Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Watendaji wa Tume ya
Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019. Kushoto ni
Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na wa tatu kulia ni Waziri wa Maji na Umwagiliaji,
Profesa Makame Mbarawa. Wa pili Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo,
Mhandisi Mathew Mtigumwe na kulia ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya
Umwagiliaji, Eliakim Chitutu.
Baadhi ya Watendaji wa Tume ya Umwagiliaji wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Mei 14, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga mara baada ya kikao cha Watendaji wa Tume ya Umwagiliaji kwenye ukumbi wa Hazina jijini
Dodoma, Mei 14, 2019.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa
amewasimamisha kazi Wakurugenzi saba wa Tume ya Umwagiliaji akiwemo Kaimu
Mkurugenzi Mtendaji wa tume hiyo ili kupisha uchunguzi wa tuhuma mbalimbali
zinazowakabili.
“CAG afanye haraka uchunguzi wa kina,
tunataka kujua ni nani alikuwa mlango wa ubadhirifu huu. Hatutamuonea mtu, wote
watakaothibitika kuhusika na matumizi mabaya ya fedha watachukuliwa hatua.”
Waziri Mkuu amechukua hatua hiyo leo
(Jumanne, Mei 14, 2019) wakati wa kikao na viongozi wa tume hiyo kilichofanyika
kwenye Ukumbi wa Hazina, jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mawaziri, Manaibu
Waziri na Makatibu Wakuu.
Mbali na kuwasimamisha kazi wakurugenzi
hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi wengine 21 wa tume hiyo wachukuliwe
hatua za kinidhamu kutokana na utendaji usioridhisha kwenye miradi mbalimbali
inayosimamiwa na tume hiyo.
Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua
hatua hiyo kutokana na udhaifu wa kiutendaji ndani ya tume hiyo ikiwemo
matumizi mabaya ya fedha za miradi, rushwa, matumizi mabaya ya madaraka,
upendeleo na kukosa umakini. “Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya ubadhirifu
uliofanyika katika miradi ya umwagiliaji.”
Amesema hali ya kilimo cha umwagiliaji
nchini hairidhishi na Serikali haijafurahishwa na utendaji wa Tume ya
Umwagiliaji licha ya kuwekeza nguvu kubwa, hivyo inataka kuona mabadiliko.
“Miradi mingi inayotekelezwa na Tume ya
Umwagiliaji nayo ina hali mbaya zaidi. Miradi mingi ya tume hiyo imejikita
katika mafunzo, semina na warsha badala ya kujenga na kuendeleza skimu za
umwagiliaji.”
Waziri Mkuu amesema tume hiyo
imeshindwa kusimamia miradi takribani 10 katika maeneo mbalimbali nchini na
kusababisha sekta ya umwagiliaji kushindwa kupata mafanikio yaliyotarajiwa
kutokana na ubadhirifu.
Miongoni mwa miradi hiyo ni pamoja na
mradi wa umwagiliaji wa Luiche unaokadiriwa kumwagilia hekta 3,000 ambao upo
katika hatua za awali za utekelezaji lakini tayari pamekuwepo na matumizi mabaya
ya fedha za mradi.
“Kaimu Mkurugenzi Mkuu alitoa kibali na
kulipa fedha taslimu masurufu ya jumla ya sh. milioni 100.7 kwa Wahandisi wa
Makao Makuu, Maafisa wa Idara ya Mipango, Tathmini na Ufuatiliaji kwenda
kufanya ukaguzi badala ya kujenga. Mkaguzi wa nje alihoji uhalali wa
malipo hayo na hajapata majibu hadi leo.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amemuagiza Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga akamilishe mchakato wa kuwapata
wajumbe wa bodi wa tume hiyo ambayo imemaliza muda wake.
Pia amemtaka Waziri huyo ahakikishe Wizara
ya Kilimo inaisimamia tume kukamilisha ujenzi wa skimu zote za umwagiliaji
zilizoanza kujengwa miaka ya nyuma zikiwemo za wakulima wadogo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza
Waziri wa Kilimo afanye mabadiliko ya muundo wa tume hiyo na kuwa na maafisa wa
umwagiliaji katika ngazi za mikoa na wilaya ili kusogeza huduma kwa wananchi.
Awali, Waziri wa Kilimo alisema skimu
zinazofanya kazi hazizidi 10 kati ya 2,678 hali iliyosababishwa na kuwepo kwa
dosari katika usimamizi na pia matumizi ya fedha za miradi katika Tume ya
Umwagiliaji si mazuri.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji
Profesa Makame Mbarawa alisema miradi mingi ya umwagiliaji ilifeli kwa sababu
ya ilijengwa chini ya kiwango hususani mabwawa na pia haikuwa ikilingana na
kiasi cha fedha kilichokuwa kinatolewa. “Mradi wa kutumia sh. bilioni mbili
wanatumia sh. bilioni nne.”
Kikao hicho kimehudhuriwa na Waziri wa
Maji Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, Naibu Waziri wa
Nchi OR-TAMISEMI, Mwita Waitara, Naibu Waziri wa Kilimo, Omar Mgumba, Naibu
Waziri wa Kilimo Innocent Bashungwa, Makatibu Wakuu wa Wizara hizo pamoja na
maofisa wengine wa Serikali.
No comments:
Post a Comment