Tuesday, July 16, 2019

AWESO AWATAKA WAHANDISI WA MAJI RUWASA KUZINGATIA WELEDI WA KAZI

Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso,akizungumza katika kikao kazi cha Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Majisafi, Usafi na Mazingira Vijijini leo jijini Dodoma.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof Kitila Mkumbo ,akizungumza na  Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Majisafi, Usafi na Mazingira Vijijini katika kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Sehemu ya  Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Majisafi, Usafi na Mazingira Vijijini wakifatilia kikao kazi kilichofanyika jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso,akiwa katika picha ya pamoja na Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Majisafi, Usafi na Mazingira Vijijini baada ya kumaliza kikao kazi kilichofanyika leo jijini Dodoma.

………………….

Na.Alex Sonna,Dodoma

Naibu Waziri wa Maji, Mhe Jumaa Aweso amewataka Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Majisafi, Usafi na Mazingira Vijijini kufanya kazi kwa weledi na kuhakikisha wanaondoa changamoto za Maji katika maeneo yao.

Mhe Aweso ameyasema hayo wakati alipokutana na Mameneja hao jijini Dodoma ambapo amesema kwa sasa Wizara hiyo imeunda kitengo cha usanifu ambacho kitasaidia katika kuangalia upya usanifu, mikataba na gharama zinazowekwa na wakandarasi kabla ya ujenzi wa miradi.

Amewataka Mameneja hao kutumia weledi na taaluma zao kuhakikisha wanamtua mama ndoo kichwani na kuwataka kuacha mambo ya hovyo yaliyokuepo awali.

” Katika ziara zangu zote katika maeneo mbalimbali nimekua mkali sana kwa wahandisi na wakandarasi, baadhi ya wataalamu wametuangusha kwa kutumia miradi kujipatia fedha, nimejionea mwenyewe miradi mingi wakishindwa kuimaliza kwa wakati. Wakandarasi hawa hatuwezi kuwavumilia hata kidogo.

” Mhe Rais ametuamini sana katika nafasi hizi tulizoteuliwa, ni jukumu letu kumsaidia kazi na kutumia taaluma zetu kuhakikisha upatikanaji wa maji kwa wananchi waliopo vijijini inafikiwa kwa asilimia 85 au zaidi ifikapo mwaka 2020,” amesema Mhe Aweso.

Amewataka Mameneja hao kutosubiri Waziri au Katibu Mkuu kufika katika maeneo yao ya kazi na kuwaonesha changamoto badala yake waunde mikakati ya kuwawezesha kufikia maeneo yenye changamoto ya Maji ili waweze kuitatua.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Prof Kitila Mkumbo amesema malengo ya Wizara hiyo ni kuongeza upatikanaji wa Maji kufikia asilimia 84 kutoka asilimia 64 kwa maeneo ya Vijijini, lakini pia wakifikia asilimia 95 kutoka asilimia 84 kwa maeneo ya Mjini.

” Tumekua tukiwekeza sana kwenye miradi mipya lakini kama tukiongeza nguvu na kumaliza miradi ambayo imekwishaanza na kuanza kufanya basi tungekua mbali sana hivyo katika bajeti zetu lazima tupange bajeti zetu Katika kukarabati miradi ya zamani.

” Mhe Naibu Waziri kazi kubwa na ya haraka kufanywa na RUWASA ni kujenga imani kubwa kwa Mhe Rais na Wananchi, na imani hiyo itajengwa na wahandisi hawa kwa kuhakikisha miradi ya wananchi inafanya kazi lakini kubwa zaidi ni kumaliza tatizo la Maji,” amesema Prof Mkumbo.

No comments:

Post a Comment