Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mhandisi
Kapuulya Musomba, akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu
maadhimisho ya miaka 50 ya TPDC.
................
Na Teresia Mhagama, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Maadhimisho ya Miaka 50 ya
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), yatakayofanyika kesho tarehe
31 Mei, 2019 jijini Dar es Salaam.
Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, tarehe 30/5/2019, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi
wa habari kuhusu maadhimisho hayo ambayo yataambatana na maonesho na utambuzi
wa watu mbalimbali waliotoa mchango uliofikisha Shirika katika hatua ya sasa.
Musomba amesema kuwa, Shirika la TPDC ambalo
lilianzishwa mwaka 1969 mwezi Mei, limefanya kazi mbalimbali za kuendeleza
sekta ya Gesi na mafuta nchini, na mwaka 1974 ndipo waligundua gesi kwa mara ya kwanza katika
visiwa vya Songosongo mkoani Lindi.
Ameeleza kuwa, ugunduzi wa Gesi umeendelea
kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini na sasa gesi iliyogundulika inafikia
kiasi cha futi za ujazo trilioni 57.54.
Amesema kuwa, licha ya utafiti wa Mafuta na Gesi, Shirika
hilo limeshiriki katika shughuli mbalimbali ikiwemo, miaka ya 1978/79 kushiriki
katika Vita vya Nduli Idd Amini, ambapo TPDC ilifanya kazi ya kupeleka mafuta
katika eneo la mapigano katika muda wote mpaka Tanzania iliposhinda vita hiyo.
Ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio mbalimbali
yaliyofikiwa na Shirika hilo, bado TPDC, imepanga kufanya shughuli mbalimbali
ikiwemo kufanya biashara ya mafuta kwa kuagiza mafuta hayo kutoka nje ya nchi
na kuleta nchini.
Pia ameeleza kuwa, kwa mwaka ujao wa fedha
2019/2020 wanatarajia kuchoronga kisima
cha utafutaji Mafuta na Gesi asilia katika kitalu cha Mnazi Bay Kaskazini kwa kuwa tafsiri za data zinaonesha
uwezekano wa kuwepo kwa Gesi asilia katika
Kitalu hicho.
Kuhusu usambazaji Gesi nchini, amesema kuwa kazi
hizo zimeanza katika mkoa wa Mtwara, Lindi, Dar es Salaam na Pwani na usanifu
unaendelea kwa ajili ya kusambaza gesi Tanzania
nzima.
Ameongeza kuwa, kazi ya usambazaji Gesi nchini
itafanywa na TPDC kwa kushirikiana na makampuni binafsi ili kuweza kufikisha
huduma hiyo kwa wananchi wengi zaidi.
Kuhusu uwepo wa Mafuta na Gesi nchini amesema kuwa,
zaidi ya nusu eneo la Tanzania lina uwezekano wa kupatikana Mafuta na Gesi na mpaka sasa eneo ambalo
limeshaangaliwa ni chini ya Theluthi moja.
No comments:
Post a Comment