DKT. NDUGULILE AONEKANA KUTORIDHISHWA NA UTAYARI WA MKOA WA KIGOMA KATIKA KUKABILIANA NA EBOLA
……………………..
Na WAJMW-Kigoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile leo ametembelea baadhi
ya maeneo ya Mkoa wa Kigoma kuona utayari wa mkoa huo katika kukabiliana
na ugonjwa wa Ebola.
Dkt. Ndugulile ametembelea maeneo ya
Bandari kuu ya Mkoa, Uwanja wa ndege, bandari ndogo ya Kibirizi na
Zahanati ya Bangwe ambayo imetengwa maalumu kwa ajili ya kutoa matibabu
kwa mtu atakayebainika kuwa na virusi vya Ebola.
Naibu Waziri ameonekana kutoridhishwa na
utayari wa Mkoa katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola nchini huku
akiitaka timu iliyoandaliwa chini ya Mkuu wa Wilaya Samson Anga na
Mganga Mkuu wa Mkoa Paul Chaote kuendelea kutoa mafunzo kwa timu
iliyoandaliwa jinsi ya kujikinga na kutoa huduma kwa mgonjwa
atakayebainika.
“Hatuna mgonjwa wa Ebola ndani ya nchi,
lakini kutokana na hali ya ugonjwa huu katika nchi jirani kuna umuhimu
wa sisi kama nchi kuendelea kujipanga na kuhakikisha kwamba mifumo yetu
yote imekaa vizuri kipindi mgonjwa atakapojitokeza, hivyo nakuomba Mkuu
wa Wilaya na Mganga Mkuu wa mkoa kuendelea kusimamia hili”. Amesema Dkt.
Ndugulile.
Mapungufu aliyobaini Dkt. Ndugulile ni
pamoja na wahudumu kutozingatia kanuni walizofunzwa juu ya kujikinga na
maambukizi pindi watakapokua wakihudumia mgonjwa, kutokua na vifaa vya
kutosha kwa ajili ya wagonjwa wa Ebola kama vitanda kwenye vituo vya
Isolation na watumishi kutokua na uelewa na utayari wa kutosha kwa ajili
ya kukabiliana na ugonjwa huu.
Dkt. Ndugulile yupo Mkoani Kigoma kwa
ziara ya siku tatu ambapo pamoja na maeneo mengine atatembelea mpaka wa
Manyovu ili kuona hali ya utayari ya mpaka huo kwa ajili ya kukabiliana
na ugonjwa wa Ebola na kisha atatembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Kigoma.
No comments:
Post a Comment