Na.AlexMathias,Dodoma
SIKU mbili baada ya mashine ya
Ultrasound kuibiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu,
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe Suleiman Jafo amemtaka Mkuu
wa Mkoa huo, Anthony Mtaka kuunda tume maalum ya kuchunguza tukio hilo.
Mashine hiyo inadaiwa kuibiwa
pamoja na kifaa chake cha kudurufu picha (printer) ambapo ilikua maalumu
kwa matumizi ya wodi mpya ya akina Mama wajawazito na iliibiwa ikiwa
katika wodi hiyo.
Akizungumza jijini Dodoma, Waziri
Jafo amesema hajafurahishwa na kitendo cha mashine hiyo kuibiwa kwa
sababu kinarudisha nyuma maendeleo makubwa ambayo Serikali imeyafanya
katika sekta ya Afya nchini.
” Kitendo cha mashine hii kuibiwa
kinaonesha jinsi gani wapo watu wenye nia ovu ya kurudisha nyuma
Uwekezaji ambao Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeufanya
katika sekta ya afya, sasa nitoe maelekezo kwa Mkuu wa Mkoa kuhakikisha
anatuma Timu ya kwenda kuchunguza ili tujue mashine hiyo
iliibiwaje,”amesema Waziri Jafo.
Aidha ametengua kauli ya Mkuu wa
Wilaya ya Bariadi aliyoagiza watumishi 137 wa Hospitali hiyo kuchangia
kutoka kwenye mishahara yao ndani wiki moja ili kulipa machine hiyo
iliyoibiwa.
” Maelekezo yangu ni kwamba
kutokana na hali iliyojitokeza huko Timu itakayoundwa kuchunguza tukio
hilo inapaswa ije na majibu ambayo tutawajua waliofanya wizi huo ambapo
kwanza watapaswa kurudisha mashine hiyo kisha wachukuliwe hatua za
kisheria ikiwemo kupandishwa mahakamani.
” Kuhusu watumishi 137 kulipia
mashine hiyo kutoka kwenye mishahara yao, nielekeze kuwa watumishi hawa
wanafanya kazi kwenye mazingira magumu kitendo cha kuwaambia walipe ni
kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma,” amesema Waziri Jafo.
Amezitaka mamlaka za Wilaya ya
Bariadi kutowachangisha fedha watumishi hao na badala yake wajielekeze
katika kuhakikisha wanawapata waliohusika na wizi huo ili wachukuliwe
hatua.
No comments:
Post a Comment