Wednesday, June 12, 2019

SERIKALI KUENDELEA KUTEKELEZA MIKAKATI YA KUPIGA VITA UTUMIKISHWAJI DHIDI YA WATOTO

*****************************
Serikali imekua na mikakati mikubwa ambayo imesaidia kuwatoa Watoto katika suala zima la utumikishwaji katika kazi na mazingira mbalimbali. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Bungeni kuhusu maadhimisho ya siku ya kupiga vita utumikishwaji dhidi ya Watoto.
Waziri Mhagama alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imekua ikichukua hatua mbalimbali dhidi ya tatizo hilo.
“Jamii inatakiwa kutambua maana ya utumikishwaji wa Watoto na kazi hatarishi zinazowakabili ili kuwa walinzi wa watoto,” alisisitiza Mhagama. Aliongeza kuwa Watoto hawatakiwi kutumikishwa bali wasaidiwe kutimiza ndoto zao kwa kuwaandaa kuwa raia wema na wajenzi wa Taifa la kesho.
Alieleza juu ya Sheria na mikakati mbalimbali inayosimamia haki za Watoto ikiwemo Sheria ya elimu ambayo inataka Watoto wote kupata fursa ya elimu, Sheria Na. 1 (2009) ambayo inalinda haki na ustawi wa mtoto, Sheria Na. 6 (2004) ya Ajira na Mahusiano Kazini inelezea mazingira ambayo mtoto hatakiwi kutumikishwa kazi ambazo hazipo kwa mujibu wa taratibu.
Pamoja na hilo alielezea pia juu ya mpango ya taifa wa kupiga vita ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto ambao umesaidia katika kuwaondoa Watoto kwenye mazingira hatarishi na Mpango Mkakati wa taifa wa kupambana na ajira dhidi ya Watoto.
“Ofisi ya Waziri Mkuu inasimamia viwango vya kazi na imekuwa ikisisitiza waajiri kufuata sheria za kazi kwa kutowahusisha Watoto katika mazingingira hatarishi au kwenye kazi zisizo na staha ambazo zinafanya Watoto waingie kwenye utumikishwaji,” alisema Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa jamii kuwapa Watoto kazi zinazozingatia umri, ukubwa wa kazi na zinazolinda afya yao.

No comments:

Post a Comment