Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula
akiwasikiliza baadhi ya wafugaji na wakulima wanaoishi katika hifadhi ya
Wembele iliyopo kijiji cha Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora
alipokwenda kusuluhisha mgogoro baina yao wakati wa ziara yake ya
kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na
kukagua masijala za ardhi katika mkoa wa Tabora jana
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa
katika picha ya pamoja na baadhi ya wafugaji na wakulima wanaoishi
katika kijiji cha Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipokwenda
kusuluhisha mgogoro baina yao wakati wa ziara ya kuhamasisha ukusanyaji
maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua masijala za ardhi
katika mkoa wa Tabora jana.
Naibu
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa
na Mkuu wa Wilaya ya Igunga John Mwaipopo wakiwasili kijiji cha
Makomelo wilaya ya Igunga mkoani Tabora alipokwenda kusuluhisha mgogoro
kati ya wafugaji na wakulima wakati wa ziara yake ya kuhamasisha
ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya ardhi na kukagua
masijala za ardhi katika mkoa wa Tabora jana (PICHA ZOTE NA HASSAN MABUYE WIZARA YA ARDHI)
…………………………………………………
Na Munir Shemweta, WANMM IGUNGA
Serikali
imeagiza kaya 13 zilizopo eneo la wafugaji katika hifadhi ya Wembele
kijiji cha Makomelo kitongoji cha Kitulo wilayani Igunga mkoani Tabora
kuondoka katika eneo hilo kwenda eneo ililopangiwa la wakulima ili
kuondoa mgogoro wa muda mrefu kati ya wafugaji na wakulima.
Kauli
hiyo ya serikali inafuatia wakulima kuvamia eneo la wafugaji katika
kijiji hicho na kuzuia wafugaji kulisha mifugo yao jambo lililokiuka
makubaliano ya awali ya kila upande kubaki katika eneo lake kwa ajili ya
shughuli zake.
Akizungumza
na pande mbili za wafugaji na wakulima katika kijiji cha Makomelo akiwa
katika ziara yake ya kuhamasisha ukusanyaji maduhuli ya serikali
kupitia kodi ya pango la ardhi na kukagua Masijala ya Ardhi katika mkoa
wa Tabora jana tarehe 24 Agosti 2019, Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alisema serikali haiwezi
kuendelea kuona watu wanapigana na kuuana wakati mipaka ya eneo hilo
ilishawekwa.
Alisema,
eneo linalogombaniwa na pande hizo mbili linajulikana kama eneo la
hifadhi ya Wembele chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii lakini kwa
busara serikali iliamua kutoa matumizi kwa ajili ya wakulima na wafugaji
na kuweka mipaka lakini wakulima wameamua kukiuka utaratibu na kuvamia
eneo la wafugaji kitu alichokieleza kuwa hakikubaliki.
‘’Waliokiuka
utaratibu wa awali waondoke, ziko kaya 13 hatuwezi kuendelea na vifo
katika haya, serikali ishaweka mipaka kinachotakiwa ni kuheshimu
maamuzi’’ alisema Dkt Mabula
Kwa
mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
kinachotakiwa kwa pande mbili zinazogombana ni kuheshimu makubaliano
hadi hapo Wizara ya Maliasili na Utalii itakalichukua eneo lake.
Aliwataka
wafugaji na wakulima wasiendelee kufanya vurugu na kuheshimu
makubaliano waliyokubaliana awali ambapo alimuagiza Mkuu wa wilaya ya
Igunga mkoani Tabora John Mwaipopo kuhakikisha anasimamia zoezi la
kuondoka kwa kaya 13 katika eneo la wakulima.
Mwenyekiti
wa Kitongoji cha Kitulo katika Kata ya Igunga Zephania Ndassa
alimueleza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa,
eneo hilo limekuwa na mgogoro mkubwa kati ya wakulima na wafugaji pamoja
na kuwepo makubaliano yaliyofikiwa mwaka 2004 wakati wa uongozi wa Mkuu wa mkoa wa Tabora wakati huo Marehemu Abbas Kandoro.
Kwa
mujibu wa Ndassa pande zinazopingana zinatambua kabisa kama eneo hilo
ni hifadhi ya Wembele tangu mwaka 2002 na wao wanalitumia eneo hilo
wakifahamu pindi litakapohitajika litachukuliwa na Maliasili lakini
mgogoro huo umekuwa ukuwasumbua.
Naye
Mkazi wa kijiji cha Makomelo Christopher Shigela alimuomba Dkt Mabula
kunusuru mgogoro huo uliodumu kwa muda mrefu hasa baada ya juhudi za
wilaya na mkoa kugonga mwamba na kubainisha kuwa, pamoja na uwepo alama
zilizoainisha maeneo ya wakulima na wafugaji lakini wakulima wameendelea
kufanya uvamizi jambo lililozusha mgogoro uliosababisha watu kuumia na
wengine kupoteza maisha.
No comments:
Post a Comment