Tuesday, June 11, 2019

Mgodi wa Namungo Ruangwa waifurahisha Tume ya Madini

Fundi Sanifu Mwandamizi Paulo Shauri wa kampuni ya Lindi Jumbo katikati akionyesha na kutoa maelezo kwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Kikula kulia kwake na Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma kushoto kwake kuhusu muundo na muonekano wake pindi utakapo anza kufanya kazi hapo mwakani mwezi August 2020.
Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula wa kwanza kushoto na Kamishna wa Tume ya Madini Prof. Abdulkarim Mruma wa pili kushoto, wakiwa kwenye mazungumzo na Mkuu wa Wilaya (DC) ya Nachingwea Rukia Muwango wa kwanza kulia na kulia kwake ni katibu tawala mkoa wa Lindi na Afisa madini mkazi mkoa wa Lindi kushoto kwa RC.
************************************
Na Issa Mtuwa (Wizara ya Madini) Rwangwa Mwenyekiti wa Tume ya Madini Prof. Idris Kikula na Kamishna wa Tume hiyo Prof. Abdulkarim Mruma wamefurahishwa na mgodi wa Namungo kwa namna unavyofanya kazi zake kwa utaratibu na mpangilio kiasi cha kutamka kuwa wanatamani migodi mbalimbali iende ikajifunze mgodini hapo.
Hatua hiyo inafuatia ziara waliyoifanya mgodi hapo kujionea uendeshaji wa shuguli za mgodi huo sambamba na kukagua na kusikiliza kero kutoka kwa wachimbaji wadogo, wakubwa na kati. Wakiwa mgodini hapo wameupongeza mgodi huo kwa namna wanavyowashirikisha wachimbaji wadogo na kuwapa umiliki wa 83% ya mapato yanayotokana na uzalishaji huku mgodi ukibakiwa na 17% ya kinacho zalishwa kitu ambacho hawajakikuta kwenye mgodi wowote hapa nchini.
Kutokana ushirikishaji wa wachimbaji wadogo, mgodi huo umekuwa ni wautofauti na migodi mingine kwani hakuna malalamiko hata kidogo kutoka kwa wachimbaji wadogo tofauti na maeneo mengine nchini ambapo kumekuwa na mivutano kati ya wachimbaji wadogo na wachimbaji wa kati na wakubwa.
“Niseme ukweli nimefika hapa nikiwa nimechoka na safari ndefu, lakini mara baada ya kupokea taarifa hii na kuwaona wahusika na hawajabisha kuhusu taarifa hii, kwa kweli nimepata nguvu sana, nyie ni mfano wa kuigwa, hiki mnachokifanya hakifanywi maeneo mengine sisi tunazunguka nchi nzima lakini nyie mnafanya kitu cha kipekee” amesema Prof. Kikula.
Aidha, wameupongeza mgodi kwa ulipaji wa maduhuli ya serikali kama inavyotakiwa huku akiwapongeza kwa utekelezaji wa shuguli za maendeleo ya jamii (Corporate Social Responsibility- CSR).
Akiwasilisha taarifa yake kwa mwenyekiti wa tume ya madini, Meneja wa mgodi wa Namungo Alfred Kimbi amesema kwa kipindi cha January – December 2018 mgodi huo ulizalisha gramu 54,920.30 yenye thamani ya Tshs. bilioni 4.302 na kuwawezesha kulipa mrabaha wa jumla ya Tshs. milioni 412,607,105, huduma za jamii (service levy) Tshs. milioni 19,290,596 mamlaka ya mapato (TRA) Tshs. milioni 156,577,270. Kwa mwaka 2019 kuanzia Januari hadi Mei mgodi umezalisha dhahabu gramu 16,671.5 yenye thamani ya jumla ya Tshs. bilioni 1.423 nakufanikiwa kulipa mrabaha na ada ya ukaguzi kiasi cha Tshs. milioni 99,599, 450.61, mgodi pia umelipa kwa TRA kiasi cha Tshs. milioni 51,142,000 katika kipindi hicho.
Kimbi ameongeza kuwa pamoja na ulipaji wa tozo hizo, kwa mwaka huu 2019 mgodi pia umelipa kodi nyingine kama vile kodi ya Mazingira milioni 5,000,000 Osha milioni 3,800,000 na ushuru wa Halmashauri milioni 21,880,990.
Kuhusu utekelezaji wa shuguli za maendeleo ya jamii, mgodi wa Namungo umetekeleza mirandi mbalimbali ya Elimu kwa baadhi ya shule ikiwa ni pamoja na kulipa walimu na wafanyakazi wengine, ujenzi wa madarasa , umefadhili ujenzi wa kisima cha maji katika kijiji cha Chingubwa chenye thamani ya Tshs. Milioni 13,000,000. Kwa upande wa afya mgodi unaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa Zahanati katika kijiji cha Chingumbwa mradi ambao utagharimu Tshs. 90,594,800. Kuhusu michezo mgodi umeshiriki kikamilifu kiasi cha kuiwezesha timu iliyopewa jina la mgodi huo “Namungo Football Club” kupanda daraja kufikia Ligi kuu kwa msimu ujao 2019/20.
Ziara hiyo iliyoanza tarehe 8/6/2019 katika mikoa ya Lindi na Mtwara leo 10/6/2019 iliendelea katika wilaya ya Nachingwea kwa Mwenyekiti na Kamishna kuzungumza na wafanyakazi wa tume hiyo mkoa wa Lindi kwenye ofisi za tume hiyo zilizopo Wilayani Nachingwea na baadae kufanya mazungumzo na Mkuu wa Wilaya hiyo Rukia Muwango kisha kuelekea wilaya ya Rwangwa ambapo walitembelea Soko la Madini, eneo la kampuni ya Ngwena Tanzania Ltd “Ngwena” inayojishugulisha na shuguli za utafiti wa madini ya Graphite na baadae kwenye kampuni ya Lindi Jumbo pia inayojishugulisha na uchimbaji wa madini ya Graphite yote ikiwa wilaya ya Rwangwa.

No comments:

Post a Comment