Wednesday, June 19, 2019

SERIKALI KUWEKA BAYANA MAJINA YA WAKANDARASI WABABAISHAJI

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa na Mhandisi wa Maji, Evaristo Mgaya kwenye eneo linapojengwa tenki la maji la Mradi wa Maji wa Itigi katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiongea kwa simu na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Nangai Engineering Ltd alipokuwa akikagua Mradi wa Maji wa Itigi, uliopo katika Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akimsikiliza Mhandisi wa Maji Halmashauri ya Itigi, Evaristo Mgaya kwenye moja ya vituo vya maji vinavyojengwa wakati akikagua Mradi wa Maji wa Itigi, uliopo katika Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Itigi, Rahabu Mwangisa.

Naibu Waziri wa Maji, Mhe. Jumaa Aweso akiwa kwenye kisima cha maji kilichopo eneo la Kanisani, moja ya visima 5 vya Mradi wa Maji wa Itigi, uliopo katika Halmashauri ya Itigi, wilayani Manyoni, mkoani Singida.

………………

Serikali imesema itaweka bayana majina ya makandarasi wote wanaoharibu miradi ya maji kwa kuitekeleza chini ya kiwango na kuwachukulia hatua kali za kisheria katika hatua ya kumaliza tatizo la utendaji mbovu kwenye kazi za miradi ya maji linalochangia wananchi kukosa huduma ya maji.

Naibu Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ametoa kauli hiyo mara baada ya kutoridhishwa na Mkandarasi wa Kampuni ya Nangai Engineering Ltd kufanya kazi kwa asilimia 30 ukilinganisha na kiasi cha Shilingi milioni 250 alizolipwa, wakati mkandarasi  wa Kampuni ya Nipo Africa Ltd akiwa amefanya kazi kwa asilimia 68 huku akidai fedha za malipo za ujenzi wa Mradi wa Maji wa Itigi uliopo katika Halmashauri ya Itigi, Wilaya ya Manyoni, mkoani Singida alipokuwa akikagua mradi huo.

‘‘Wakandarasi wababaishaji wa namna hii wote tutawaanika hadharani na watachukuliwa hatua kali za kisheria na Bodi ya Wakandarasi (CRB), Wakala wa Maji Vijijini (RUWASA) utakapoanza Julai Mosi, 2019 utakuwa ni mwisho wa wakandarasi wababaishaji kupata kazi za miradi ya maji ’’, amesema Aweso.

‘‘Serikali imelenga kufikisha huduma ya maji kwa wananchi, hatutakubali mkandarasi au mtu yeyote kukwamisha juhudi zetu za dhati za kumaliza tatizo la maji. Kuanzia sasa tutaorodhesa wakandarasi wote wasio na sifa na kuwafungia wasipewe kazi miradi yoyote ya maji nchini, ameelekeza Naibu Waziri.

Aidha, Aweso ameipongeza Kampuni ya Nipo Africa Ltd kwa kufanya kazi nzuri, akiahidi kuyafanyia kazi madeni yao na kuwalipa haraka. Pia, amewataka Wakurugenzi Watendaji wa Kampuni za Nangai Engineering Ltd na Nipo Africa Ltd kukutana nae siku ya Alhamisi Julai 20, 2019 kwenye kikao kitakaochuhusisha viongozi na wataalam wa Sekta ya Maji mkoani Singida kitakacholenga kukwamua mradi huo uweze kukamilika kwa wakati.

Wakati huo, Mkuu wa Wilaya ya Manyoni, Rahabu Mwangisa amemshukuru Naibu Waziri kwa ahadi yake ya kumlipa mkandarasi huyo na kumuahidi kuwa viongozi wa Wilaya ya Manyoni watasimamia mradi huo kwa ukaribu uweze kukamilika haraka.

Ujenzi wa Mradi wa Maji Itigi umeanza kutekelezwa mnamo 3/12/2018 na unategemewa kukamilika 2/9/2019 kwa zaidi ya Shilingi bilioni 2.6 ukihusisha uchimbaji wa visima 5 virefu vyenye uwezo wa kutoa jumla lita za ujazo 112,000 kwa saa, pamoja na ujenzi wa miundombinu ya maji.

Mradi huu utakapokamilika unatarajiwa kuhudumia vijiji 6 vya Songambele, Mlowa, Majengo, Tambukareli, Zinginali na Itigi unahusisha Mradi wa Maji wa Itigi  utakaogharimu zaidi ya Shilingi bilioni 2.6.

No comments:

Post a Comment