NAIBU WAZIRI OLE NASHA ATAKA WATOTO KULINDWA NA KUWEZESHWA ILI WAWEZE KUSHIRIKI FURSA MBALIMBALI ZA ELIMU
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku
ya Mtoto wa Afirika yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam Juni 20, 2019
Naibu Waziri wa Elimu,Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha,akichangia mjadala wakati wa maadhimisho ya
siku ya mtoto Afrika yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha akipokea risala kutoka kwa mmoja wa watoto
walioshiriki Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika Jijini Dar es
Salaam.
……………………….
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na
Teknolojia William Ole Nasha amesema Serikali inatambua na kuthamini
umuhimu wa mtoto wa kitanzania na ndio maana imekuwa ikizifanyia kazi
haki za msingi za mtoto ili aweze kuishi katika mazingira mazuri ikiwa
ni pamoja na kupata elimu.
Naibu Waziri Ole Nasha ameyasema hayo
Jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika
yaliyoandaiwa na Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Afrika
(WiLDAF) ambapo amesema watoto wanapaswa kulindwa na kuwezeshwa ili
waweze kushiriki katika fursa mbalimbali zilizopo kwenye elimu.
Amesema maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa
Afrika yanatoa fursa ya kujadili changamoto na fursa katika kuhakikisha
kuwa haki za mtoto zinalindwa na kwamba Serikali imefanya jitihada
kubwa na za makusudi katika kuhakikisha kuwa watoto wanapata haki zao za
msingi katika jamii zetu za kitanzania.
Ole Nasha amezitaja jitihada hizo kuwa ni
pamoja na kuridhiwa kwa mikataba mbalimbali ya Kimataifa inayolinda
haki za watoto, kutunga sheria zinazolinda haki za watoto dhidi ya
uonevu na ubaguzi wowote na pia imepitisha Sera zinazowalinda na
kuwapatia fursa watoto.
Jitihada nyingine ni pamoja na ujenzi wa
shule karibu na makazi ya watu ili kupunguza watoto kutembea umbali
mrefu, ujenzi wa mabweni na pia mafunzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na
kuweka mkazo juu ya stadi za maisha, elimu ya afya ya uzazi na ujinsia
katika shule za msingi na sekondari na vyuo vya ualimu.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri Ole
Nasha ameutaka umma kutambua kuwa jukumu la kuwaendeleza watoto kielimu
ni la kila mmoja wetu na kwamba ifahamike kuwa watoto wa kike na wa
kiume wote ni sawa, hivyo hatuna budi kuwapunguzia watoto wa kike mzigo
wa kazi za nyumbani ili wapate muda wa kujisomea sawa na ilivyo kwa
watoto wa kiume.
Siku ya Mtoto wa Afrika huadhimishwa Juni
16 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka 2019 maadhimisho hayo Kitaifa
yamefanyika Mkoani Geita na yalikuwa na Kauli Mbiu isemayo “Mtoto ni Msingi wa Taifa Endelevu: Tumtunze, Tumlinde na Kumuendeleza”.
No comments:
Post a Comment