Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiongea na Viongozi na Watumishi wa Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, katika ukumbi wa Halmashauri Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua darasa
lililokarabatiwa la Shule Kongwe ya Same Sekondari, mkoani
Kilimanjaro Julai 19.2019. Kulia ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Same
Sekondari Hoza Mgonja. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akikagua maabara katika
Shule Kongwe ya Same Sekondari, kabla ya kuzindua mradi wa ukarabati wa
shule hiyo kongwe, mkoani Kilimanjaro Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya
Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia darasa
lililokarabatiwa la Shule Kongwe ya Same Sekondari, katika mradi wa
ukarabati wa shule hiyo kongwe mkoani Kilimanjaro, Julai 19.2019. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiangalia vitabu katika maktaba
iliyokarabatiwa ya Shule Kongwe ya Same Sekondari, katika mradi wa
ukarabati wa shule hiyo kongwe mkoani Kilimanjaro, Julai 19.2019.
Kushoto ni Mwalimu Mkuu wa Shule ya Same Sekondari Hoza Mgonja. (Picha
na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizindua mradi
wa ukarabati wa shule kongwe ya Same Sekondari, iliyoko wilayani Same
katika mkoa wa Kilimanjaro, Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri
Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wanafunzi wa Same Sekondari mara baada ya kuzindua mradi
wa ukarabati wa shule hiyo kongwe, iliyoko wilayani Same katika mkoa wa
Kilimanjaro, Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa, akimsikiliza mwanafunzi wa Same Sekondari, Omari
Pundugu, akielezea changamoto mafanikio na changamoto za shule hiyo mara
baada ya uzinduzi wa mradi
wa ukarabati wa shule hiyo kongwe, iliyoko wilayani Same katika mkoa wa
Kilimanjaro, Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi,
baada ya kuzindua mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya Same Sekondari,
mkoani Kilimanjaro Julai 19.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
*************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wawe na mipango ya kazi ambayo itaweza kupimika na kutoa matokeo.
“Kila mtumishi anapaswa awe na
mpango kazi katika sekta yake na ni lazima aende kupima matokeo. Awamu
hii, tunataka kuona matokeo ya kazi zenu.”
Ametoa kauli hiyo leo asubuhi
(Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya
Same kwenye ukumbi wa Halmashauri ya wilaya hiyo, mjini Same.
“Watumishi mmeletwa kwenye
wilaya hii ili muwahudumie wananchi. Tulioajiriwa, kazi yetu kubwa ni
kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wowote uwe ni wa kabila, itikadi au
rangi.”
Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuwakumbusha watumishi hao kwamba baada ya mchujo wa watumishi
hewa, waliobakia wanapaswa kufanya kazi kwa bidii.
“Fanyeni kazi kwa bidii,
msimamo wa Serikali hii ni kwamba hatumvumilii mtumishi ambaye si
mwajibikaji, ni mwizi, mzembe au anaomba rushwa. Serikali hii hatuna
muda wa kujadili matatizo ya watumishi, tunamalizana hapo hapo,”
amesema.
Amewataka watumishi hao
wasimamie utekelezaji wa ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya
Chama cha Mapinduzi kwa sababu ndiyo chama tawala.
“Mtumishi angalia sekta yako
inasema nini, ifanyie kazi. Kama ni maji, tafuta ni wapi yanapatikana,
changanua zinahitajika shilingi ngapi, tafuta njia ya kupata hizo fedha
ili wananchi wapate maji.”
Kuhusu tabia ya kukaa ofisini,
Waziri Mkuu amekemea tabia hiyo na kuwataka watumishi wote nchini
waache tabia ya kukaa ofisini na badala yake waende vijijini
kuwasikiliza wananchi.
“Watumishi wa umma msikae
ofisini. Nendeni vijijini walau kwa siku nne za juma. Hizo mbili
zinazobakia, zitumieni kuandaa taarifa. Nendeni huko ili wananchi
wasipate usumbufu wa kuja hapa mjini kuwatafuta,” amesisitiza.
“Mkuu wa Wilaya simamia zoezi
la wakuu wa idara na wasaidizi wao kwenda vijijini. Wakienda vijijini ni
lazima waonane na waheshimiwa madiwani, washirikiane kusikiliza kero na
kutafuta majibu kwa wananchi. Huo ndiyo mshikamano wenyewe
unaohitajika,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amewataka watumishi wa umma watambue mipaka yao na wajenge mahusiano baina yao na wengine.
Alitoa kauli hiyo jana jioni
(Alhamisi, Julai 18, 2019) wakati akizungumza na watumishi wa Manispaa
ya Moshi, kwenye ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
“Kila mmoja lazima atambue
mipaka yake na mamlaka baina yake na wengine. Hapa mko wateuliwa,
waajiriwa na wachaguliwa. Kila mtu ana nafasi yake ya kuwatumikia
wananchi.
Aliwataka watumishi hao
watambue falsafa ya Kiongozi mkuu wa nchi ambayo inahimiza uchapakazi.
“Kwa hiyo tunaposema Hapa Kazi Tu, maana yake chapa kazi na tuone
matokeo. Tunasisitiza kazi na tunataka kazi unayoifanya, itoe matokeo,”
alisema.
No comments:
Post a Comment