Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza umuhimu wa Sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya moja, wakati akifungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019.
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu,
(Watu wenye Ulemavu), Mhe. Stella Ikupa, akitoa hotuba wakati wa
mkutano wa kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya
ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo
mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni,
2019.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Mhe. Ummy Mwalimu, akisisitiza umuhimu wa Sekta za Afya kutumia Dhana ya Afya moja, wakati akiongea na Waandishi wa Habari mara baada ya kufungua zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019.
Mratibu wa Dawati la Afya Moja, Ofisi ya Waziri Mkuu, Harrison Chinyuka (wa kwanza kulia) akiwa katika chumba maalum cha Menejimenti ya Taarifa za zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, leo mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, tarehe 11 Juni, 2019.
*************************************
Kufuatia nchi za Kanda ya
Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya kuathirika na magonjwa ya mlipuko
kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya Ndege na Ebola, na kwa kuwa
magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi nyingine, Tanzania
kwa kushirikiana na Kenya wameanza kutekeleza zoezi la Kupima Utayari wa
nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa
ya mlipuko mipakani, lilofunguliwa leo mpakani mwa Tanzania na Kenya
kwenye eneo la Namanga, kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu.
Zoezi hilo, linazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha
sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo na mazingira katika
kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa yanayoathiri binadamu. Jumla
ya washiriki 150 ambao wanatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya
na Tanzania washiriki 130 kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika
mpaka wa Namanga; pamoja na nchi nyingine wanachama ambapo watakuwa
watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na Sudani Kusini
wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.
Akiongea leo tarehe 11 Juni, 2019, wakati wa Kufungua rasmi
zoezi hilo la siku nne, mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la
Namanga, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto,
Mhe. Ummy Mwalimu, amefafanua kuwa, serikali kupitia Wizara hiyo
inatumia zoezi hilo kufanyia majaribio ya utekelezaji wa Mipango ya
Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na kuwapa washiriki
fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza majukumu katika
kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na maafa ya
magonjwa ya mlipuko.
“Hapa nchini Tanzania tunalo
Dawati la Kuratibu masuala ya Afya Moja chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu,
kupitia Dawati hilo sisi kama wizara ya Afya tunasubiri tu ripoti ya
zoezi hili na tutaitekeleza mara moja. Utekelezaji wa ripoti hiyo
tutahakikisha unakuwa wa ufanisi na tija kwa nchi ili tuweze kusaidia
kuimarisha ushirikiano wa sekta za Afya hapa nchini kwa kuzingatia
dhana ya Afya moja.” Amesisitiza Waziri Ummy.
Aidha, Waziri Ummy, ameongeza
kuwa zoezi hilo linalenga kutathmini utaratibu wa kutumia kikosi cha
taifa cha dharura cha kukabili lakini pia kuhakiki matumizi ya maabara
zinazohamishika, kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa
ya mlipuko kwa vituo vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na
binadamu; kupima hatua za kujiandaa kukabiliana katika viwanja vya
kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Watu Wenye Ulemavu),
Mhe. Stella Ikupa, akiongea kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu) Mhe.
Jenista Mhagama, ameeleza kuwa Serikali kupitia ofisi hiyo, itaendelea
kuratibu sekta zote za Afya nchini kwa kutumia Dhana ya Afya moja, ili
kuhakikisha Afya za wananchi zinakuwa imara na salama kwa kudhibiti
magonjwa ya mlipuko ambayo yanaweza kusababisha maafa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega, akiongea kwa niaba ya Waziri wa
Mifugo na Uvuvi, Mhe. Luhaga Mpina, amebainisha kuwa, kwa kutambua
umuhimu wa Dhana ya Afya moja, Wizara inafahamu kuwa mifugo huwa ni
chanzo cha vimelea vya magonjwa ambayohuambukizwa binadamu,hivyo
serikali imeendelea kuboresha maabara za Mifugo nchini ili kuweza
kutambua vimelea kwa haraka na wakati ili visisababishe magonjwa ya
mlipuko kwa binadamu.
Naye, Waziri wa Afya wa Kenya,
Mhe. Sicily Kariuki, amebainisha kuwa zoezi hilo ambalo linahusisha
mlipuko wa virusi vinavyo shabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika
eneo la mpakani, ni muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa sekta za
Afya, kwa kuwa washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana
na ugonjwa huo kwakuzingatia Dhana ya Afya Moja.
Zoezi hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha
Kawaida cha Mawaziri wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
kilichofanyika mwezi Machi, 2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa Zoezi la Nadharia la kukabiliana na
magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa Tanzania na Kenya kwenye eneo la
Namanga.
Zoezi hilo ambalo linafanyika
mpakani mwa Tanzania na Kenya, kwenye eneo la Namanga, linaratibiwa na
Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi
wanachama kwa ufadhili wa Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.
No comments:
Post a Comment