
***************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema hatua ya kudhibiti upotevu wa mapato na matumizi ya fedha za
Serikali, uboreshwaji wa mazingira ya biashara na uwekezaji pamoja na
kusimamia uwajibikaji kwa watumishi wa umma kumesababisha kukua kwa
uchumi.
Amesema Tanzania ni nchi yenye
amani na utulivu na Serikali imeendelea kuongeza nguvu katika kudumisha
amani na utulivu kwenye maeneo yote nchini, hali inayotoa fursa kwa
wananchi wake kuendeleza shughuli zao za maendeleo.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumatatu, Julai 8, 2019) wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na
Waziri Mkuu wa Misri, Dkt. Mostafa Madbouly akiwa katika siku yake ya
kwanza ya ziara yake ya kikazi nchini Misri.
Hivyo, amemuhakikishia Waziri Mkuu
wa Misri kwamba Serikali ya Tanzanzia na wananchi wake wapo tayari
kuendelea kushirikiana na Serikali ya nchi hiyo na wananchi wake katika
kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili.
Amesema nchi za Tanzania na Misri
zinahitaji kutumia nafasi ya ushirikiano wa kibiashara na uwekezaji
katika ukuzaji wa uchumi, hivyo Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo
kuwakaribisha wawekezaji na wafanyabiashara kutoka Misri waje kuwekeza
nchini.
Amesema Serikali ya Tanzania
imefanikiwa kiuchumi na kwa sasa ni nchi pili ambayo uchumi wake unakua
kwa kasi barani Afrika, ikitanguliwa na nchi ya Ivory Coast. Uchumi wa
Tanzania ulitarajiwa kukua kwa asilimia 7.2 mwaka jana kutoka asilimia
saba.
“Hali ya uchumi wa Tanzania
inaendelea vizuri, tumeendelea kushuhudia kushuka kwa mfumuko wa bei
ambapo kwa sasa tumefikia asilimia 3.2, kiwango hiki ni matokeo ya
kukuza sekta za madini, ujenzi, mawasiliano, utalii pamoja na kushuka
kwa bidhaa za chakula na mafuta. Tunatarajia kiwango hiki kitashuka
zaidi kwa sababu ya uwekezaji”.
Waziri Mkuu amesema Serikali ya
Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, kipaumbele chake
kilikuwa ni kukuza kiwango cha uchumi kutoka cha chini kwenda cha kati
ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.
No comments:
Post a Comment