Tumepokea Maombi Mapya ya kuuza Mahindi Tani Milioni Moja kwenda Kenya – Naibu Waziri Mgumba
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba
akipata amelezo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa kwa upande wa ndani
kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)
Makao Makuu Bwana Iman Nzobonaliba kulia kwake na wengine ni Mkurugenzi
wa Uhifadhi Bwana Mikalu Mapunda na kushoto kwake ni Mhandisi Mgole
Chambili Msimamizi kutoka Kampuni ya Feruum
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba
akipata amelezo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa kutoka Mhandisi wa
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Makao Makuu Bwana Iman
Nzobonaliba kulia kwake na wengine ni Mtendaji Mkuu wa NFRA Bwana Milton
Lupa
Mafunsi wa Kampuni ya Feruum wakiendelea
na kazi ya kuunganisha vyuma vya ujenzi wa vihenge vya kisasa eneo la
Kizota Jijini Dodoma wakati wa ziara ya Naibu Waziri wa Kilimo Mhe.
Omary Mgumba alasiri ya leo
…………………………
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Omary Mgumba
amesema Serikali ya Tanzania imepokea maombi mapya ya kuuza mahindi
kwenda nchini Kenya yenye jumla ya Tani milioni 1.
Mhe. Mgumba ameyasema hayo wakati
alipofanya ziara ya gafla kwenye Ofisi za Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya
Chakula (NFRA – Makao Makuu) Jijini, Dodoma alipotembelea leo alasiri
ili kujionea maendeleo ya ujenzi wa vihenge vya kisasa vya kuhifadhia
chakula katika eneo la Kizota, Jijini Dodoma.
Naibu Waziri Mgumba amesema wakati
Serikali ikiwa kwenye hatua ya kuiuzia Zimbabwe kiasi cha mahindi Tani
laki saba (700,000) na tani laki moja (100,000) kwa mazao mengine ya
nafaka, Serikali ya Kenya imewasilisha ombi rasmi la kununua kiasi hicho
kutoka Tanzania.
Naibu Waziri Mgumba amesema huu ni wakati
muhafaka kwa Wakulima wa Tanzania kuchangamkia fursa ya kuuza chakula
cha ziada nje ya nchi na kwa bei nzuri ambayo italeta tija na maendeleo
na uchumi wao.
Aidha Mhe. Mgumba alidokeza kuwa amefanya
ziara hiyo lengo lake likiwa ni kujionea maendeleo ya ujenzi wa vihenge
vya kisasa (Silos) vya kuhifadhia mazao kwa lengo la kuongeza akiba ya
taifa ya chakula kwa Kanda ya Kati yenye kuhudumia mikoa ya Dodoma,
Singida kutoka uwezo wake wa sasa wa kuhifadhi, tani elfu thelasini na
tisa (39,000) hadi kufikia tani elfu hamsini na tisa (59,000).
Mradi wa ujenzi wa vihenge hivyo vya
kisasa, ulizinduliwa rasmi tarehe 24 Aprili, 2018 na Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na
ulianza rasmi Mwezi Juni 2018 huku Kampuni ya Feruum kutoka nchini
Poland ndiyo iliyoshinda zabuni ya ujenzi huo.
Akijibu swali la Mhe. Mgumba, Mhandisi wa
Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bwana Iman Nzobonaliba
amesema Mradi unataraji kuisha kwa wakati mnamo Mwezi Disemba 2019.
Akijibu swali la Naibu Waziri Mgumba
ambaye alitaka kufaham namna Wakala ilivyojianda kununua mazao ya
Wakulima katika msimu wa kilimo wa 2019/2020 Mtendaji Mkuu wa Wakala wa
Taifa wa Hifadhi ya Chakula Bwana Milton Lupa amemwambia Naibu Waziri
Mgumba kuwa NFRA imeanza zoezi la kununua chakula cha ziada kutoka kwa
Wakulima tangu tarehe 17 Juni 2019 katika Kanda ya Makambako na
Sumbawanga na kwamba kiasi cha shilingi bilioni 2.5 kitatumika kwa sasa.
Bwana Lupa amesema NFRA imejipanga
kutumia bajeti ya kiasi cha bilioni 15 pamoja na kuomba mkopo kutoka
Benki ya Kilimo wenye riba nafuu na kuongeza kuwa zaidi ya shilingi
bilioni 62.6 zitatumika kwa ununuzi wa nafaka kwa msimu wa kilimo wa
2019/2020.
Akizungumzia bei ya kununulia mahindi kwa
kilo, Mtendaji Mkuu amesema bei ya ununuzi itakuwa ikitofautiana kutoka
eneo moja na eneo linguine.
“Niseme tu kuwa tutaanza na bei ya
shilingi 400 hadi 500 kwa kila kilo moja ya mahindi lakini bei hii pia
itakuwa ikibadilika kutokana na sababu mbalimbali” Amekaririwa Bwana
Milton Lupa.
Naibu Waziri Mgumba ameongeza kuwa NFRA
ni Taasisi ya Serikali na imeaminiwa kusimamia jukumu la uhifadhi wa
chakula na kuwa Taifa linatarajia makubwa katika kuhakikisha Taifa
linakuwa na akiba ya chakula ya kutosha.
“Sisi kama Viongozi wenu, hatuna shaka na
uzoefu wenu na umahiri wenu katika nyanja ya uhifadhi wa chakula
hususan nafaka kama mahindi, endeleeni mbele na sisi tutahakikisha
mnapata mahitaji yenu, nawahakiki kuwa fedha za ununuzi mtazipata kwa
kuwa Wizara ya Fedha na Mipango imetuahidi kuwa zitakuja mapema kama
mlivyopanga” Amekaririwa Mhe. Mgumba
No comments:
Post a Comment