananchi wote hadi wanyonge na
ameelekeza wahudumiwe vizuri bila ya ubaguzi. Wananchi kama kuna
mtumishi asiyewahudumia vizuri msisite kumtaja kwa sababu Serikali hii
haitomvumia.”
Waziri Mkuu asema ni lazima kila
mtumishi wa umma anayelipwa mshahara kwa kutumia kodi za wananchi
ahakikishe anatekeleza ipasavyo majukumu yake kwani asipofanya hivyo
hatokuwa na nafasi ya kuendelea na kufanya kazi ndani ya Serikali.
“Watumishi fanyeni kazi kwa bidii
na msitarajie kuundiwa tume pale mnapofanya vibaya, ukiharibu kazi
tunakushughulikia hapo hapo na huu ndio msimamo wa Serikali ya Awamu ya
Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli.”
Waziri Mkuu amesema kuwa
watumishi wanatakiwa wafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni za
kazi na pia watambue dhamana kubwa waliyonayo, ambayo ni kuwahudumia
wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Amesema watumshi wa umma
hawapaswi kukaa maofisini bali wanatakiwa wapange siku nne katika juma
kwa ajili ya kwenda kutembelea wananchi hususani waishio maeneo ya
vijijini kwa ajili ya kuwasikiliza kero zao na kuzipatia ufumbuzi.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imedhamiria kuboresha huduma za jamii ambazo zilikuwa zikiwakwaza
wananchi zikiwemo za miundombinu ya barabara, tatizo la maji, elimu na
afya, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania wote waishi vizuri.
Awali, akizungumza kwaniaba ya
wabunge wa mkoa wa Lindi, Mbunge wa Viti Maalumu, Riziki Lulida alisema
wakazi wa kata ya Rutamba wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa
huduma ya maji licha ya kuwepo kwa vyanzo, hivyo aliiomba Serikali
iwasaidie.
Hata hivyo alilalamikia kuwepo kwa
uharibifu mkubwa wa mazingira katika maeneo hayo ikiwemo uvamizi katika
vyanzo vya maji pamoja na ukataji hovyo wa misitu unaohatarisha kuibuka
kwa jangwa, ambapo Waziri Mkuu ameagiza viongozi wa wilaya hiyo
kuzishughulikia suala hilo.
No comments:
Post a Comment