WAZIRI MKUU AAGIZA SAME SEKONDARI IPEWE GARI
*DED aahidi kuliwasilisha kesho kutwa jioni
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Same, Bi. Anna-Clare Shija
apeleke gari haraka katika shule ya sekondari ya wavulana ya bweni ya
Same ili kumsaidia mwalimu mkuu endapo kutatokea dharura.
“Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 800
lazima iwe na chombo cha usafiri kitakachotumika kwa dharura za
kuwapeleka hospitali wanafunzi pale wanapougua. Sasa hivi mwanafuzi
akiugua, Mwalimu Mkuu anafanyaje? Ni kama ameachiwa jukumu hili peke
yake,” alisema Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo jana
(Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati alipotembelea shule hiyo na kuzindua
mradi wa ukarabati wa shule kongwe ya sekondari ya Same na kisha
kuzungumza na wanafunzi, walimu na baadhi ya wazazi waliokuwepo.
Waziri Mkuu alimwita Mkurugenzi wa wilaya
hiyo, Bi. Shija na kumtaka atoe jibu hadharani kwamba ni lini atapeleka
gari hilo shuleni hapo. Mkurugenzi huyo aliahidi kulipeleka gari hilo
ifikapo Jumatatu jioni (Julai 22, 2019).
“Haya maelekezo ni kwa wakurugenzi wa
Halmashauri zote nchini wenye shule ambazo zina wanafunzi zaidi ya 700.
Mnapaswa kuhakikisha kunakuwa na gari la shule ili ikitokea dharura,
Mkuu wa Shule aweze kuingilia kati na kupata ufumbuzi.”
“Wakurugenzi mnatakiwa kutambua shule
hizi ni zenu, kwa hiyo mnalo jukumu la kuzihudumia. Shule hii ya Same
ina wanafunzi zaidi ya 800 na wanalala hapa hapa, ni lazima kuwe na gari
la kuwahudumia hasa wakati wa dharura.”
Pia amemuagiza Mkurugenzi huyo atafute
daktari na muuguzi mmoja na awapangie kwenye shule hiyo ili waweze
kutoka huduma kwa wanafunzi na kuwapunguzia adha ya kwenda mjini
kutafuta huduma hiyo.
Waziri Mkuu alifikia uamuzi huo baada ya
kupokea changamoto zilizowasilishwa na kijana Omary Said wa kidato cha
sita mchepuo wa PCB ambaye alisema shule hiyo inakabiliwa na uhaba
mkubwa wa maji; uchakavu wa mabweni; ukosefu wa zahanati ya shule na
uhaba wa walimu wa sayansi hasa wa masomo ya fizikia.
Mapema, akitoa taarifa
ya ukarabati, mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bw. Hoza Mgonja alisema
ukarabati huo ambao umegharimu sh. milioni 919, ulifanikisha ukarabati
wa majengo saba ya madarasa yenye vyumba 22; maabara tatu, vyoo viwili
vyenye matundu tisa; jengo moja la walimu; maktaba yenye vyumba viwili
na ofisi mbili; vyoo viwili vyenye matundu manne na miundombinu ya umeme
na majitaka.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake
mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na
watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua
mradi wa maji wa Same – Mwanga – Korogwe.
No comments:
Post a Comment