***************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amesema ni wakati muafaka kwa Watanzania kuanza kujiwekea akiba
kwa kununua hisa kupitia taasisi za kifedha nchini ikiwemo benki ya
CRDB.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili,
Juni 16, 2019) wakati wa bonanza kati ya Wabunge na watumishi wa benki
ya CRDB lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amesema suala la
wananchi kujiwekea akiba ni muhimu kwa ajili ya maendeleo yao. “Nashauri
wananchi tutumie taasisi za fedha kujiwekea akiba pamoja na kukopa
mikopo kwa ajili ya maendeleo yetu.”
Akizungumzia kuhusu bonanza hilo
lililoandaliwa na benki ya CRDB, Waziri Mkuu amesema michezo ni sehemu
nzuri kujenga afya, furaha na kujenga mshikamano wa karibu baina ya
benki hiyo na wananchi ambao ni wateja.
Michezo iliyochezwa katika bonanza
hilo ni mpira wa miguu ambapo timu ya CRDB ilishinda baada ya kuifunga
timu ya Bunge penati tatu kwa moja na kwa upande wa mchezo wa mpira wa
pete timu ya Bunge iliibuka na ushindi baada ya kuibugiza CRDB magoli 35
kwa mawili.
Katika mchezo wa kuvuta kamba timu
ya Wabunge Wanawake na Wanaume waliibuka na ushindi baada ya kuzishinda
timu za CRDB. Upande wa mchezo wa basketball timu ya Bunge ilishinda
vikapu 53 kwa 51.
No comments:
Post a Comment