MTATURU (CCM) APITA BILA KUPINGWA JIMBO LA SINGIDA MASHARIKI
Mgombea ubunge wa CCM Singida Mashariki,
Miraji Mtaturu ndio pekee aliyerejesha fomu za kuwania nafasi hiyo kati
ya wagombea 13 waliojitokeza.
Mtaturu amerejesha fomu hiyo leo Alhamisi
Julai 18, 2019 kabla ya saa 10:00 jioni, muda ambao wagombea wote
waliochukua fomu walitakiwa kuwa wamezirejesha.
Wagombea wengine waliochukua fomu ni
Hamidu Hussein (ADA-Thadea), Tirubya Mwanga (UPDP), Ameni Npondia (CCK),
Amina Ramadhan (DP) na Ayuni John (UDP).
Wengine ni Amina Mcheka (AAF), Maulid
Mustafa (ADC), Selemani Ntandu (CUF), Feruzy Fenezyson (NRA), Abdallah
Tumbo (UMD), Donald Mwanga (TLP) na Masalio Kyara (SAU).
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni
Ofisa Mipango wa Halmashauri ya Ikungi, Thomas Mwailafu akizungumza na
Mwananchi amesema hadi muda wa mwisho wa uchukuaji na urejeshaji fomu
unamalizika, ni Mtaturu pekee ndio aliyerejesha fomu.
Uchaguzi katika jimbo hilo utafanyika
Julai 31, 2019 kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Tundu Lissu aliyepoteza
sifa za kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na utoro
bungeni.
Tayari Mwailafu amebandika fomu ya
Mtaturu katika mbao za matangazo wa ofisi ya halmashauri ya Ikungi ili
kutoa fursa ya watoa pingamizi hadi kesho Ijumaa saa 10 jioni.
Mwailafu amesema kama hakutakuwa na
pingamizi lolote atamkabidhi cheti cha ubunge wa jimbo hilo lililokuwa
likiongozwa na Lissu tangu mwaka 2010 hadi Juni 28, 2019.
No comments:
Post a Comment