SERIKALI KUENDELEA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAWEKEZAJI NCHINI
Waziri wa Nchi – Ofisi
ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe. Angellah Kairuki (Mb) akitoa neon la
ufunguzi wakati wa mkutano wake na wawekezaji wa Uingereza nchini
alipokutana nao Mei 29, 2019 katika Ukumbi wa Mikutano wa Coral Beach
Jijini Dar es Salaam ili kujadili masuala ya uwekezaji nchini.
……………………….
MWANDISHI WETU
Serikali imedhamiria kuendelea kutatua
changamoto zinazowakabili wawekezaji nchini ili kuhakikisha kunakuwa na
mazingira rafiki yatakayowavutia kuwekeza nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki
wakati akifungua mkutano wa wawekezaji wa Uingereza waliopo nchini
walipokutana kujadili masuala ya Uwekezaji uliofanyika Mei 29, 2019
katika Ukumbi wa Mikutano wa Coral Beach Jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Naibu Waziri
wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira
Mhe.Anthony Mavunde, Balozi wa Uingereza Nchini Mhe.Sarah Cooke pamoja
na Mwenyekiti wa Makampuni ya Biashara ya Uingereza Bw.Kalpesh Mehta,
viongozi wa makampuni ya uwekezaji nchini, pamoja na baadhi ya viongozi
wa Taasisi za Sekta ya Umma na Binafsi.
Akizungumza wakati wa mkutano huo, Waziri
Kairuki alieleza lengo la kukutana na wawekezaji kutoka Uingereza ni
pamoja na kujadili masuala yote yanayowahusu wawekezaji kwa kuzingatia
changamoto zinazowakabili na kuona namna bora ya kuzitatua ili kuendelea
kufikia lengo la kuwa na mazingira bora ya biashara na uwekezaji
nchini.
“Tumezingati umuhimu wa wawekezaji
nchini, hivyo tumekutana hii leo ili kusikiliza kero na changamoto
zinazowakabili ili kuona namna bora ya kuboresha mazingira na kutambua
fursa zilizopo nchini ili kuendelea kuwekeza nchini”, alisema Waziri
Kairuki.
Waziri aliongezea kwamba, kwa kuzingatia
kuwa mnamo mwezi Machi mwaka 2019 Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli aliutangaza mwaka huu kuwa ni mwaka wa
uwekezaji alipokutana na waheshimiwa mabalozi wa nchi za nje ambao wapo
nchini ikiwa ni kiashiria cha kufungua mwaka mpya.
Aliongezea kuwa, kwa kuzingatia mchango
wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi ikiwemo ongezeko la ajira hivyo
tunapaswa kuzingatia na kuboresha mazingira yatakayochochea kuendelea
kuchangia katika uzalishaji wa ajira nyingi nchini.
“Sekta binafsi ndiyo kiini cha ukuaji wa
uchumi kwa upande wa kuongeza ajira hivyo tunatambua mchango huo ambapo
hadi sasa wawekezaji wa uingereza wamechangia katika ukuaji wa ajira kwa
kuzalisha ajira laki tatu,”alisisitiza Waziri Kairuki.
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza
Nchini Mhe.Sarah Cooke aliipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuona
umuhimu wa kukutana pamoja kujadili masuala ya uwekezaji na kuendelea
kujadili namna ya kuwezesha wawekezaji kutoka uingereza kuendelea kuwa
wadau muhimu nchini na kuhakikisha nchi zote mbili zinanufaika.
“Ni kweli tumeenedelea kuwekeza Tanzania
kwa kuzingatia mazingira yaliyopo hivyo ni vyema kukawa na maboresho
zaidi katika mazingira hayo kwa kuendelea kutatua changamoto zilizopo
kwa sasa ili tuendelea kushirikiana pamoja,” alieleza Balozi.Cooke
Aliongezea kuwa nchi ya Uingereza
imelenga kuwa kinara cha uwekezaji katika nchi za Afrika hiyo ni wakati
sahihi wa kuendelea kutumia fursa zilizopo barani humo ili kufikia
malengo.
“Ifikapo mwaka 2022 Nchi yetu imeweka
malengo ya kuwa wawekezaji bora barani Afrika hivyo tunaendelea
kushirikianana nchi za Afrika ili kuwa na nia moja na kuwa na mahusiano
yenye tija hasa katika masuala ya uwekezaji”,alisema Balozi Cooke.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde
alieleza kuwa, Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya biashara ili
kuchangia ongezeko la ajira kwa vijana wa Kitanzania ili kujikwamua
kiuchumi.
Aidha alifafanua kuwa, ili kuendelea
kukuza ujuzi kwa vijana na kuondokana na changamoto za ukosefu wa ajira
Serikali itaendelea kulinda ajira za watanzania na kuboresha mazingira
ya sekta binafsi ambao ni wadau muhimu katika kuzalisha ajira nchini.
No comments:
Post a Comment