Monday, July 15, 2019

NATOA SIKU SABA KITUO CHA AFYA IBABA KIANZE KAZI-BRIGEDIA MWANGELA

Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela akizungumza na viongozi katika humba cha upasuaji katika kituo cha Afya Ibaba ambapo ameagiza huduma zianze kutolewa ndani ya siku saba.
Majengo ya Kituo cha Afya Ibaba, Wilaya ya Ileje yaliyojengwa kwa fedha za serikali shilingi milioni 400 ambayo yamekamilika lakini huduma za Afya hazijaanza kutolewa.
***************
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela amempa siku saba Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ileje ahakikishe kuwa kituo cha Afya cha Ibaba Wilayani humo kinatoa huduma za Afya hususani huduma za Mama na mtoto,
Brigedia Mwangela ametoa agizo hilo mara bada ya kukagua maendeleo ya ujenzi katika kituo hicho na kukuta miundombinu yote muhimu ikiwa ni pamoja na majengo yote yakiwa yamekamilika lakini huduma za afya hazitolewi.
“Mkurugenzi nakups siku saba akina mama na watoto waanze kupata huduma hapa, kituo hiki kimekamilika isipokuwa kwa mambo machache ambayo yapo ndani ya uwezo wenu”, amesisitiza Brigedia Mwangela.
Amemuelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha kuwa Daktari aliyepaswa kuhudumia kituo hicho anafika siku ya Jumatatu na pia halmashauri ihakikishe ujenzi wa njia za wagonjwa (walkways) wenye thamani ya shilingi milioni 20 unakamilika mapema.
Aidha Brigedia Mwangela amewataka wananchi wa Ibaba kukitunza na kukitumia hicho na endapo kutakuwa na ucheleweshwaji wa kuanza kutolewa huduma watoe taarifa ofisini kwake.
“Wananchi wa Ibaba nia ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za Afya ndio maana kumekuwa na ujenzi wa Kituo hiki, sasa ikifika Jumatatu Daktari hamjamuona hapa mnitaarifu na mkiona imefika siku ya ijumaa akina mama na watoto hawapati huduma hapa nijulisheni”, amesema Brigedia Mwangela
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Kheri Kagya amesema serikali imetoa shilingi milioni 400 zilizojenga majengo ya upasuaji, maabara, jengo la kuhifadhia maiti, wodi ya wazazi na nyumba ya daktari pia imepeleka vifaa vya kutolea huduma vyenye thamani ya shilingi milioni 92.2 katika kituo hicho.
Dkt. Kagya ameeleza kuwa kwa majengo ambayo tayari yamekamilia na vifaa vilivyokwisha tolewa kituo hicho kinaweza kutoa huduma za mama na mtoto isipokuwa huduma ya upasuaji ambayo itahitaji uwepo wa njia ya kupitia wagonjwa (Walkways).
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ileje Joseph Mkude amemueleza Mkuu wa Mkoa kuwa watazingatia maagizo yake na kuhakikisha wananchi wa Ibaba wanapata huduma za Afya katika kituo hicho ndani ya siku ya saba walizopewa.

No comments:

Post a Comment