Saturday, July 13, 2019

SUALA LA KUWAONDOA WATUMISHI WALA RUSHWA, WAZEMBE NI ENDELEVU-MAJALIWA

*****************

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema suala la kuwaondoa kazini watumishi wa umma ambao ni wazembe, wala rushwa na wasiotimiza majukumu yao ipasavyo ni endelevu.
‘Serikali inahitaji watumishi wenye heshima na nidhamu ya kazi ili waweze kuwatumikia wananchi bila ya ubaguzi wa aina yoyote iwe wa kiuchumi, kidini au kikabila.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Jumamosi, Julai 13, 2019) wakati akihutubia mwananchi katika kongamano la kumpongeza Rais Dkt. John Magufuli kwa utekelezaji wa ilani.
Kongamano hilo limeandaliwa na Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) ili kumpongeza Rais Dkt. Magufuli lilifanyika katika uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Amesema Serikali imejipanga vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa, hivyo amewataka wananchi watoe taarifa iwapo watabaini uwepo wa watumishi wanaojihusisha na rushwa.
“Watumishi wa umma tunataka watambue kwamba wao ni watumishi wa wananchi, hivyo hawana budi kutambua wajibu wao ambao ni kuwatumikia mwananchi ipasavyo.”
Amesema kuwa Serikali imepiga hatua kubwa katika vita dhidi ya rushwa ambapo kwa Afrika Tanzania inaongoza kwa mujibu wa ripoti ya taasisi ya Transparency Internation.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa UWT, Queen Mlozi amesema kongamano hilo ni muendelezo wa makongamano mengine ya kumpongeza Rais yaliyofanyika kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Mbeya na Unguja na Pemba.
Amesema viongozi hao wameonesha dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo. “Tutaendelea kushirikiana na viongozi wetu na hatupo tayari kugawanyika.”
Awali, Mawaziri na Manaibu Waziri mbalimbali walipata fursa ya kuelezea namna ilani ilivyotekelezwa katika maeneo mbalimbali kupitia wizara zao.
Katika kongamano hilo viongozi na wanachama wa vyama mbalimbali walivihama vyama vyao na kujiunga na CCM akiwemo na aliyekuwa Kalibu wa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe.

No comments:

Post a Comment