SERIKALI YATOA MILIONI 700 KUSAIDIA KAZI WABUNIFU NCHINI
Na Mwandishi Wetu
MAELEZO
DAR ES SALAAM
NAIBU Waziri
wa Elimu Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha amesema Serikali
kupitia Tume ya Tafa ya Sayansi na Teknolojia ( COSTECH) imetoa kiasi
cha Tsh Milioni 700 kwa wabunifu 60 ili kuendeleza tafiti na bunifu zao
na kuleta tija na manufaa kwa Taifa.
Akizungumza
leo Jumatano (Julai 10, 2019) wakati wa Kongamano maalum la Ubunifu
lililoandaliwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE)
kwa kushirikiana na COSTECH katika Maonesho ya 43 ya Biashara ya
Kimataifa Dar es Salaam (DITF), Ole Nasha alisema Serikali itaendelea
kuwatambua wabunifu na wagunduzi wa kazi mbalimbali nchini.
Ole Nasha
alisema kwa sasa wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi za ugunduzi na
bunifu za kazi mbalimbali lakini zimeshindwa kutambulika na hivyo
kuilazimu Serikali kuanza kuweka utaratibu maalum ikiwemo kuandaa
mwongozo unaotarajiwa kuwatambua wabunifu hao katika ngazi mbalimbali.
“Mwaka jana
tuliandaa mashindano maalum ya ubunifu na walipatikana washindi wa
kitaifa 60, kwa kutambua umuhimu wa kazi zao, pamoja na kutoa fedha pia
tumeanza mchakato wa kutoa mwongozo maalum wenye utaratibu wa kuendesha
vituo vya teknolojia na ubunifu” alisema Ole Nasha.
Aidha Ole
Nasha aliitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuandaa kongamano la kila
mwaka kwa ajili ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wabunifu hao kwa
ajili ya kupokea maoni, ushauri na mapendekezo mbalimbali kwa kuwa hatua
hiyo itasaidia kubaini kazi mbalimbali za wabunifu na watafiti na
kuweza kutambulika.
Kwa mujibu
wa Ole Nasha alisema wabunifu na wagunduzi nchini kutambua kuwa masuala
ya ubunifu hayana kiwango cha elimu na kuwataka wabunifu wasio katika
sekta rasmi kuendelea kubuni bidhaa na vifaa mbalimbali kwa kuwa COSTECH
si taasisi inayowagusa wasomi peke yao bali wabunifu wote waliopo
katika maeneo mbalimbali nchini.
Akifafanua
zaidi Ole Nasha alisema kutokana na wabunifu na watafiti wengi
kukabiliwa na changamoto ya kuibiwa kazi zao, aliitaka COSTECH kukaa
pamoja na Wakala wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA) ili
kuhakikisha kuwa wabunifu wanawekewa utaratibu maalum kwa ajili ya
kulinda bunifu zao.
Kwa upande
wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Tekonolojia, Prof.
James Mdoe alisema Serikali itaendelea kuzitambua kazi mbalimbali za
wabunifu na wagunduzi nchini ili kuhakikisha kuwa kunakuwepo na
ushirikiano madhubuti kwa ajili ya kutambua na kuendeleza kazi za
ubunifu na ugunduzi nchini.
Naye Mbunifu
wa Maji taka kutoka Kampuni ya Biocon Africa Ltd, Prof. Karoli Njau
aliitaka COSTECH kuweka utaratibu wa kuwakutanisha wabunifu na wagunduzi
wote nchini ili waweze kuonyesha kazi zao na kuhakikisha kuwa kuna
utaratibu mzuri wa kuwapata watoa huduma katika kazi mbalimbali
zinazoweza kupatikana nchini.
No comments:
Post a Comment